
Karagwe. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewaonya viongozi wa chama hicho Mkoa wa Kagera kuacha tabia ya kuwakaribisha raia kutoka nchi jirani kufanya shughuli za kilimo katika maeneo ya Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kulinda usalama wa Taifa.
Akizungumza katika mkutano wa ndani wa chama, Wasira alitahadharisha kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa mipaka na rasilimali za Taifa, na kuongeza kuwa ni jukumu la viongozi kuhakikisha kwamba sheria na taratibu za nchi zinaheshimiwa na kutekelezwa ipasavyo.
“Usalama wa Taifa ni jukumu letu sote. Tunapowakaribisha wageni kufanya shughuli za kilimo bila kuzingatia sheria, tunaweza kujikuta katika hali ya hatari. Inapaswa kuwa kipaumbele chetu kulinda rasilimali na ustawi wa nchi yetu,” amesema Wasira.
Pia, ameahidi kwenda kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, ambaye pia ni mbunge wa Karagwe, ili afanye uchunguzi.
Amesisitiza kuwa wale wote waliobainika kuanzisha makazi na kufanya shughuli za kilimo kinyume cha sheria ndani ya Tanzania wafukuzwe na wachukuliwe hatua za kisheria.
Msingi wa maagizo hayo kwa viongozi wa chama hicho unatokana na malalamiko yaliyotolewa na wanachama wa CCM kwenye mkutano wa ndani uliofanyika katika Ukumbi wa Mjerumani, Wilaya ya Karagwe. Mkutano huo uliwahusisha pia viongozi kutoka Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, uliofanyika leo, Jumapili, Machi 23, 2025.
Kwa mujibu wa maelezo ya wananchi hao, raia wengi kutoka Rwanda wamekuwa wakiingia katika vijiji vya mpakani na kutumia mbinu mbalimbali kuhalalisha uwepo wao, ikiwa ni pamoja na kulima kwa muda mrefu, kisha kula ‘dili’ na viongozi wa CCM ili wapewe kadi za uanachama wa chama hicho.
Wamedai kuwa tatizo hilo limekua kwa kiasi kikubwa, hasa katika wilaya za Karagwe na Kyerwa, kiasi cha baadhi ya Watanzania kujikuta katika migogoro ya ardhi na raia hao wa kigeni. Raia hao hujinasibisha kuwa ni Watanzania kwa kutumia kadi za CCM kama kinga.
Akizungumza katika mkutano huo, Wasira, anayeendelea kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, amewataka viongozi wa chama hicho kuacha mara moja tabia hiyo.
“Kama kuna maeneo ambayo yamevamiwa, nitakwenda kulifikisha suala hili kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, lazima ashughulikie kwa sababu tumempa kazi. Wakihitaji kuja Tanzania, lazima wafuate utaratibu,” amesema Wasira.
Amesisitiza kuwa ikiwa hali hii itaendelea, siku za baadaye itasababisha migogoro mikubwa, ikiwa ni pamoja na machafuko ya ardhi na madai ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Watanzania walionyang’anywa ardhi niwaambie, hakuna jambo gumu duniani kama ardhi. Mnasema mna ardhi kubwa, lakini kila siku mnazaliana kwa asilimia tatu kila mwaka. Wakati tunapata uhuru, tulikuwa milioni nane, lakini sasa tuko zaidi ya milioni 63, huku ardhi ikiwa ileile,” amesema.
Wasira amewataka viongozi wa CCM kuacha kusherehekea jambo hilo, kwani wamepewa mamlaka ya kusimamia usalama wa Taifa kwa niaba ya wananchi walio wengi.
“Hatuna ugomvi nao kule wanakotoka. Ni marafiki zetu, lakini na sisi tukitoka hapa Karagwe na kuhamia huko kwao, wanatufukuza haraka. Wananchi wao wako milioni 12, lakini ukubwa wa nchi yao ni kama Mkoa wa Kagera. Jambo hili lazima tulikemee, na kwa kuwa kuna Wizara inayohusika, tutaiomba ije kulishughulikia,” amesema.
“Wengine mnawakaribisha, wakiona mambo hayaendi, wanakuja kuomba uanachama wa CCM. Hawa ni raia wa Tanzania? Huwezi kuomba uanachama wa CCM wakati wewe si raia wa Tanzania. Mnataka kukichukua chama chetu ili kiwe na tabia za kule mlikotoka? Maana wanavyama vyao kule, lakini wanaviheshimu,” amesema Wasira.
Katika mkutano huo, hoja ya Wasira iliungwa mkono na makada wengi, akiwemo Medison Kiagatuka, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji Mkoa wa Kagera na mkazi wa Kijiji cha Rugera, aliyesema migogoro ya ardhi imekuwa kubwa katika maeneo ya mpakani kati ya wenyeji na raia kutoka Rwanda.
“Walianza kuingia kidogo kidogo kwa ajili ya kulima, lakini sasa wanalima kwa wingi, huku wakila dili na wenyeviti wa CCM ili wapewe kadi na kuendelea kumiliki ardhi. Wamesababisha migogoro mingi na ukiangalia, wanalindwa na viongozi wetu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi, amesema kuwa jimbo la Karagwe ni mojawapo ya maeneo salama zaidi kwa CCM katika kujikusanyia kura kwa ajili ya uchaguzi ujao kutokana na sifa nzuri ya kisiasa ya eneo hilo.
“Pamoja na uhakika huu, hatupaswi kubweteka. Tunatakiwa kuendeleza muendelezo huu. Changamoto zipo, lakini Serikali itaendelea kuzitatua,” amesema Karamagi.
Amesema kuwa uchaguzi mkuu unakaribia, na vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali, badala ya kuendelea kuwa wafuasi wa wagombea.
Naye, Mussa Usi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM akiwakilisha vijana upande wa Zanzibar, amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika siasa badala ya kutumika kama wafuasi wa wagombea wengine.
“Vijana tuache kulalamika, tuchukue hatua. Kama kuna kijana amejipima na kuona anaweza kugombea udiwani, achukue fomu. Na kama amejipima na kuona anaweza kugombea ubunge, naye achukue fomu,” amesema.
Amesema kuwa vijana wanapaswa kuepuka siasa za kibaguzi na za kikanda zinazopandikizwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, kwani jambo hilo linahatarisha mshikamano wa Taifa.
Naye, Richard Kasesela, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia Viti 20 kutoka Tanzania Bara, amesema kuwa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama mara nyingi huambatana na changamoto nyingi, lakini wanachama wanapaswa kuwa watulivu.
“Tuache mchezo wa kuwaburuza wengine. Wanaotaka kugombea wasiwe na hofu kwa sura za watu waliokunja nyuso. Nendeni mkachukue fomu. Ndiyo kwanza tunajifunza siasa,” amesema Kasesela.
Source: mwananchi.co.tz