Viongozi nchini Tanzania kikaangoni uharibifu wa mazingira

Viongozi nchini Tanzania kikaangoni uharibifu wa mazingira

Alfred Lasteck, Nafasi,BBC

Serikali ya Tanzania imesema kuna baadhi ya viongozi nchini humo kwa maslahi yao binafsi wanachangia katika uharibifu wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji na kupelekea mito kukauka.

Aidha imeelezwa kuwa familia 12 ya viongozi wakiwemo mawaziri, wanasiasa na majaji wanatuhumiwa kuhusika katika uharibifu katika vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkuu uliopo katika ukanda wa nyanda za juu kusini mwa Tanzania.

Kauli hiyo ya serikali iitolewa jana mkoani Iringa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt Philip Mpango alipohudhuria Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji.

Dkt Mpango alisema, “Wapo baadhi ya viongozi kwa maslahi binafsi, wanachangia sana kwenye uharibifu wa mazingira. Siamini wakulima wetu masikini, wafugaji kwamba ndio wanaoharibu mazingira. Lazima tunusuru mito yetu yote hasa mito ya kimkakati kama Ruaha, viongozi wa namna hii hawatufai.”

Aliongeza, “Mimi najiuliza kule hifadhi wale ng’ombe zaidi ya 3,000 ni wa mfugaji masikini au yale ‘macombine harvest’ makubwa ni ya wakulima wale ninaowafahamu mimi?,” Alisema na kuongeza kuwa kutokana na uharibifu huo, “mazingira sasa yanalipa kisasi na tumeanza kulipa jeuri yetu.”

Wataalamu wanasema shughuli za kibinadamu kando ya mto zimesababisha mto huo kukauka

Wanahabari wafanya uchunguzi

Katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameishauri serikali kuchukua hatua ya kuiondoa Ranchi ya Usangu ambayo ipo ndani ya bonde oevu linalolisha maji Mto Ruaha Mkuu sambamba na kujenga tuta eneo la Ngiliamu ili kuunusuru mto na ukame.

“Sisi tunafanya habari za uchunguzi na tumebaini Ranchi ya Usangu inamilikiwa na familia 12, wamo majaji, wamo wabunge, wamo mawaziri na nitakukabidhi majina ili hatua stahiki zichukuliwe kwa maslahi ya Taifa,” alisema Balile ambaye pia ni mwandishi mwandamizi wa Habari za uchunguzi.

Wanaharakati wataka hatua kuchukuliwa

Wanaharakati wa Mazingira nao wanataja kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kunusuru vyanzo vya maji na mazingira.

Habib Mchange ambaye ni Mwanaharakati wa Mazingira aliiambia BBC kuwa hatua za haraka zinahitajika na kwamba hawata kaa kimya wakiona mazingira yanaharibika.

Mchange amesema, ni zaidi ya siku 130 Mto Ruaha hautiririshi maji.

“Leo Mto Ruaha Mkuu una zaidi ya siku 130 bila kutiririsha maji, na ukienda hifadhini utasikitika kuona viboko wanagombania mchanga na si maji kutokana na uharibifu wa mazingira,” anaeleza Mchange.

Mchange anasema kupitia ripoti ya mazingira za Taifa, asilimia 16 ya ardhi ya Tanzania ni jangwa huku asilimia 63 ikiwa imeharibiwa.

Anaeleza, kuwa sio mto Ruaha pekee inayokumbana na changamoto hizo bali hata mto malagarasi, Ruvu, Ruvuma na mingine mingi inapitia hali hiyo na kwamba kama hatua za haraka hazitachukuliwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi.

Nini kimesababisha mto Ruaha kukauka?

Mto Ruaha Mkuu umekauka kutokana na vyanzo vyake kwa maana ya Bonde la Ihefu na Usangu kuwa vimeharibiwa.

Wahifadhi wanaeleza kuwa shughuli za kibinadamu kama kilimo na ufugaji ndio chanzo kwa ardhi katika bonde hilo hilo kuharibika.

Wanasema uchepushaji mkubwa wa maji umepelekea kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu ambao unaotegemewa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na n ahata katika kuzalisha umeme kwenye mabwawa ikiwamo Mtera, Kidatu na Mwalimu Nyerere (mradi mkubwa zaidi wa umeme nchini Tanzania).

Leaders in Tanzania are linked to the destruction of the environment

Uharibifu ni mkubwa kiasi gani?

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha, Godwell Ole Meing’ataki anasema Mto Ruaha ulikuwa unataririsha maji mwaka mzima hapo zamani, lakini kuanzia miaka ya 90 ukaanza kuonesha dalili ya kukauka.

“Uhai wa taifa unategemea uwepo wa Mto Ruaha. Ihefu ni chanzo cha Mto Ruaha Mkuu, miaka ya 90 hadi sasa ukubwa wa eneo la Ihefu linasinyaa na kushindwa kukusanya maji kwa ajili ya Mto Ruaha Mkuu, na namna linavyozidi kusinyaa Mto Ruaha Mkuu unaathiriwa,” Kamishna huyo aliileza BBC na kuongeza; “Mwaka 1985 kulikuwa na hekta 14,000 za kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Ihefu, mwaka 1998 hekta za kilimo cha umwagiliaji zilifika 24,000, mwaka 2013 zilifika hekta 115,000, maji yanaelekezwa zaidi katika mashamba. Tunavyozungumza Ruaha umekauka ni zaidi ya siku 130 mto hautoi maji japo kuna mvua ndogo imepita.”

Ni hatua gani zinachukuliwa na serikali ya Tanzania?

Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango alisema yeye alipojitosa katika vita alijuwa si vita rahisi, lakini alidhamiria kuishinda vita hiyo.

Alisema, “Hayo majina ya familia 12 yaliyotajwa nitaomba nikabidhiwe na kwa kuwa nchi hii inaendeshwa kwa haki na sheria, tutaenda kuyafanyia kazi ili kutoa haki.”

Pia aliagiza watendaji wa mabonde ya maji nchini kuanza kuchukua hatua dhidi ya wale wote waliovamia maeneo ya uhifadhi wakiwamo waliojenga kuta katika kingo za maji za Mto Ruaha Mkuu. Sambamba aliagiza kufikishiwa vibali vyote vya wale wanaofanya shughuli kwenye bonde hilo.

Pamoja na yote pia liagiza apelekewe tathmini ya matumizi ya ardhi ambayo aliiagiza ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira nchini.

Aidha, aliagiza kukamilishwa haraka kwa kazi ya kuweka mipaka ya Ruaha.

Mto Ruaha una umuhimu gani kwa Tanzania?

Mto huo wenye urefu wa kilomita 475 unaanzia katika Mlima Kipengere wilayani Makete mkoani Njombe, ukimwaga maji katika ardhi oevu ya Usangu wilayani Mbarali mkoani Mbeya kupitia Runapa hadi katika Mto Rufiji.

Mto huu unachangia asilimia 22 ya maji ya Bonde la Rufiji ukiwa na zaidi ya aina 39 za samaki na viumbe wengine waishio majini wakiwemo mamba na viboko.

Mtu huu ni muhimu kwani ndio unaipa uhai ikolojia ya hifadhi ya Ruaha sambamba na kuwa chanzo cha uzalishaji umeme kwenye mabwawa ya Mtera, Kidatu na Mwalimu Nyerere.

Kwa mantiki hiyo, kukauka kwa mto huo, utahathiri pato la taifa la utalii kutokana na hifadhi ya Ruaha kutokuwa na uhifadhi dhabiti.

Pia utahathiri ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na ule wa taifa kutokana na kukusekana kwa umeme wa uhakika kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea nishati hiyo itokanayo na maji.

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year’s Most Read News Stories