TIA kuwapiga msasa kidigitali watu wenye mahitaji maalumu

TIA kuwapiga msasa kidigitali watu wenye mahitaji maalumu

Morogoro. Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kupitia kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wake, Dk Momole Kasambala imetangaza mpango wake wa kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanaosoma kwenye vyuo vya taasisi hiyo, wanapata mafunzo ya teknolojia kama wanafunzi wengine.

Imesema lengo ni kutaka wakidhi mahitaji ya soko la ajira na kujiajiri wenyewe.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Juni 9, 2024 baada ya kikao kazi cha wakufunzi na wakutubi kilichofanyika Kilakala, Morogoro, Dk Kasambala amesema mabadiliko mbalimbali ya mitalaa ya kufundishia kwenye taasisi hiyo, ikiwemo mafunzo kupitia teknolojia, yatawahusisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Amesema awali mafunzo hayo hayakuwa yakitolewa kwa kundi hilo. “Mabadiliko haya yatarahisisha matumizi sahihi ya teknolojia na kuwafanya wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo vya taasisi yetu, wawe na uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira ya kisasa,” amesema Kasambala.

Amesema mafunzo hayo pia yanalenga zaidi watumishi wa taasisi, wakutubi na wanafunzi wenye mahitaji maalumu kama walemavu wa kuona na kusikia.

“Lengo kubwa ni kuhakikisha tunaendana na mahitaji ya mitalaa ambayo yamebadilika na yameongeza utumiaji wa mifumo,” amesema Dk Kasambala.

Naye Lucina Comino, Mratibu wa Makundi ya watu wenye mahitaji maalumu kutoka TIA, akizungumzia hilo, amesema wakufunzi wa vyuo vyote vilivyoko chini ya taasisi hiyo wanapaswa kuwa karibu na wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

“Katika suala la ufundishaji na kujifunza, maktaba zetu lazima ziweke vifaa vitakavyowawezesha wanafunzi hususan wenye mahitaji maalumu, kujisomea na kujipatia maarifa, ikiwemo vitabu vyenye maandishi nundu na vifaa vya kusikiliza pale wanapohitaji kujisomea,” amesema Comino.

Amesema zipo njia nyingi za kutumia hasa kwa wanafunzi ambao ni walemavu wa kuona wanapohitaji kujisomea.

“Teknolojia inavyoendelea kukua, tumeshuhudia vitabu vya kusikiliza. Tunataka vitabu hivyo visambae kwenye maktaba zetu ili wanafunzi wenye mahitaji maalumu waweze kujipatia maarifa na wakihitimu elimu yao, waweze kupata ajira kama wanafunzi wengine,” amesema.

Magreth Joseph ni mwanafunzi mwenye ulemavu wa macho anayeishi Mrogoro Mjini, amesema endapo mitalaa hiyo itatekelezwa ipasavyo, watu wenye ulemavu wa kuona na kusikia wataweza kuajirika tofauti na hali ilivyo sasa.

“Mara nyingi sisi walemavu wa kuona tunasoma kupitia alama kwenye vitabu, lakini kwa ukuaji wa teknolojia, kuna vitabu vya kusikiliza. Kama hilo litafanyika ipasavyo, itatupa nafasi sisi wenye mahitaji maalumu kusoma na kukidhi matakwa ya kupata ajira kama wahitimu wengine,” amesema Joseph.

Magreth Emmanuel, mdhahiri kutoka TIA Kampasi ya Mbeya, amesema masomo yataanza kupatikana kwa njia ya mtandao na walengwa wakuu ni walemavu.

“Baada ya mabadiliko ya mitaala, masomo yatapatikana kwa njia ya mtandao na tutahakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanakuwa wanufaika na elimu,” amesema Emmanuel.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories