TPA kunadi bandari za Tanga, Mtwara, Kigoma kimataifa

TPA kunadi bandari za Tanga, Mtwara, Kigoma kimataifa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imejipanga kuzitangaza kimataifa bandari nyingine zilizopo maeneo tofauti na ile ya Dar es Salaam ili ziweze kuhudumia nchi mbalimbali zinazopitisha mizigo yake Tanzania.

TPA inapanga kuzinadi bandari hizo kupitia mkutano wa Global Logistic Convention 2024 unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kati ya Agosti 14 na 16, 2024 na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 400 kutoka mataifa mbalimbali.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumatano, Agosti 7, 2024, Mwakilishi wa TPA, Beatrice Jairo amesema wamejipanga kutumia mkutano huo kuangalia nini mataifa mengine wanafanya na kujifunza ili kuboresha huduma kwa wateja kutoka mataifa mbalimbali.

Amesema mkutano huo pia utaisaidia TPA kufanya intelijensia ya masoko na kupata takwimu sahihi ambazo wanazikosa ili kuja namna inavyoweza kuwafanya kuongeza umiliki wa soko.

“Pia, itakuwa ni nafasi nzuri ya kuzitangaza bandari zilizopo, kwa sababu hatuna Bandari ya Dar es Salam pekee bali tunayo ya Tanga, Mtwara na Mwanza, Kigoma na Kyela ambazo zote zinafanya vizuri, hivyo hii ni fursa ya kuwaeleza Watanzania na wageni kwa jumla kufahamu sehemu ambayo tunafanya kazi na mipaka yake,” amesema Beatrice.

Amesema fursa hiyo itatumika kuwaelezea wateja maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam na shughuli zinazotekelezwa kwa sasa.

Akitoa maoni yake kuhusu kuzitangaza bandari nyingine, mtaalamu wa uchumi Profesa, Aurelia Kamuzora amesema ni moja ya jambo linaloweza kuchochea matumizi yake na kuwa na matokeo chanya kwenye uchumi.

Amesema hadi kufikia uamuzi huu anaamini TPA imejipanga ipasavyo katika kuhudumia mizigo ya nchi jirani itakayopitia bandari nyingine tofauti na Dar es Salaam.

“Tusije kutangaza kitu ambacho hakijawekwa vizuri, kama hatujajipanga inaweza kuwa mbaya lakini naamini viongozi waliopo wanao mkakati na mpango kazi wanaoutumia kuimarisha bandari hizo,” amesema Profesa Kamuzora huku akionyesha kuvutiwa na uwekezaji wa miundombinu ya barabara mbalimbali zilizojengwa nchini.

Hayo yanasemwa wakati ambao Tanzania imeshuhudia ukuaji wa ongezeko la shehena ya mizigo inayoihudumia katika bandari zake kwa asilimia 42.3 kati ya Julai mwaka 2023 hadi Machi 2024.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akisoma bajeti yake bungeni 2024 alisema ongezeko hilo lilikuwa kutoka tani milioni 14.56 hadi tani milioni 20.72, mtawaliwa.

Ukuaji huo ulienda sambamba na ongezeko la mizigo ya nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zimbabwe zilizopitia bandari ya Tanzania iliongezeka hadi kufikia tani 8,871,438 kwa mwaka 2023 kutoka tani 8,239,112 kwa mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 7.67.

Katika hotuba hiyo pia, Prosefa Mbarawa aliliambia Bunge namna maboresho yanavyoendelea kufanyika katika bandari tofauti ikiwamo Tanga, Mbamba Bay, Bagamoyo, mwanza North katika ujenzi wa miundombinu ili kuziwezesha kutoa huduma nzuri.

Walichokisema Taffa

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Chama cha mawakala wa forodha Tanzania (Taffa), Edward Urio amesema itakuwa ni fursa kwa kampuni za usafirishaji mizigo za Tanzania kutafuta masoko zaidi na kujuana.

“Kampuni za usafirishaji zitakutana na watumiaji wa bandari zilizopo nchini kwenda nchini kwao. Pia, itaongeza utangazaji biashara kwa kampuni na wadau waliopo katika sekta ya usafirishaji,” amesema Urio.

Pamoja na mengine, mkutano huo pia utaangazia changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya usafirishaji majini ikiwamo kuangalia hali halisi ilivyo.

Hata hivyo, Urio amesema uwepo wa changamoto mbalimbali wakiwamo maharamia katika korido mbalimbali kama Suez Canal umekuwa na athari za moja kwa moja katika kuongeza gharama za usafirishaji mizigo.

“Mnyororo wa usafirishaji unapoingiliwa maana yake unaongeza gharama, kutokuwapo kwa usalama katika korido hizo unaongeza gharama za usafirishaji mizigo,” amesema Urio.

Hiyo ni kutokana na wamiliki wa meli za mizigo kukodi ulinzi wa ziada wanapopita katika mifereji isiyo salama ili kuepusha kutekwa au kuvamiwa.

“Ulinzi huo wa ziada unapokodiwa ni gharama tayari, gharama hii itashuka kwa mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi, mfanyabiashara anaposafirisha mizigo yake, atakapolipa kodi na kuweka thamani ya mizigo yake ataiingiza gharama hiyo katika bei ya bidhaa yake ili atakapoingia sokoni ili aweze kuwa sawa,” amesema Urio.

Urio amesema hali iliyopo Suez Canal inagusa watu wengi na tayari jumuiya za kimataifa zimeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha matatizo hayo yanapotokea na hayaongezi gharama katika korido hizo.

Tofauti na hilo amesema kitu kingine kinachochangia kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa mizigo ni mahitaji dhidi ya usambazaji unaofanyika.

Akitolea mfano wa hivi karibuni bidhaa zinazotoka China kuja Tanzania gharama ya usafirishaji wake kudaiwa kuongezeka mara dufu amesema:“Utafuatiliwa kwa kina meli zilizokuwa zikipakia mizigo kuleta Dar zinapata mzigo mwingine mwingi kwenda Ulaya na sehemu nyingine za dunia, ikiwa kuna uhitaji eneo hilo bei inakuwa nzuri.”

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories