Dar es Salaam. Ikiwa imebaki miezi minne kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amehoji kutotolewa kwa kanuni za uchaguzi huo hadi sasa ukiwa umebaki muda mfupi.
Mbowe amehoji hayo leo Jumatano, Mei 8, 2024 jana jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa kitaifa wa kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja, juu ya sheria za uchaguzi zilizopitishwa kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, John Mongella, mbunge wa Kilosa ambaye alikuwa mwakilishi wa CCM, Profesa Palamagamba Kabudi na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Bara), Issihaka Mchinjita.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chassot.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbowe amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakijadili masuala yaleyale, lakini hamna suluhisho la maana lililopatikana kwa sababu Serikali ya CCM haina dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli.
Amesisitiza hata sasa wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, bado Serikali kupitia Ofisi ya Rais (Tamisemi) ambayo ndiyo inaratibu uchaguzi huo, haijatoa kanuni hizo kwa wadau ambao ni vyama vya siasa.
“Tunakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, miezi minne ijayo, hatujui kanuni, sisi ni players (wadau). Wanaojua ni Serikali na Chama cha Mapinduzi, wanahodhi kila process (mchakato), kila kitu. Hivi mmeshindwa nini kuwashirikisha wadau kwenye hizo process.
“Unakwenda kwenye uchaguzi, hujui kanuni zinatoka lini, zikitoka zitatoka na nini. Wanaotengeneza ni wao, wanaosimamia ni wao, wanaokwenda kuchezesha ni wao…chama ambacho kitajizatiti kusimamisha wagombea, kuna wagombea zaidi ya 400,000 nchi nzima, hawa watu unawaandaaje, katika muda upi,” amehoji.
Kauli ya Tamisemi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa akizungumza na Mwananchi Digital amesema, kanuni hizo zitakuwa shirikishi na zinakwenda ka ratiba za uchaguzi.
“Tamisemi hatutakurupuka, kanuni hizi ni za wadau wenyewe, wao wenyewe ndio wataziandaa na sisi ni wasimamizi tu, kama ambavyo Rais amekuwa akisisitiza anataka ushirikishwaji na sisi tutafanya hivyo,” amesema.
Waziri huyo amesema uchaguzi unakwenda na ratiba: “Na ratiba ya huu uchaguzi ilianza tangu Oktoba mwaka jana inakwenda hadi Novemba mwaka huu na tuko ndani ya muda. Nisisitize tu kanuni hizi ni za kwao, tutawashirikisha muda ukifika.”
Mwananchi Digital lilipotaka kujua hasa lini watashirikishwa hasa ikizingatiwa imebaki miezi michache, Waziri Mchengerwa amesema: “Hivi karibuni tutawashirikisha.” Amewaomba wadau kutokuwa na wasiwasi na wao kama wasaidizi wa Rais watahakikisha wanaishi maoni yake (Rais) kupitia 4R.
“Kanuni zinazoandaliwa ni za Watanzania wote na zina uratibu kama zinavyoandaliwa na sheria. Ndani ya Serikali tumeshamaliza, sasa tunaendelea na taratibu za wadau na mchakato utakuwa wazi kwa sababu Rais anaamini katika demokrasia, ili kuleta mshikamano wa Taifa,” amesema.
Walichosema wadau
Kwenye mkutano huo wa TCD, Mbowe ameeleza kuwa walitoa maoni kuhusu ushirikishwaji wa vyama kwenye michakato mbalimbali, wakapendekeza uwakilishi wa vyama kwenye Tume ya Uchaguzi hata kama siyo makamishna, bali hata watazamaji ili wajue ile michakato ndani ya tume.
“Sisi kama wadau, hatujui masanduku ya kura yanaagizwa kutoka wapi, hatujui karatasi za kura zinaagizwa kutoka wapi. Uchaguzi uliopita, kuna kura zilichapishwa nje ya nchi, kuna kura zilichapishwa Dar es Salaam, ambazo zilikwenda kuwekwa kwenye masanduku, tumeona kwa macho.
“Hatushirikishwi Tume inapata wapi vifaa vyake, mifumo ya Tehama inayotumiwa na Tume ku-tally (kujumlisha kura), kutuma matokeo, inatoka katika nchi gani? Tuna-access gani ya kujua hiyo mifumo kama wadau muhimu? Hakuna vitu kama hivyo, na vyote hivyo tulijadili kwenye maridhiano,” amesema.
Amesisitiza kwamba mabadiliko yaliyofanyika kwenye sheria za uchaguzi ni urembo, kwani hazijatibu kiini cha tatizo. Alisema viongozi wamekuwa wakitoka na kauli nzuri kwamba kutakuwa na tume huru na uchaguzi huru, lakini mifumo haiakisi kauli hizo.
Mbowe amesema bado Taifa halijafanikiwa kufanya mabadiliko ya msingi ambayo yatasaidia kuwa na uchaguzi ambao angalau utakuwa wa kuaminika. Hata hivyo alisisitiza kwamba muda bado upo kama kuna utashi wa kisiasa.
Akisisitiza hoja hiyo, Makamu Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, Joseph Selasini ameeleza kushangazwa hadi sasa na kanuni kutowekwa mezani, kwani lazima zipitie mchakato wa kujadiliwa na wadau kisha kupitishwa.
“Tunaomba mambo yasifanyike kwa kuviziana, kimagumashimagumashi, sasa uchaguzi ni Septemba, kama mambo yataenda kama yalivyopangwa kwenye kalenda yao, sasa hii ni Mei, hadi sasa hivi kanuni hazijatolewa ili wadau watoe mawazo yao, wazijadili.
“Hakuna elimu yoyote inayotolewa kwa wapigakura, huko vijijini watu hata hawajui kama kuna uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu. Kwa hiyo inaonekana ni mtindo uleule wa kuviziana, tunaitaka Ofisi ya Rais (Tamisemi) iweke utaratibu wa zamani wa kutoa rasimu ya kwanza, wadau waitwe watoe maoni yao, ndiyo itengenezwe rasimu ya pili,” amesema Selasini.
Hata hivyo, Selasini amehoji kwamba Sheria ya Tume ya Uchaguzi iliyopitishwa na Bunge inaeleza uchaguzi wa Serikali za mitaa utasimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi, lakini sasa Tamisemi wanaandaa kanuni, maana yake wanakwenda kinyume na sheria hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa amesema sheria imetungwa kwa kuchelewa na walitarajia kwamba kanuni zitawahi lakini hadi sasa bado hazijatoka.
“Sisi tunatoa wito kwamba hili jambo lifanyike haraka kwa sababu kanuni zikiwa na upungufu wowote, lazima hayo yajulikane mapema ili hatimaye marekebisho yaweze kufanyika,” amesema Ngulangwa.
Amesisitiza kusiwe na mpango wowote wa kuzuia uchaguzi huru na wa haki, na kwamba kama wamebadilisha jina la Tume ya Uchaguzi, basi na mchakato mzima wa uchaguzi, uonekane kuwa huru na wa haki ili maoni ya Watanzania yaheshimiwe.
Hofu hiyo ya wadau inashabihiana na ile aliyoitoa Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba aliyesema makundi mawili yanayosigana juu ya uhuru na haki katika chaguzi zijazo, yanapaswa kukutana na kukubaliana kwanza kabla ya kuingia kwenye uchaguzi.
Jaji Warioba akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili Aprili 15 mwaka huu, alisema yaliyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020, yamevifanya vyama vya upinzani kupoteza imani na kuzidisha hofu kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na haki.
Jaji Warioba katika maelezo yake alitolea mfano kwenye uchaguzi uliopita wa madiwani katika kata 23 uliofanyika Machi 22 mwaka huu akisema ni dalili kama hizo za mwaka 2019 na 2020 zimeanza kujitokeza katika uchaguzi mdogo wa madiwani.
“Tumeanza kuona dalili. Hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa.”
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana akizungumza na wana-CCM wa Mkoa wa Dodoma alisema Serikali itahakikisha michakato ya uchaguzi inakuwa huru na ya haki.
Sheria za uchaguzi
Mwakilishi wa CCM kwenye majadiliano hayo, Profesa Kabudi amesema tangu uchaguzi wa mwaka 1958 hadi sasa, hatua kubwa imepigwa kwenye masuala ya uchaguzi kwani wakati huo masharti yalikuwa mengi ikiwemo mgombea kutakiwa kujua kuzungumza lugha ya Kiingereza.
Amesema kila nchi inapitia milima na mabonde, hivyo jambo la msingi ni kujifunza kwa yale yanayotokea na kusonga mbele. Hata hivyo, alisema CCM imepokea maoni yaliyotolewa na wadau kwani ni ya msingi.
“Yapo mambo ambayo lazima yafanyiwe kazi baada ya mwaka 2030, sasa haya lazima yajadiliwe. Tujenge tafakuri ya pamoja na kusonga mbele. Yapo mengi ya kufanyiwa kazi lakini hapa tulipofika, hatua kubwa imepigwa,” amesema.
Mbunge huyo wa Kilosa, amesisitiza kuna haja ya watu kujadili pia mfumo wa uchaguzi badala ya kujikita kwenye tume pekee huku akihoji kama mfumo wa sasa wa mwenye kura nyingi ndiyo mshindi (FPTP) unafaa kwa nyakati za sasa.
“Tunatumia muda mwingi kujadili kuhusu vyombo vya uchaguzi (tume) lakini tunasahau kujadili mfumo wa uchaguzi. Huu mfumo tulionao wa FPTP, unatufaa?” amehoji Profesa Kabudi wakati wa mkutano huo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Issihaka Mchinjita amesema kutungwa kwa sheria hizo bila kufanyika kwa mabadiliko madogo ya Katiba, hakuna maana kwa sababu sheria zinaakisi Katiba.
Akizungumzia Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Mchinjita amesema imebainisha upatikanaji wa wajumbe wa Tume hiyo, hivyo chama chake kinapendekeza wajumbe waliopo sasa wajiondoe kama sheria haijawapa nafasi hiyo.
“Sheria hizi zimejaribu kuweka msingi mdogo lakini bado hazijakidhi matarajio ya wadau. Tunahitaji kufanya mabadiliko makubwa ya kikatiba,” amesema Mchinjita wakati wa majadiliano hayo yaliyowaleta pamoja wadau mbalimbali.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael battle amesema vijana wana nguvu ya kubadilisha mustakabali wa nchi hii kwa sababu vijana ni nguvu. Alisisitiza umuhimu wa kujifunza demokrasia kila siku kwa maendeleo ya nchi.
“Marekani siyo mwalimu wa Tanzania katika demokrasia, wala Tanzania siyo mwalimu wa Marekani, tunajifunza pamoja,” amesema Balozi Battle.
Source: mwananchi.co.tz