Wadau wakubaliana kupunguza gharama za tiketi za ndege Afrika

Wadau wakubaliana kupunguza gharama za tiketi za ndege Afrika

Unguja. Wadau wa anga wa Afrika wamekubaliana kupunguza bei ya tiketi za ndege kwa lengo la kuwarahisishia watumiaji na kuongeza ufanisi katika sekta ya anga.

Hayo yamebainishwa jana Ijumaa Mei 17 2024  katika kongamano la usafiri wa anga lililojumuisha wadau 200 wa anga kutoka nchi 10, uliofanyika visiwani Zanzibar kwa siku tatu.

Washiriki wa kongamano hilo wanatoka nchi za Uganda, Kenya, Rwanda, Afrika ya Kusini, Somalia, Sudan Kusini, Burundi, Kongo, Ethiopia na wenyeji Zanzibar Tanzania.

Pia, katika mkutano huo, wadau hao wamekubaliana kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kudhibiti wizi wa mitandao na kuifanya sekta hiyo kubaki salama.

Akizungumza baada ya kuhitimisha kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya usafiri wa Anga ya Kenya (KCAA), Emile Arao amesema miongoni mwa changamoto kubwa zinazolikumba Bara la Afrika ni gharama kubwa ya tiketi za ndege jambo ambalo ni kikwazo kwa watumiaji.

Amesema kutokana na kuliona hilo wadau wa anga  katika kongamano hilo wamekubaliana kupunguza gharama hizo  ili kuongeza ufanisi wa anga.

“Suala la bei za tiketi za ndege ni jambo lililowaibua wadau wengi wa anga na kutaka kupunguziwa gharama hizo kwa kuwa, hilo limeonekana kuwa kikwazo kwa nchi nyingi kushindwa kutumia usafiri wa ndege,” amesema Arao.

Sambamba na hilo amesema kutokana na kuongezeka kwa uhalifu wa mitandao (cyber crime), wadau hao wamesema wataimarisha mifumo ya Tehama ili kuufanya usafiri wa ndege kuendelea kuwa salama.

Amesema watumiaji wa Tehama duniani wameongezeka, hivyo uwezekano wa kuiba mifumo ya ndege na kusababisha kurejesha nyuma jitihada hizo hivyo kuepukana na hilo lazima waimarishe mifumo ili kulithibiti.

Mkurugenzi Udhibiti Uchumi Maendeleo ya Usafiri wa anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga amesema kuwepo kwa jumuiya ya mawakala wa usafiri wa anga Afrika utaufanya usafiri huo kuendelea kuaminika kuwa salama wakati wote.

Amesema Kongamano hilo limewakumbusha wakaguzi kuzingatia vigezo vya usalama wa anga ili kuwaondoa hofu wateja wake kutumia usafiri huo.

“Washiriki wa jumuiya hii wanashindwa kufuatilia ukaguzi wa usalama wa anga kwa kukaa muda mrefu bila kufuatilia alichokikagua hivyo tumekumbusha kuwepo kwa mpango endelevu wa ukaguzi kwa nchi hizi,” amesema Malanga.

Amesema kufanya hivyo kutawajengea uwezo wa kutambua umuhimu wa kuwepo usalama wa anga wakati wote jambo litakalosaidia nchi kuwa salama na sio kusubiria Shirika la Kimataifa Usafiri wa Anga (ICAO) kufanya ukaguzi.

Pia, amesema wanaofanya ukaguzi wanapaswa kupewa mafunzo maalumu yatakayowajenga kuyafanyia kazi maswali wanayopewa ya ukaguzi na kuandaa nyaraka ili kuweka uthibitisho.

Malanga amezitaka nchi ambazo hazijajiunga kuharakisha utekelezaji wa anga kuwa wengi kwa lengo kuondoa vikwazo vilivyopo na kupata soko huru lenye gharama nafuu za usafiri.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Udhibiti na Usalama wa Anga Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC CAssoa) kwa TCAA, kauli mbiu yake ni “Mustakabali wa usafiri wa anga, kudumisha mifumo ya usafiri wa anga yenye ustahimilivu, uendelevu, ubunifu na usalama.”

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories