Unguja. Utaratibu ulioanzishwa na Serikali wa kuendesha huduma za maabara za afya kwa utaratibu wa ubia kupitia kampuni na mashirika binafsi kwenye hospitali, umeendelea kuibua wasiwasi kwa wataalamu na wameshauri uangaliwe upya.
Mfumo huo ulianza kufanya kazi mwaka 2023 ambapo katika baadhi ya hospitali za Serikali huduma za maabara zinaendeshwa na kampuni binafsi, lengo likiwa kuleta ufanisi.
Katika risala ya wataalamu wa maabara iliyosomwa na Ussi Hamza Ussi, katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maabara leo Aprili 21, 2024, amesema bado uendeshaji wa maabara hizo si rafiki kwa wahudumu ambao tayari wapo kwenye mfumo rasmi wa ajira wa Serikali au wanaotarajia kuingia kwenye mfumo huo.
“Wabia waliomo kwenye uendeshaji wa maabara hizo kwa sasa bado hawajatambua umuhimu wa kutumia wataalamu wa maabara wa ngazi ya kati na ile ya wabobezi.
Ussi, ambaye pia ni mtaalamu wa maabara, amesema masilahi hayatoi fursa kwa wataalamu hao kuondoka serikalini kwenda kufanya kazi kwenye maabara zenye ubia.
Wameshauri Serikali iangalie jambo hilo ili uendeshaji ubadilike na utoe fursa kwa wataalamu wa kuanzia ngazi ya Shahada ya kwanza na wabobezi wajiunge, kwani wana hamu kubwa na wana wajibu wa kuhudumia wananchi.
Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi, katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Afya, Ahmed Mazrui, amesema nia ya Serikali si kuua kada ya maabara bali kuboresha huduma.
“Nia ya Serikali si kuua kada ya maabara kama mnavyodhani bali ni kuboresha huduma kwa wagonjwa. Ninakubali, kweli Serikali haikuandaa mwongozo na utaratibu wa watumishi kwenye taasisi ambazo zinachukua ubia wa maabara zetu,” amesema Dk Mwinyi.
Hata hivyo, amewataka watendaji wa taasisi zinazohusika wakae na wabia wawashauri utaratibu mzuri wa mishahara na posho kwa mujibu wa miongozo ya Serikali, ili watumishi wa ngazi hizo ambao wapo serikalini na wale wanaotegemea kujiunga na ajira ya Serikali waone fursa hiyo na kujiunga.
Pia amezitaka taasisi za maabara kujikita katika utafiti na kuongeza nguvu kwenye taasisi hizo.
Amesema kufanya uchuguzi kwa njia za kiutafiti zitasaidia udhibiti wa maradhi kwa njia za kisayansi.
Amesema Serikali itaendelea kuziboresha maabara hizo ili ziendelee kufanya uchunguzi na utafiti wenye tija katika maradhi, vinasaba, kemikali, vyakula kwa pande zote za binaadamu, mifugo na kilimo.
Amewataka kuongeza bidii kuwatumikia wananchi wote kwa utii na kwa mujibu wa taaluma zao na viapo kwa kutoa majibu sahihi ya uchunguzi na kutunza siri kwa wanayoyagundua.
Dk Mwinyi amesema kada hiyo ina dhima kubwa kwa jamii na Serikali maana wote wanawaamini na kuwategemea.
Source: mwananchi.co.tz