Wanaojifungua watoto njiti wataka ongezeko la likizo

Wanaojifungua watoto njiti wataka ongezeko la likizo

Kibaha. Wanawake wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti wamesema siku 84 zilizowekwa kisheria kama likizo ya uzazi hazitoshelezi kulea watoto hao, wakiomba kufanyika wa marekebisho ya sheria ili kuwaongezea muda.

Wamesema hayo leo Machi 6, 2024 wakati wakipokea msaada wa vifaa vya usafi vilivyotolewa na idara ya wanawake ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (Tughe) waliotembelea Hospital ya rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi.

“Siku 80 ni chache kumuacha mtoto njiti na kuanza kazi, kwani anakuwa hajatengamaa vizuri. Ni vema iwekwe sheria ambayo inatambua kulipiza miezi inayotimiza kipindi cha kujifungua kama mjamzito amejifungua ndani ya miezi saba basi likizo yake ijumlishwe miezi mitatu na siku 80,” amesema Felister Assenga ambaye ni ofisa muuguzi kwenye hospitala ya Tumbi.

Amesema kuwa wanawake wanaojifungua watoto njiti wakiongezewa muda wa likizo,  watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi,  pindi wanaporejea kazini kwa kuwa hawatakuwa na mawazo mengi kichwani kwa kuwaza watoto wao.

Kwa upande wake,  Sikitu Salumu ambaye pia ni miongoni mwa wanawake waliojifungua watoto njiti ndani ya hospitali hiyo,  amesema kuwa malezi ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati,  yanahitaji nafasi na muda wa kutosha hivyo kuna kila sababu ya jamii kulitambua hilo ili kutoa ushirikiano.

“Natoa wito kwa jamii kuna baadhi wamekuwa wakihusisha na imani potofu pindi mwanamke anapojifungua mtoto njiti,  jambo ambalo siyo kweli ni lazima watambue kuwa kila kitu kinapangwa na Mungu,  hivyo tunapaswa tuwapende watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na si kuwawazia vibaya,” amesema.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo ambao ni vifaa vya usafi na nguo za kusitiri watoto wachanga, Ofisa Elimu Kazi wa Tughe makao makuu, Nsubisi Mwasendede amesema chama hicho kinaiomba Serikali kufanya maboresho katika sheria zake,  ili kuwaongezea siku za likizo ya uzazi wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti.

“Sheria ya sasa ya ajira na mahusiano kazini imekuwa ikitoa siku 84 kwa wanawake wanaojifungua mtoto mmoja na pia siku 100 kwa wanajifungua zaidi ya mtoto mmoja wala haisemi chochote kuhusu wanawake wanaojifungua watoto njiti.

“Ndio maaana tumeona ni vyema kuikumbusha Serikali kufanya mabadiliko ili kuwaongezea muda wanawake hao,” amesema.

Likizo watoto njiti bungeni

Suala hilo la likizo liliwahi kuibuliwa bungeni jijini Dodoma Juni 25, 2019, ambapo aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na utawala bora), Mary Mwanjelwa alisema kuwa Serikali imeweka utaratibu kuwa mtumishi wa umma anayejifungua pacha zaidi ya wawili au watoto njiti.

Alisema mwajiri wake anapaswa kuwailisha hoja kwa katibu Mkuu (Utumishi) ili kupata kibali cha kuongezewa muda wa likizo.

“Ikitokea mtumishi wa umma kajifungua watoto pacha zaidi ya wawili au watoto njiti na kulazimika kuwa na muda zaidi wa kuhudumia watoto hao, mwajiri wake anapaswa kuwasiliana na katibu Mkuu (Utumishi) ili atoe kibali cha kuongezewa muda wa likizo ya uzazi,” alisema.

Ziara ya TUGHE

Naye Mwenyekiti wa idara ya wanawake (TUGHE) makao makuu Agnes Ngereza, amesema katika kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani, wameona ni vema kuwatembelea na kutoa msaada kwenye wodi ya wanawake waliojifungua watoto njiti na kupata changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuziwasilisha kwa wadau wengine.

Kwa upande wake,  muuguzi bingwa wa watoto hospitalini hapo,  Maua Pendo ameushukuru uongozi wa TUGHE kwa kutoa msaada huo kwa wanawake na kuziomba taasisi zingine kuiga mfano huo.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories