Zuchu afungiwa kufanya shughuli za sanaa Zanzibar

Zuchu afungiwa kufanya shughuli za sanaa Zanzibar

Unguja. Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni la Zanzibar, limemfungia msaanii wa kizazi kipya Zuhura Othman Masoud maarufu Zuchu kuendesha shughuli zote za sanaa visiwani hapa.

Mbali na kumfungia kuendesha shughuli za sanaa, pia imepiga marufuku redio na televisheni za Zanzibar kupiga nyimbo zake zote kwa kipindi cha miezi sita.

Hatua hiyo imekuja baada ya tukio la Februari 24 mwaka huu Zuchu wakati akitumbuiza katika usiku wa Fullmoon Kendwa Mkoa wa Kaskazini Unguja kudaiwa kuimba nyimbo, kutoa matamshi na kuonyesha ishara mbaya ambazo ni kinyume na maadili ya kizanzibari.

Akizungumza leo Machi 5, 2024 ofisini kwake na waandishi wa habari, katibu mtendaji wa baraza hilo, Omar Abdalla Adam amesema baraza limemfungia kwa kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.

“Baraza lina wajibu wa kusimamia mila, silka desturi na utamaduni wa Mzanzibari, kwa hiyo linatamka rasmi kumfungia msanii Zuhura Othman Soud (Zuchu) kufanya shughuli yoyote ya sanaa kwa Zanzibar kwa kipindi cha muda wa miezi sita kuanzia leo Machi 5, 2024,” amesema.

Amesema wanafanya hivyo kutokana na tabia yake kuimba nyimbo ambazo hazina maadili, hazifuati misingi na hazina afya njema kwa jamii ya Wazanzibari.

Pia, amesema licha ya msanii huyo kutokuwa na usajili Zanzibar lakini amekuwa akiendesha shughuli zake za sanaa bila kupata kibali.

Mbali na adhabu hiyo, pia msanii huyo ametakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni moja kwa Baraza la Sanaa na aandike barua ya kuomba radhi na kuthibitisha kwamba hatafanya kosa hilo ndani ya kipindi alichofungiwa.

Amesema iwapo akishindwa kufanya hayo zuio lake litaendelea kwa muda usiojulikana.

Amesema wanafanya hivyo ili iwe fundisho kwa wengine kwa wasanii wa Zanzibar na wajue kuna taratibu, sheria na kuna mambo yanatakiwa kuzingatia katika kazi ya sanaa.

“Tunaomba jamii ya Wazanzibari wampuuze na wasisikilize nyimbo zake zote na vyombo vya habari wasipige kabisa nyimbo zake,” amesema.

Amesema kabla ya kuchukua hatua hiyo walimuita lakini alikaidi wito huo hivyo wakaamua kuchukua hatua hizo za awali na akiendelea atachukuliwa hatua kali zaidi.

Mrajisi wa Baraza la Sanaa, Juma Chum Juma amesema wana wajibu wa kuwasimamia na kuwakuza wasanii, lakini inapotokea kuvuka mipaka lazima kuchukua hatua.

“Ule mchezo alipindukia kwa Zanzibar, inawezekana pengine angekuwa nje ya Zanzibar sawa, lakini pia kuna matamshi, ishara za mbele na nyuma alikuwa anonyesha na mengine huwezi kuyasema lakini sisi wachambuzi wa sanaa na watu wa lugha tumejua alichokusudia,” amesema.

 “Ukienda kwenye sheria ibara ya nane kifungu kidogo cha kwanza (1), mtu anapofanya kitendo kisicho cha kawaida kwenye stage basi tunachukua hatua.”

Amesema wanalazimika kwenda mbali zaidi, kipingele namba 23 (b) kinawataka kuchukua hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kumfungia.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories

Popular
Swahili News Editor

MGAO WA MAJI WAWATESA WAZANZIBARI

Wananchi wengi hasa katika maeneo ya Mjini Unguja, wanalalamikia ukosefu wa maji safi na salama huku Mamlaka ya Maji Zanzibar ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ujuzi na wataalam katika masuala ya uandisi wa Maji na fani nyengine.Continue Reading