Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu Watanzania 56 kulipa faini ya Sh50,000 kila mmoja au kwenda jela miezi mitatu, baada ya kupatikana na hatia ya kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu za uhamiaji.
Wamehukumiwa adhabu hiyo katika kesi ya jinai namba 9930/2024. Wote wamelipa faini.
Hukumu imetolewa jana Jumatano Aprili 17, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Gwantwa Mwankuga baada ya washtakiwa kukiri kosa na mahakakama kutiwa hatiani kwa kosa hilo.
Hakimu Mwankuga amesema washtakiwa wametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa na wamekiri shtaka lao, hivyo anawahukumu kila mshitakiwa kulipa faini Sh50,000 na wakishindwa kulia watatumikia kifungo cha miezi mitatu jela kila mmoja.
Awali, wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Raphael Mpuya akishirikiana na Wakili Ezekiel Kibona, waliwasomea washtakiwa mashtaka.
Wanadaiwa Aprili 11, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wilayani Ilala walitenda kosa hilo.
Inaelezwa washtakiwa wakiwa raia wa Tanzania, waliondoka isivyo halali nchini kueleleka Afrika Kusini.
Baada ya kusomewa shtaka walikiri kutenda kosa ndipo upande wa mashtaka ulipowasomewa hoja za awali.
Mpuya alidai kwa nyakati tofauti waliondoka nchini bila kufuata utaratibu, bila kuwa na hati ya kusafiria au nyaraka yoyote na pia walishindwa kupita kwenye mipaka rasmi iliyoainishwa na sheria za uhamiaji ikishirikiana na Serikali ili kujua madhumuni ya safari zao.
Wanadaiwa kuingia Afrika Kusini isivyo halali wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Alidai baada ya kurejeshwa nchini na kuhojiwa na Uhamiaji, washtakiwa walikiri kuondoka nchini wakiwa hawana hati za kusafiria, hivyo walifikishwa mahakamani.
Wakili Mpuya, baada ya kuwasomea maelezo alidai upande wa mashtaka hauna rekodi za makosa ya nyuma dhidi ya washtakiwa. Aliiomba Mahakama itoa adhabu ili iwe fundisho kwa vijana wengine.
“Tunaiomba Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye nia ovu wanaoenda Afrika Kusini bila kufuata utaratibu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” amesema Mpuya.
Kabla ya hakimu kutoa adhabu, washtakiwa kwa nyakati tofauti waliomba kupunguziwa adhabu kwa wakidai wamekaa mahabusu muda mrefu nchini Afrika Kusini, hivyo wamejifunza na wanajutia kosa walilotenda.
Akitoa hukumu, Hakimu Mwankuga amesema amezingatia maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka kuwa washtakiwa hawana rekodi za makosa ya jinai na jinsi washtakiwa walivyokiri kwa dhati shtaka.
“Kutokana na mazingira hayo na jinsi washtakiwa walivyojutia kosa lao, Mahakama hii inawahukumu kulipa faini ya Sh50,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela kila mmoja,” ameamuru Hakimu Mwankuga.
Source: mwananchi.co.tz