Dar es Salaam. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), limesaidia kampuni tatu za Tanzania kupata soko la parachichi nchini China.
Mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika sekta ya kilimo na biashara.
Soko hilo limepatikana baada ya TPHPA kuwezeshwa kufuata utaratibu unaohitajiwa na Mamlaka Kuu ya Forodha wa China (GACC).
Msaada huo ulitolewa kuypitia mradi wa Kuimarisha Afya ya Mimea Tanzania kwa Usalama wa Chakula Ulioboreshwa, (STREPHIT), unaolenga kuboresha upatikanaji wa mazao ya kilimo salama na ya ubora wa juu kwa masoko ya kitaifa na kimataifa.
Akizungumzia soko hilo kupitia taarifa iliyotolewa na Fao leo Jumatano Septemba 4, 2024, Meneja wa Ufuatiliaji wa Afya ya Mimea na Uwezeshaji wa Biashara wa TPHPA, Mdili Katemani amesema,”kwa msaada kutoka kwa mshirika wetu Fao, tumekamilisha kwa mafanikio taratibu zinazohitajika na soko la China na kuruhusu wakulima na wazalishaji kuuza aina tatu za parachichi mbichi ambazo ni Hass, Fuerte na Pinkertons.”
Katemani ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa STREPHIT amesisitiza kuwa, mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja za Serikali ya Tanzania, ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na msaada wa kiufundi kutoka kwa Fao.
Ili wazalishaji wa ndani waweze kuuza parachichi China, wanapaswa kusajiliwa na GACC kupitia TPHPA.
Aidha, mashamba ya uzalishaji, vituo vya upakiaji na kampuni za kuondoa vijidudu lazima zisajiliwe na TPHPA ili kupata nambari za ufuatiliaji zinazohitajika kwa utambulisho wa wauzaji.
Zaidi ya hayo, mashamba haya yanapaswa kuzingatia mbinu bora za kilimo na usimamizi wa wadudu ili kudhibiti wadudu wa karantini kama vile nzi wa matunda, viwavi jeshi na vidukari.
Ufungaji, uhifadhi na usafirishaji wa parachichi lazima pia ufuate itifaki zote zilizokubaliwa kati ya Tanzania na China.
Mbali na parachichi, China imekuwa ikipokea mazao ya kilimo kutoka Tanzania, ikiwamo kahawa, soya, ufuta, korosho na mazao ya baharini.
Wakati wa ziara yake ya kidiplomasia nchini China mwaka 2023, Rais Samia alitia saini Itifaki ya Mahitaji ya Usafi wa Mimea kwa Mauzo ya Parachichi Mbichi kutoka Tanzania kwenda China, hatua iliyofungua njia kwa upatikanaji huu wa soko kihistoria.
Chini ya mradi wa STREPHIT, unaotekelezwa na Fao kupitia Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Tanzania, juhudi zinaendelea kuhakikisha mahitaji yote muhimu yanatimizwa ili kuweka mazao ya kilimo ya Tanzania katika soko la kimataifa.
Tanzania tayari inauza parachichi kwa nchi mbalimbali, zikiwamo India, Uholanzi, Kenya, Uingereza, Umoja wa Falme za Kiarabu, Afrika Kusini na Ufaransa.
Source: mwananchi.co.tz