Kigoma. Chama cha ACT Wazalendo kimeweka wazi mpango wa kuhakikisha katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kinampa nafasi Zitto Kabwe kuwa Rais wa Tanzania na Masoud Othman kushika wadhifa huo visiwani Zanzibar.
Kabwe ambaye ni kiongozi mstaafu wa chama hicho, mara kadhaa amesikika akitangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo la Kigoma Mjini alilowahi kuliongoza mwaka 2015 hadi 2020.
Lakini, mwanasiasa huyo pia amewahi kuweka wazi nia yake ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2025, ingawa baadaye alibadili msimamo akiutaka ubunge wa Kigoma kwa kile alichoeleza analenga kwenda kuweka mambo sawa bungeni.
Kwa upande wa Othman ambaye kwa sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliushika wadhifa huo akimrithi Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki Februari mwaka 2021.
Hayo yameelezwa mkoani Kigoma leo Jumapili Mei 5, 2024 na Kabwe katika mkutano wa hadhara uliofanyika kuhitimisha sherehe za kuadhimisha miaka 10 ya kuzaliwa kwa ACT Wazalendo.
Mkakati wa Kabwe
Katika hotuba yake, mwanasiasa huyo aliyestaafu uongozi wa juu ndani ya chama hicho, amesema yupo tayari kwa kila namna na wakati wowote kuwa Rais wa Tanzania.
Uamuzi wake wa kuingia katika kinyang’anyiro hicho, amesema utatokana na matakwa ya wananchi.
“Nataka niwaambie na nataka nimwambie ndugu Jussa, nimejiandaa kisaikolojia, kiakili na kimaarifa, kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa hiyo wakati wowote mkinihitaji hatuna shida ya Jimbo hapa vijana wapo tunaweza kumleta yeyote agombee,” amesema. Mzizi wa kauli hiyo ya Kabwe ni hoja iliyoibuliwa na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa aliyesema mwaka 2025 wanamtaka mwanasiasa huyo awe Rais wa Tanzania.
“Adhma ya ACT Wazalendo ni Rais wa awamu ya saba wa Tanzania awe Zitto Kabwe,” amesema huku akiahidi kuhakikisha Othman anakuwa Rais kwa upande wa Zanzibar.
Katika mwendelezo wa hotuba yake, Kabwe amesema pamoja na kuweka msingi kwa miaka 10, bado chama hicho hakijatimiza lengo lake.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini, miaka 10 ijayo ni kwa ajili ya chama hicho kushika dola na kuleta mabadiliko serikalini.
Amegusia safari ya chama hicho, akisema kilianza kwa kuitwa cha watu wa Kigoma, lakini sasa kimeenea kila kona ya Tanzania na viongozi wake ni kielelezo cha hilo.
“Kiongozi wa chama ni mtu wa Kilimanjaro, Mwenyekiti ni mtu wa Pemba, Makamu Mwenyekiti Bara ni mtu wa Lindi, Makamu Zanzibar ni mtu wa Unguja, Katibu Mkuu mtu wa Tunduru.
“Wanachama mjivunie mbegu mliyoipanda kwa miaka 10 iliyopita kwa sasa imeenea Tanzania nzima mnapaswa kutembea kifua mbele,” amesisitiza.
Mkakati wa Othman
Katika hotuba yake, Jussa amesema mwaka 2025 atahakikisha Othman anakuwa Rais wa Zanzibar.
Amesisitiza ahadi yake kwamba atakabidhi Serikali itakayotokana na chama hicho katika uchaguzi wa mwakani.
“Othman atakuwa Rais wa Zanzibar mwaka huo,” amesema.
Hata hivyo, ahadi hiyo imeonekana kupokelewa vema na Othman aliyesema pamoja naye katika uchaguzi huo, Kabwe anapaswa kuwa Rais wa Tanzania.
“Mungu akipenda 2025 tunataka tushindane na Kigoma, mkikabidhiwa Serikali kule huku Kigoma pia mtukabidhi kwa sababu ng’ombe hachinjwi mkiani,” amesema.
Amesema kufanya hivyo kutawezesha kupatikana kwa uongozi bora na kuuondoa ule aliodai umeshindwa kusimamia vema rasilimali za nchi.
Ameielekeza hotuba yake hiyo katika hoja kuwa, Tanzania ina rasilimali nzuri isipokuwa imekosa viongozi bora.
Othman amesema hilo lipo hata Kigoma, Mkoa ambao umejaa rasilimali, lakini wenyewe umebaki kuwa masikini.
“Unaweza kuwa hodari na madhubuti, lakini ukiwa na dereva mbovu hutafika mjini,” amesema.
Amesema ni muhimu kubadili dereva ili kuweka mambo yote sawa.
Lakini, amesema haitawezekana kumbadilisha dereva iwapo wananchi hawataamua kupitia uchaguzi wa mwaka 2025.
Amesisitiza ili kuepuka ya mwaka 2020 na udhalimu ni vema kuwa na Katiba Mpya itakayowapa wananchi haki na uhuru wa kuchagua.
Amesema kabla ya Katiba Mpya, lazima itangulie kupatikana tume huru ya uchaguzi itakayosimamia maoni ya wananchi.
Katika ufunguzi wa mkutano huo, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Kizza Mayeye ameielekeza hotuba yake kwa kutaja changamoto tano zinazoufanya mkoa huo uwe mahali pagumu pa kuishi.
Kwa mujibu wa Mayeye, Serikali mkoani humo imezuia matumizi ya Ziwa Tanganyika kwa madai ya upungufu wa samaki, akisema kitendo hicho kinaumiza wananchi.
Amesema Serikali inafanya hivyo ilhali tegemeo kubwa la maisha ya wananchi wa Mkoa huo ni shughuli za uvuvi.
Mwenyekiti huyo ameeleza hatua hiyo imewafanya wananchi wakose uhakika wa milo mitatu, kadhalika wazazi kushindwa kuhudumia familia.
Amesisitiza kitendo hicho ni kukosa huruma dhidi ya wananchi na kwamba ACT Wazalendo haiungi mkono.
“Sisi hatuungi mkono ufungaji wa ziwa kwa sababu unahatarisha maisha ya wananchi wa Kigoma,” amesema.
Lingine alilolitaja kuwa changamoto kwa wananchi hao ni usumbufu wa kushukiwa uraia wao.
Kinachosababisha usumbufu huo, amesema ni Mkoa huo kupakana na nchi jirani.
“Maisha ya wananchi wa Kigoma ni magumu, tunashukiwa kutokuwa raia, hili linafanya tuishi kwenye ardhi yetu bila amani,” amesema.
Kwa mujibu wa Mayeye, pamoja na uwepo wa vyanzo vya maji katika Mkoa huo, bado wananchi wa Kigoma hawana uhakika wa maji safi na salama.
Hata hivyo, Mayeye amesema Suluhu ya changamoto hiyo ni wananchi kuchagua viongozi kutoka katika chama hicho katika chaguzi zijazo.
“Mkoa huu ndiyo ngome ya chama hiki, tutashinda uchaguzi wa Serikali za mitaa, Uchaguzi Mkuu kwa maana majimbo ya kutosha, madiwani na wabunge,” amesema.
Pamoja na hilo, amesema matamanio ya wananchi ni kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi isiyoishia kwenye nyaraka pekee, bali iwe na uhalisia.
“Hatutaki kuwa na tume huru lakini bado tunaendelea kukamata kura za wizi katika chaguzi,” amesema.
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama hicho, Abdul Nondo amegusia dalili ya kuendelea kwa changamoto katika chaguzi zijazo.
Hisia zake hizo zinatokana na kile alichoeleza, bado mabadiliko ya sheria yanaikingia kifua tume ya uchaguzi iliyoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan iendelee kubaki madarakani.
Msimamo wa chama hicho kwa mujibu wa Nondo, ni kujiuzulu kwa watendaji hao na kamati ya usaili itekeleze wajibu wake kama sheria mpya inavyoeleza.
“Sisi tunataka ahadi ya Rais Samia kwamba atafanya mabadiliko ya siasa, tuone anatekeleza kwa vitendo na sio maneno tupu,” amesema.
Ushahidi wa kutoimarika kwa mifumo ya uchaguzi, amesema kumeshuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa Kasingilima ambao dhuluma imeendelea kufanywa.
Source: mwananchi.co.tz