Habari ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), si yenye kushtua, maana ni utaratibu wa vyama vyenye wabunge kupishana katika uongozi wa taasisi hiyo.
Habari kuwa Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, ndiye amekuwa Makamu Mwenyekiti wa TCD, ndiyo inasogeza mjadala. Mwenyekiti Chadema, Mwenyekiti TCD, halafu Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Makamu Mwenyekiti TCD. Watafanyaje kazi?
Tafsiri ambayo haikwepeki baina ya vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo ni kuwa vimekuwa hasimu kwenye jukwaa la “vyama vya upinzani”. Yaani, baada ya mchuano wa CCM na vyama vya upinzani, nje ya chama hicho kinachoongoza dola Tanzania, kuna msigano wa wazi kati ya Chadema na ACT-Wazalendo.
Vyama vya ACT-Wazalendo na Chadema, mara nyingi vina mitazamo ya aina moja kuhusu masuala, lakini hutofautiana njia ya kuyafikia mambo husika. Ajabu, tofauti hiyo ya njia ndiyo husababisha migongano, kiasi cha viongozi na wafuasi wao hulumbana majukwaani na mitandaoni hadi kudhihirisha uhasimu mkubwa uliopo baina yao.
Mathalan, Chadema na ACT-Wazalendo, wote maono yao yanaweza kuwa yanasema Mwanza kuna sangara wa kutosha. Halafu, wakatofautiana jinsi ya kufika Mwanza. Chama kimoja kikasema njia bora ni kwenda kwa treni, kingine kikawa na mapendekezo ya kutumia barabara. Treni na barabara huzua zogo na kusahau makubaliano ya kimsingi kuwa sangara wapo Mwanza.
Huu siyo mfano, bali ndivyo ilivyokuwa. Chadema walijenga msimamo kwamba wanahitaji Katiba mpya. ACT-Wazalendo, wakatoa maono yao ya kupata Tume Huru ya Uchaguzi kuelekea Katiba mpya. Mpaka hapo, utaona kuwa Chadema na ACT-Wazalendo, walikuwa na makubaliano kwamba Katiba mpya ni lazima.
Sasa, Katiba mpya moja kwa moja, ambao ni msimamo wa Chadema, halafu Tume Huru kwanza kuelekea Katiba mpya, mtazamo wa ACT-Wazalendo, ikawa ndiyo hoja ya mapambano baina ya vyama hivyo. Hawatofautiani hatima, wanatofautiana namna ya kuifikia.
Namna ambavyo hutofautiana njia ya kufikia hatima ya jambo, ndivyo hujenga misuguano kijamii. Upo wakati watu hujiuliza, kwani wapinzani wa Chadema ni ACT-Wazalendo au CCM? Swali hilohilo lipo upande wa ACT-Wazalendo dhidi ya Chadema.
Kipindi hiki, Mbowe na Dorothy, wamekabidhiwa uongozi wa TCD, lipo swali linaweza kuwa linagonga vichwa vya wengi; watafanyaje kazi? Watasikilizana na kuelewana kwa sababu wanatambua hatima yao ni moja au watachagua kulumbana kwenye njia ya kufikia hatima kama kawaida yao?
Ushauri kwa Mbowe, Dorothy
Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln anatajwa kuwa bora kuliko wengine 45 waliopata kuongoza taifa hilo kubwa duniani. Sifa zipi ambazo zinampambanua kwa ubora miongoni mwa wengine wote waliowahi kukalia ofisi ya Rais wa Marekani, Oval Office? Kwa utangulizi tu ni kwamba ukiona kiongozi anaitwa bora, ujue alionyesha ubora.
Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, anatajwa kuwa mmoja wa viongozi bora zaidi kupata kuliongoza Taifa la Marekani. Obama mwenyewe alipata kujipambanua katika hotuba zake kwa kunakili nukuu nyingi za Lincoln, zaidi alishakiri kwamba alijifunza mengi kiuongozi kupitia mtindo wa uongozi wa Lincoln.
Kitabu kinachoitwa “Team of Rivals: The Political Genius of Abraham Lincoln”, kilichoandikwa na mwanahistoria wa Marekani, Doris Kearns Goodwin na kuchapishwa mwaka 2005, kinaeleza kwa nini Lincoln alikuwa bora. Kinadhihirisha kwamba Lincoln ni kiongozi wa kufaa kuigwa na vizazi vyote. Obama amepata kukiri kuwa kitabu hicho kilimsaidia kuteua Baraza la Mawaziri.
Watu wengi humsifu Lincoln kwa uongozi wa utu, ulioweka misingi ya haki za binadamu na kupiga marufuku ubaguzi. Ni Lincoln aliyefanya kampeni ya kupinga biashara ya utumwa Marekani na alipochaguliwa kuwa Rais, alitangaza ukomo wa biashara ya utumwa na kupitisha azimio la kumuweka huru kila mtumwa (Emancipation Proclamation), Januari mosi, 1963.
Hata hivyo, yapo mengi yenye kumfanya Lincoln awe bora. Alionyesha utofauti chanya ndiyo maana viongozi wengi hutamani kumuiga. Ni hakika kwamba kila kiongozi wa nyakati za sasa akimuiga Lincoln na kumpatia, naye atatamkwa kuwa bora. Viongozi aina ya Lincoln hutokea mara chache, ili kutoa tafsiri ya maana ya uongozi uliotukuka.
Ndani ya kitabu cha Team of Rivals, sifa kubwa ya Lincoln inatajwa ni jinsi ambavyo alikuwa na uwezo mkubwa wa kumudu presha za kiuongozi. Uwezo wake mkubwa wa kutambua karama na uwezo wa watu wengine, hata wale waliokuwa wapinzani wake wa kisiasa. Hapa ndipo hasa kwenye ukuu wa Lincoln na ndipo ushauri kwa Mbowe na Dorothy, unapopenya.
Ni sababu ya Goodwin kukiita kitabu chake, Team of Rivals; The Political Genius of Abraham Lincoln, akimaanisha kwamba Serikali ya Lincoln ilijumuisha watu waliokuwa wapinzani wa kisiasa wa Lincoln, lakini mwenyewe alitambua kile walichokuwa nacho, akawaheshimu, akawateua na kushirikiana nao kufanya kazi bora kwa nchi.
Kwa tafsiri ambayo si rasmi, unaweza kusema Timu ya Wapinzani; Maarifa ya Kisiasa ya Abraham Lincoln. Sababu namba moja ambayo ilimfanya Lincoln atambue uwezo wa wapinzani wake na kuwapa nafasi za uongozi ni utulivu na usikivu wake. Alipenda kusikiliza watu wenye mitazamo tofauti na ya kwake, ndiyo maana aliweza kuujua ubora wa wapinzani wake.
Washindani wa Lincoln wa kisiasa ambao aliwapa nafasi kwenye Baraza la Mawaziri ni Waziri wa Fedha, Salmon Chase, Waziri wa Mambo ya Nje, William Seward, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Edward Bates. Hao ni kuwataja kwa uchache, waliopata kutoana jasho la kisiasa na Lincoln, lakini akatambua uwezo wao na kuwateua wamsaidie kazi.
Obama anaposema kitabu cha Team of Rivals kilimjenga katika kufanya uteuzi wa Baraza la Mawaziri, anaaminisha kweli. Maana alishindana vikali na aliyekuwa Seneta wa New York, Hillary Clinton, kuwania tiketi ya chama cha Democratic kuwa mgombea urais katika Uchaguzi wa Rais wa Marekani mwaka 2008. Hata hivyo, Obama baada ya kushinda urais alimteua Hillary kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Hoja ya kushika
Imeelezwa kuwa Lincoln aliweza kufanya kazi na wasaidizi wake, ambao aliwateua miongoni mwa wapinzani wake kwa kuwa alikuwa msikivu. Kusikilizana ndiyo njia itakayowawezesha Mbowe na Dorothy kufanya kazi kwa maelewano, licha ya historia ya vyama vyao kutofautiana na kulumbana mara kwa mara.
Katika kusikilizana, pengine wakafanya kazi iliyotukuka, ambayo inaweza kushawishi ushirikiano mkubwa mbele ya safari. Tanzania itafanya uchaguzi wa Serikali za mitaa, Novemba 2024, hivyo huu ni mwaka wa uchaguzi. Vyama vya ACT-Wazalendo na Chadema, vitakuwa imara zaidi kwenye uchaguzi, endapo vitashirikiana.
Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu 2025, kwa maana hiyo umebaki mwaka mmoja. Chadema na ACT-Wazalendo, ili kuikabili CCM wakiwa imara, wanahitaji ushirikiano. Hivyo, kitendo cha Mbowe na Dorothy, kuongoza TCD, ni fursa ya kuona jinsi ambavyo inawezekana kufanya kazi pamoja.
Uchaguzi Mkuu 2020, Chadema na ACT-Wazalendo, walikuwa na makubaliano. Walishiriki uchaguzi kama timu. Matokeo yaliwasambaratisha. Walisimama pamoja kuyakataa matokeo. Wakatofautiana jinsi ya kuyaendea matokeo.
Chadema walikataa kila kilichotokana na Uchaguzi Mkuu 2020. ACT-Wazalendo, wao waliyakataa, halafu wakachukua walichopata. Hilo lilizua malumbano baina ya vyama hivyo.
TCD ni taasisi inayounganisha vyama vyenye uwakilishi bungeni; CCM, Chadema, ACT-Wazalendo na CUF, wakati NCCR-Mageuzi ambacho hakina uwakilishi, chenye ni mwanachama mshiriki, maana hadi Uchaguzi Mkuu 2020, kilikuwa na ushiriki bungeni. Kila mwaka unachaguliwa uongo mpya. Mbowe na Dorothy, wataongoza TCD kwa mwaka mmoja.
Source: mwananchi.co.tz