Wadau waonyesha kasoro ulaji mbogamboga, matunda

Wadau waonyesha kasoro ulaji mbogamboga, matunda

Dar es Salaam. Wakati ulaji wa mbogamboga na matunda ukitajwa kuwa moja ya njia ya kujenga mwili wa binadamu na kumuepusha na magonjwa, imeelezwa mboga nyingi zinazozalishwa hazifai kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Hiyo ni kutokana na kuwa na bakteria wanaoweza kuathiri matumbo ya watu na viuatilifu vilivyozidi kiwango.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Julai 22, 2024 katika mjadala wa X Space ulioandaliwa na Mwananchi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) wenye mada inayosema: ‘Mambo muhimu ya kuzingatia katika uandaaji, ulaji wa mbogamboga na matunda.’

Akizungumza katika mjadala huo, Mtaalamu wa Kituo cha Mbogamboga duniani, Jeremiah Sigalla amesema kupitia ukaguzi waliofanya waligundua baadhi ya mboga katika masoko ya Arusha na Dar es Salaam zilikuwa chafu na zinahatarisha afya ya mlaji.

Mtaalamu huyo amesema katika taasisi yao ya World Vegetable Centre kupitia tafiti walizozifanya wamegundua mboga hizo zina kiwango kikubwa cha wadudu wanaodhuru tumbo.

“Kupitia kuangalia viambata ambavyo vinaathiri lishe na afya ya mlaji, mboga hizi zimekuwa na kiwango kikubwa cha bakteria wanaodhuru mazingira ya tumbo na katika baadhi ya masoko ya Arusha ya Dar es Salaam tumekuta mboga nyingi ambazo zinaonekana nzuri kwa macho ukazinunua, lakini kwa afya si salama,” amesema Jeremiah.

Amesema kwa kuwa maeneo mengi ya mijini mboga hizo zinahitajika kwa wingi, ndio maana hata mazingira ya uzalishaji wake si salama.

Hivyo amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama FAO wanaona ni muhimu elimu kutolewa kwa wakulima katika matumizi ya dawa ambazo zinatumika kuzitunza mboga hizo.

“Kuna baadhi ya dawa na mbolea maarufu kama busta zinachangia uharabifu wa hizi mboga. Teknolojia inakua, lakini njia za teknolojia hiyo kama mzalishaji asipopata taarifa sahihi itaathiri uzalishaji na tija inayopatikana katika uzalishaji wake,” amebainisha Sigalla.

Katika hilo, Mtafiti na mtaalamu wa chakula, Martin Kimanya amesema mtu anapokula mbogamboga zilizochafuliwa ikiwemo kemikali ni sawa na kutokuwa navyo nyumbani.

 “Tatizo kubwa lililopo nchini katika eneo la mbogamboga ni uchafuzi kutokana na matumizi ya viuatilifu katika kiwango ambacho si bora,” amesema.

Amesema kuwa pia kuna wakulima wanataka kuongeza uzalishaji, lakini wamekuwa wakifanya katika namna ambayo haifai na wengi hawana ufahamu ambao utawafanya wajue ni aina gani ya viuatilifu si sahihi vya kutumia.

“Kwa bahati mbaya udhibiti wa viatilifu vilivyopo sokoni kwetu pia si mzuri, kwani baadhi vinaweza kuwa vimepigwa marufuku huko nje, lakini bado vikawepo sokoni huku wakulima wakikosa mbinu sahihi ya kutumia viatifu hivyo,” amesema Profesa Kimanya.

Amesema ukubwa wa hili tatizo unatokana na mambo matatu la kwanza ni wakulima kutumia viatifu ambavyo baadhi haviruhusiwi na hawajui namna nzuri ya kuvitumia, maofisa ugani na kilimo kutokuwa na uwezo wa kumfikia mtu kwa namna inayotakiwa ili kumueleza namna nzuri ya utumiaji ili kutoathiri afya ya mlaji.

Alichokisema Malembo

Kuhusu maofisa ugani kuhudumia wakulima, Mkurugenzi wa Malembo Farm, Lucas Malembo amesema utafiti uliofanywa na Jukwaa Huru la Kilimo ANSAF mwaka 2017 umeonyesha asilimia 48 ya vijiji 15,082 vilivyosajiliwa nchini havina maofisa ugani wa kutosha. 

Utafiti unaonyesha pengo hilo wakati ambao sera ya kilimo ya mwaka 2013 ikitaka kila kijiji kuwa na afisa ugani mmoja.

“Katika hali ya kawaida bado kuna changamoto ya usalama wa mboga tunazokula kutokana na uhaba wa watalaamu. Matumizi mabaya ya viuatilifu ni matokeo ya wakulima wengi kutokuwa na elimu ya kilimo biashara sensa ya kilimo ya mwaka 2019/2020 inaonyesha matumizi ya viuatilifu ni asilimia mbili ya wakulima wote nchini,” amesema.

Hata hivyo, Profesa Kimanya amesema kutokana na kutokuwa na uhakika na usalama wa tunda linapotoka ni vyema kuliosha na kulimenya kabla ya kuanza kula.

Kuosha na kumenya kunapunguza kemikali ambazo zinapatikana, ijapokuwa utapunguza baadhi ya virutubisho katika tunda hilo.

Faida za tunda

Pamoja na changamoto hizo, Mkurugenzi Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC,) Dk Esther Nkuba amesema mwili wa binadamu unahitaji virutubisho zaidi ya 50 kwa siku na kila chakula kina virutubisho zaidi ya kimoja, hivyo ulaji wa matunda wakati wa kula iwe asubuhi mchana au jioni hauna tatizo.

“Hakuna tafiti inayosema ukila matunda kwa kuchanganya inatengeneza sumu. Ukila ndizi ukachanganya na parachichi mwili wenyewe unajua chakufanya,” amesema Dk Nkuba.

Akichangia hoja hiyo, Mkurugenzi wa Hospitali ya Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi amependekeza watu kupenda kula matunda yenyewe badala ya kunywa juisi, ili kupunguza wingi wa sukari anayoweza kuinywa kwa wakati mmoja.

“Pia watu wale vyakula badala ya kutumia dawa za virutubishi, kwani haviwezi kuwa mbadala wake,” amesema Profesa Janabi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Zanziba, Dk Omar Ally Amir amesema katika kukabiliana na changamoto hizo wanachokifanya sasa ni kuangalia namna wanayoweza kuwafikia wakulima, ili kuzalisha mbogamboga na matunda ambayo ni salama kwa walaji.

“Pia tunajaribu kuhimiza kilimo hai kisichotumia viuatilifu, ili mazao yanapozalishwa yawe salama kwa watumiaji,” amesema Dk Amir.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories