Dar es Salaam. Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha teknolojia mpya ya intaneti iliyoibuka duniani ya Metaverse inayotokana na intaneti ya vitu iitwayo (IOT).
Intaneti ya Metaverse inaunganisha dunia halisi na dunia isiyo halisi (virtual) ambayo kwa ujumla inatumika maeneo muhimu, ikiwemo elimu, afya, takwimu, viwanda na uchumi.
Kwa tafsiri, Metaverse inatengeneza uhalisia wa kitu kama kilivyo, lakini kwa njia ya kidijitali hivyo kuondoka gharama mbalimbali, ikiwemo usafiri na vifaa husika.
Akizungumza leo Jumatatu, Agosti 5, 2024 baada ya kupokea ugeni wa Rais wa Chuo cha Turku cha Finland, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga amesema fursa katika teknolojia hiyo zipo nyingi, hivyo Tanzania inakwenda kujenga umahiri katika eneo hilo.
“Intaneti tunayoitumia sasa inatumika kubadilshana taarifa katika namna ya kurasa, picha, video na imetupatia mafanikio makubwa.
“Sasa hivi teknolojia imekua na ipo hii mpya ya Metaverse ambayo inatumika duniani, ikiwemo katika kuunda meli, kufundishia wanafunzi kwa uhalisia. Tumeona tutumie fursa tuwe kitovu kwa bara letu,” amesema Dk Mwasaga.
Amesema kwa sasa Afrika hakuna nchi inayosema ni mahiri katika teknolojia hiyo, hivyo ni fursa kwa Tanzania kuanza na kwa sasa mipango iliyopo ni kujenga maabara ya kisasa ya teknolojia hiyo.
“Serikali kupitia bajeti ya mwaka jana na mwaka huu tumepewa fedha ya kujua tunajenga maabara ya aina gani ya Metaverse. Kwa sasa tunafanya upembuzi yakinifu na wenzetu wa Turku watatupa ushauri ya namna gani ya kufanya,” amesema.
Amesema maabara za Metaverse inatakiwa iwe katika muundo wa namna ya shule, au sehemu kama Mlima Kilimanjaro, Mbuga kama Ruaha, Ngorongoro hivyo inategemea na wapi inahitajika.
Kwa upande wa elimu, amesema teknolojia hiyo itaondoa uhaba wa vifaa hususani vya maabara, kwani mwanafunzi atajifunza kwenye Metaverse kwa kuwa atatumia vifaa kama vilivyo lakini kwa kidijitali, kisha akishapata uelewa ndipo anakwenda kwenye uhalisia.
Ameongeza kuwa hayo yote yanafanywa kwa sababu ya vijana wapate jukwaa la kujiajiri kupitia kuanzisha kampuni changa bunifu (start-ups) waweze kupambana katika soko la dunia.
Amesema Tume ya Tehama ipo kwa ajili ya teknolojia ibuka, hivyo Metaverse itaingizwa katika Wizara ya Elimu ili iwe faida kwa nchi.
Aidha, Serikali inataka hadi mwaka 2030 iwe kitovu cha uchumi wa digitali Afrika, ikiwa ni njia ya kuelekea katika dira ya mwaka 2050.
Katika kuhakikisha hilo, ndio maana Serikali inafanya jitihada kuchukua teknolojia ibuka zitakazofanya suala hilo kutimia.
Katika upande mwingine, Serikali ina mpango wa kujenga chuo cha kidijitali cha (DTI) Nala, jijini Dodoma ambacho kitatumia mikono zaidi ya nadharia kama anavyosema Mshauri Mwandamizi wa dijitali, Dk George Mulamula.
Amesema, DTI itafundisha kwa kutumia mitaala ya Metaverse, ili kuwafanya wanafunzi kuwa wabunifu. Amesema Ushirikiano na Chuo cha Turku ni mwanzo wa mwelekeo mpya katika gurudumu la kidijitiali.
DTI itajikita kutoa mafunzo ya Akili Mnemba (AI), IOT, usalama wa kimtandao na zote zinatumika kitengeneza Metaverse.
Faida zake amesema ni kutengeneza ajira, kutatua changamoto za kibiashara, jamii na serikalini ili kuendelea kiuchumi.
Kwa upande wake, Rais wa Chuo cha Turku, Profesa Vesa Taatila amesema teknolojia ya Metaverse ni muhimu zaidi katika dunia ya sasa, akitolea mfano katika elimu ya mafunzo.
Amesema teknolojia inatumika katika elimu, viwanda, afya na hata mafunzo ya kiusalama. Pia inaongeza thamani ya nchi.
Akithibitisha hilo amesema nchini kwao wanatengeneza dawa kupitia teknolojia hiyo, “Metaverse ni uti wa mgongo wa mapinduzi yajayo ya kiviwanda,” amesema Profesa Taatila.
Source: mwananchi.co.tz