Tanzania yapewa miezi sita kufuta adhabu ya kifo

Tanzania yapewa miezi sita kufuta adhabu ya kifo

Arusha/Dar es Salaam. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) kwa mara nyingine imeiamuru Serikali ya Tanzania kufuta adhabu ya kifo kama sharti la lazima kwenye sheria zake, huku ikiipa miezi sita kuanzia sasa kutekeleza amri hiyo.

Mahakama hiyo imetoa amri hiyo katika hukumu iliyoitoa Juni 4, 2024 kutokana na shauri la rufaa lililofunguliwa mahakamani hapo na mfungwa aliyehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Dominick Damian, dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika hukumu, mahakama hiyo yenye makao jijini Arusha, imeiamuru Serikali ya Tanzania kumfutia adhabu ya kifo Dominick, aliyesubiri utekelezaji wa adhabu hiyo katika Gereza la Butimba mkoani Mwanza.

Uamuzi wa Mahakama ya Afrika umetolewa wakati kukiwa na pendekezo la Tume ya Haki Jinai, ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini, la kutaka kurekebishwa sheria kuhusu adhabu hiyo, ambalo pia linasubiri utekelezaji wa Serikali.

Tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande, katika ripoti yake iliyowasilishwa kwa Rais Samia Julai, 2023 imependekeza sheria inayotoa adhabu hiyo irekebishwe.

Tume ilipendekeza Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, ifanyiwe marekebisho ili adhabu ya kifo isiwe adhabu pekee kwa kosa la mauaji, bali adhabu itolewe kulingana na mazingira ya utendaji kosa.

Pia imependekeza adhabu ya kifo isiporidhiwa na Rais kwa kipindi cha miaka mitatu, adhabu hiyo itenguke kuwa kifungo cha maisha.

Tume katika ripoti hiyo imebainisha adhabu hiyo imekuwa haitekelezwi kwa miaka mingi, hivyo kusababisha waliopewa adhabu hiyo kuishi maisha ya hofu, huku wakisubiri utekelezaji wa adhabu hiyo. Kwa takwimu za Mei, 2023, wanaosubiria kunyongwa walikuwa 691.

Dominick alikata rufaa katika mahakama hiyo dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba iliyomtia hatiani kwa kosa la mauaji na kumhukumu adhabu hiyo Desemba 14, 2012, katika kesi ya jinai namba 61 ya mwaka 2008.

Kabla ya kukata rufaa AfCHPR, Dominick alijaribu kujinasua katika adhabu hiyo kwa kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo.

Hata hivyo, Mahakama Rufani katika hukumu ya Machi 17, 2014 iliitupilia mbali rufani yake na kuunga mkono hukumu ya Mahakama Kuu. Baada ya hukumu hiyo ndipo akaenda Mahakama ya Afrika.

Msingi wa rufaa

Katika shauri namba 048/2016, Dominick aliiomba mahakama hiyo kubatilisha adhabu ya kifo, akidai inakiuka haki zake za kikatiba, akizitaja haki hizo kuwa ni haki ya kusikilizwa, haki ya kuishi na haki ya kuheshimu utu wake.

Dominick alidai alizuiwa kwa muda mrefu kizuizini tangu alipokamatwa mpaka kesi ilipoanza kusikilizwa baada ya miaka mitano na miezi mitatu.

Mahakama katika hukumu iliyotolewa na jopo la majaji Blaise Tchikaya na Dumisa Ntsebeza, imekataa madai yake mengine lakini imekubaliana naye katika hoja ya adhabu ya kifo.

Mahakama hiyo imesema kwa kuhukumiwa adhabu ya kifo kama adhabu ya lazima chini Kifungu cha 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu inaondoa haki yake ya kuishi.

“Kutokana na hilo, mahakama hii inamuamru mlalamikiwa, Serikali ya Tanzania, kumfutia hukumu ya kifo mwombaji na kumuondoa kabisa kwenye adhabu hiyo,” imesema mahakama katika hukumu.

“Pia mahakama hii inamuamuru mlalamikiwa, kuondoa adhabu ya kifo ya lazima kutoka katika sheria zake ndani ya miezi sita baada ya taarifa ya hukumu hii; na kuchukua hatua zote muhimu,” inasema sehemu ya hukumu.

Kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (PC), mtu anayepatikana na hatia katika kesi za mauaji adhabu yake ni kunyongwa mpaka kifo, ambayo kwa mujibu wa kifungu hicho ni sharti la lazima bila mbadala wala mjadala.

Si mara ya kwanza

Hata hivyo, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imeshaiamuru Serikali ya Tanzania mara kadhaa kufuta adhabu hiyo, katika hukumu zake ambazo imekuwa ikizitoa katika mashauri ya rufaa yanayowasilishwa hapo na watu mbalimbali waliohukumiwa adhabu hiyo kwenye mahakama za ndani.

Mwaka 2019 mahakama hiyo katika shauri la maombi namba 007 la mwaka 2015, lililofunguliwa na Ali Rajabu na wenzake wanne, dhidi ya Serikali ya Tanzania, mahakama hiyo pia iliiamuru Serikali kufanya marekebisho na kuondoa adhabu ya kunyongwa kama sharti la lazima.

Ali na wenzake, Angaja Kazeni maarufu kama Oria, Geofrey Stanley ‘Babu’, Emmanuel Michael maarufu Atuu na Julius Petro walihukumiwa adhabu ya kunyongwa mwaka 2011 baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya mauaji.

Hata hivyo, hukumu hiyo na nyingine za aina hiyo hazijawahi kutekelezwa na Serikali wala kuondoa adhabu ya kifo, ambayo imekuwa ikiibua mjadala nchini.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Juni 7, 2024, wakili wa kujitegemea Fulgence Massawe amesema mbali ya hukumu ya Ali Rajabu na wenzeka ambayo ndiyo imekuwa maarufu, mahakama hiyo imeshatoa hukumu kama hizo nyingi.

“Nakumbuku mimi nimeshasimamia kesi tatu ambazo mahakama imetoa hukumu kama hiyo. Nakumbuka kuna ya Martin Msuguri, nyingine ya Mwigulo na nyingine nimezisahau, hata hivyo kumekuwa na changamoto kwenye utekelezaji,” amesema Massawe.

Wakili Massawe kutoka Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria (LHRC), amesema Tanzania imeingia kwenye mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu, ambayo imeisaini na kuiridhia hivyo inapaswa kuitekeleza kwa kuwa inaifunga.

“Kwa sababu tunaamini katika utawala wa sheria, lazima tuheshimu sheria zetu na sheria zetu zina nguvu sawa, ziwe za kimataifa au za kikanda, zote zina nguvu sawa na sheria za ndani. Kwa hiyo zinapaswa zitekelezwe pamoja na maamuzi ya mahakama kwa namna zinavyotakiwa,” amesema.

Wadau, wakiwamo wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakipinga adhabu hiyo katika majukwaa mbalimbali wakipendekeza ifutwe, huku baadhi yao wakieleza hivyo mbele ya Tume ya Haki Jinai.

Miongoni mwa waliotoa mapendekezo ni Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Fredrick Werema na Wakili wa Kujitegemea, Jebra Kambole.

Pinda alipinga adhabu hiyo akisema kuitekeleza ni kufanya kosa juu ya kosa na kwamba, hadhani kama ina tija wala kutibu tatizo na akuwa nchi nyingi zilishaiondoa.

Alisisitiza kiuhalisia haisaidii kupunguza wauaji badala yake, alipendekeza kifungo cha maisha.

Jaji Werema kwa upande wake alisema angependa ibaki hivyo, licha ya adhabu inatisha na wazungu walioileta wenyewe walishaiondoa na makosa ya mauaji yameendelea kuwepo licha adhabu hiyo kuwapo.

“Mimi nataka ibaki kwenye statute (sheria) kwa sababu inaweza kutokea pia mahali ikabidi unyonge. Kuna watu wanafanya mauaji ya kishenzi, kwa hiyo ukifika wakati huo, unaweza kutumia hiyo kuwaondoa katika jamii,” alisema.

Kambole alisema kifungu cha 197 cha Kanuni za Adhabu, kinachotoa sharti la lazima la adhabu hiyo, kinakinzana na Katiba ya nchi kwa sababu kinaondoa haki mbalimbali za binadamu zinazolindwa na Katiba ya nchi, hasa haki ya kuishi.

Alisema inaondoa haki ya kusikilizwa kwani hairuhusu mtu kujitetea kuhusu adhabu tofauti na washtakiwa wa makosa mengine ambao huruhusiwa kujitetea na kwamba, Mahakama inaondolewa haki yake ya uchambuzi sahihi na tathmini kabla ya kutoa adhabu.

Kambole anapendekeza mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hizo (Mahakama Kuu) iwe na mamlaka ya uchaguzi wa kutoa adhabu kulingana na mazingira ya kesi na kwamba mtu aliyetiwa hatiani ana haki kujitetea ili apewe adhabu ndogo.

Wakili Kambole anasema mazingira yanayosababisha makosa ya mauaji hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja na mwingine au tukio moja na lingine.

Kambole alijaribu kupinga sharti hilo kwa njia za kisheria baada ya kufungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu mwaka 2018 bila mafanikio.

Julai 18, 2019 Mahakama Kuu iliitupilia mbali na hata alipokata rufaa Mahakama ya Rufani pia ilitupiliwa mbali.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories