Mufindi. Ili kupunguza utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Ilongo iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), kupitia shamba la miti la Sao Hill wametoa vifaa vya ujenzi wa bweni la wasichana vyenye thamani ya zaidi ya Sh30 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo leo Juni 29, 2024, Ofisa Elimu Sekondari Wilaya Mufindi, Daniel Mapilya amesema msaada huo uliotolewa na Sao Hill, una manufaa katika kupunguza viashiria hatarishi vya mimba kwa watoto wa kike shuleni.
“Wanafunzi hawa walikuwa wanapanga mitaani kwenye nyumba za wananchi bila kuwa na uangalizi wa aina yoyote, hivyo msaada huo wa vifaa vya kujenga bweni kutoka Sao Hill utawasaidia kusoma kwa pamoja wakiwa bwenini bila usumbufu wowote,” amesema Mapilya.
Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bweni hilo, litawasaidia wanafunzi wao kwa kuwapunguzia kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa nane hadi kufika shuleni hapo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ikweha, Tabia Chibwana amesema uwepo wa bweni hilo utasaidia kupunguza changamoto ya watoto wa kike kupata ujauzito, hivyo litasaidia watoto hao kutimiza ndoto zao.
Ofisa huyo amesema shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 448, kati yao 268 ni wanafunzi wa kike ambapo tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2007, wamekuwa wakipata changamoto ya wanafunzi hao kurubuniwa, hali ambayo imesababisha kupata ujauzito kwa sababu ya kukaa mitaani kwenye vyumba vya kupanga.
Mhifadhi Mkuu wa Sao Hill, Yebby Yoram amesema wataendelea kusaidia kadri bajeti itakavyokuwa kusaidia miradi kama hiyo katika maeneo mengine.
“Maombi mengi yanahusu miradi kama hii lakini kuna baadhi ya shule tumesaidia miradi hiyo ikiwemo shule ya sekondari Luganga, Changalawe pamoja na shule zingine,” amesema.
Awali akisoma taarifa ya vifaa hivyo, Mhifadhi Mwandamizi wa shamba la Sao Hill, Peter Nyahende amesema Sao Hill wanatambua umuhimu wa mazingira bora ya kutolea elimu kwa watoto hao kwa kukabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule hiyo.
Source: mwananchi.co.tz