Dar es Salaam. Serikali imevunja ukimya kuhusu uwepo wa viongozi wa dini nchini wasiozingatia misingi ya sheria na maandiko ya vitabu vitakatifu, badala yake wanawatumia waumini kama mtaji wa kujilimbikizia mali, huku wakiwapa mafundisho yasiyofaa.
Kutokana na hayo, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, kusimamia kikamilifu Sheria ya Usajili wa Jumuiya na kanuni zake, ili kuhakikisha taasisi zinazosajiliwa zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo na masharti ya usajili wake.
Pia amewasihi viongozi wa dini kuungana na Serikali kukemea vikali mafundisho na matendo yasiyofaa katika jamii na yasiyozingatia sheria za nchi, yakiwamo yanayofanywa na baadhi ya viongozi hao.
Dk Mpango ametoa kauli hiyo Septemba 7, 2024 mkoani Arusha, ikiwa tayari zimeshachukuliwa hatua na Serikali, za kulifunga Kanisa la Christian Life na kiongozi wake mkuu Mchungaji Domique Kashoix Dibwe maarufu Kiboko ya Wachawi raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuondolewa nchini.
Kiongozi huyo anadaiwa kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume cha maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania na matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya.
Madai mengine ni kutoa mahubiri yanayodhalilisha watu madhabahuni, kutoa mahubiri chonganishi na kuhamasisha waumini wa kanisa lake kuua watu kwa dhana au tuhuma za uchawi au ushirikina.
Hatua ya kulifunga kanisa hilo na kumuondoa nchini kiongozi wake mkuu ilikuja siku kadhaa baada ya gazeti la Mwananchi kuchapisha mfululuzo wa habari kuhusu kuwapo viongozi wa makanisa wanaotoza fedha waumini wao na kuwahadaa huku wakijipatia ukwasi mkubwa.
Hata baada ya kanisa lake kufungiwa na yeye kuondolewa nchini, gazeti la Mwananchi lilifichua kuwa Kiboko ya Wachawi aliendelea kutoa huduma akiwa DRC akiwataka watoe fedha ili awafanyie maombi.
Kauli ya Dk Mpango
Akizungumza jijini Arusha wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach, Dk Mpango amesema yameibuka mafundisho ya baadhi ya viongozi wa dini yanayowaaminisha wafuasi wao kutegemea miujiza zaidi ili kupata maendeleo badala ya kufanya kazi kwa bidii.
Dk Mpango amesema ni muhimu kwa viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uzalendo, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu abariki kazi zao.
“Miaka ya karibuni imeshuhudiwa kuongezeka kwa wahubiri wanaojilimbikizia fedha na mali binafsi kutokana na sadaka na mauzo ya vitu mbalimbali na wengi wa wahanga (waathirika) wa mahubiri ya aina hiyo ni wananchi wanaokabiliwa na shida au matatizo mbalimbali ya maisha,” amesema Dk Mpango katika taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na ofisi yake.
Kauli ya Masauni
Wakati Dk Mpango akisema hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni akizungumza wakati wa sherehe za ufungaji wa makambi ya Waadventista Wasabato jijini Arusha leo Septemba 7, aliwataka watu wote wanaojihusisha na shughuli za kidini kufuata sheria za nchi.
“Hivi karibuni kuna mchungaji mmoja tulimuondosha nchini kutokana na kukiuka sheria za usajili na mmeshuhudia huko alikokwenda amekuwa akisambaza video kuthibitisha kwamba yale aliyokuwa akiyafanya yalikuwa kinyume kabisa na mafundisho ya kitabu cha dini.
“Yakiwemo masuala ya utapeli, kuwatoza watu fedha kinyume cha utaratibu na kuwaaminisha watu kwamba miujiza inaweza kuwafanya wawe matajiri au kupata ufumbuzi wa matatizo yao,” amesema Masauni.
“Nitoe wito kwa watu wote walioamua kufanya shughuli za kidini kufuata misingi ya kisheria ambayo inalenga dhamira ya kuhakikisha kwamba inafuata mafundisho ya vitabu vya Mungu. Uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba upo lakini hautakiwi kuvuka mipaka hadi kuvunja sheria za nchi yetu. Hili sizungumzii kwa wageni tu bali hata kwa wenyeji ziko sheria ambazo ni lazima zifuatwe,” amesema.
Hivi karibuni kupitia video kadhaa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Kiboko ya Wachawi alionekana akiwakejeli Watanzania akieleza namna anavyozikosa fedha alizokuwa akiwatoza ambazo anazitumia kwa ajili ya kufanya uwekezaji nchini kwake.
Katika moja ya video hizo, Kiboko ya Wachawi anaonekana akihesabu fedha, huku akisema bado anakumbuka Sh500,000 alizokuwa akiwatoza waumini wake ili awaombee.
Julai 25, 2024 Serikali ilipolifunga kanisa lake lililokuwa Buza, wilayani Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, katika barua ya kufutwa usajili wa kanisa hilo iliyotolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ilitaja suala la kutoza fedha kuanzia Sh500,000 kwa waumini ili awape huduma ya uponyaji wa kiroho, akisema inakiuka matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2019.
Onyo kwa vijana
Katika hatua nyingine Dk Mpango alikemea matumizi holela ya mitandao ya kijamii akieleza wananchi hususan vijana wengi wanadhani ili kuwa kijana wa kisasa, inawalazimu kuiga mambo yanayooneshwa kwenye mitandao hiyo yakiwemo yale yasiyo endana na mila na desturi.
“Kukosekana kwa hofu ya Mungu katika jamii kunapelekea kuongezeka kwa matukio ya mauaji ya kikatili, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na wanawake, familia za mzazi mmoja, watoto waliozaliwa nje ya ndoa, migogoro ya ndoa, talaka, migogoro ya mirathi na ardhi, ubadhirifu wa mali za umma na matukio ya watu kujinyonga,” alisema Dk Mpango.
Masauni pia aligusia suala la mmomonyoko wa maadili akieleza kuwepo kwa ongezeko la matukio ya ukatili yanayohusisha mauaji, ubakaji, ulawiti yanayochochewa na mambo mbalimbali ikiwemo imani za kishirikina.
“Katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai, Agosti na hii Septemba tumeshuhudia ongezeko la matukio yanayohusu mauaji ya kikatili yanayohusishwa na masuala mbalimbali ikiwemo imani za kishirikina. Pia kuna matukio ya ubakaji, uuaji wa kutumia silaha za jadi na hata upoteaji wa watu.
Vyombo vya usalama vinapata kazi kubwa katika kuyadhibiti haya, yote haya yanachangiwa na mmomonyoko wa maadili, hakuna hata tu mmoja mwenye hofu ya Mungu anayeweza kufikiria kufanya kitendo ambacho kinaweza kuleta madhara na athari kwa binadamu mwingine,” amesema.
Kwa upande wake Muasisi wa Kanisa la New Life Outreach Tanzania Mwinjilisti Dk Egon Falk alishukuru Serikali kwa kutoa kibali kwa kanisa hilo kuhubiri neno la Mungu kwa miaka 50.
Amesema kanisa hilo litaendelea kufuata sheria na taratibu za nchi wakati wa utoaji wa huduma ya kuhubiri neno la Mungu na huduma nyingine za kijamii.
Source: mwananchi.co.tz