Dar es Salaam. Kampuni ya Orca Energy Group Inc, iliyoorodheshwa katika soko la hisa la Toronto ikitokea visiwa vya Virgin vya Uingereza, imewasilisha madai ya Dola bilioni 1.2 za Marekani (Sh3.2 trilioni) dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Hatua hii ya kisheria ya Orca, inayomiliki kampuni za PanAfrican Energy Tanzania (PAET) na Pan African Energy Corporation Mauritius (PAEM), inaelezwa na kampuni hiyo inatokana na madai ya ukiukaji wa majukumu ya mikataba na uwekezaji.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa katika mtandao wa kampuni hiyo, ni madai ya ukiukwaji wa Mkataba wa Uwekezaji wa Mauritius-Tanzania (BIT), PSA (Production Sharing Agreement), na GA (Gas Agreement).
Serikali yafafanua
Akizungumza na gazeti dada la The Citizen jana, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Bonipace Luhende alikiri kupokea notisi kuhusu mgogoro huo kutoka Kampuni ya Orca kama inavyotakiwa na utaratibu wa ICSID.
“Pande zote mbili zina muda wa miezi sita wa kusuluhisha suala hilo, kama ikishindikana ndipo taratibu za kesi zitakapoanza,” alisema.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alipotafutwa na Mwananchi alisema Serikali ipo katika majadiliano na kampuni hiyo.
Alisema hafikirii kushindwa kuafikiana kupitia majadiliano hayo, akieleza wamekuwa wakifanya kazi na kampuni hiyo kwa muda mrefu.
“Lakini ikilazimika kufikia huko (mahakamani) tutafika, lakini sidhani kama tunaweza kufika huko,” alisema.
Kwa mujibu wa Kapinga, mkataba wa kampuni hiyo na Tanzania unatarajiwa kuisha mwaka 2026 na hawezi kueleza kwa kina yaliyopo ndani ya majadiliano.
“Kwa kuwa tupo kwenye majadiliano, tukiyaeleza tutakuwa tunaingilia majadiliano,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, mgogoro huo unatokana na TPDC kukataa mapendekezo ya PAET ya masharti ya kibiashara ya ziada ya gesi (AG) na mkataba mpya wa mauzo ya gesi, licha ya kumalizika kwa stahili za PG.
PAET inashikilia kuwa hatua hizi zinakiuka haki na matarajio yao ya kimkataba na inatafuta fidia inayozidi Dola 1.2 bilioni (Sh3.2 trilioni).
Notisi ya mzozo huo inataka mazungumzo na Serikali ya Tanzania na TPDC, huku taratibu za usuluhishi zikisubiriwa, ikiwa masuluhisho hayatafikiwa ndani ya muda uliopangwa.
“Chini ya Notisi ya Migogoro, PAET na PAEM wanataka mazungumzo zaidi na Serikali ya Tanzania na TPDC, endapo azimio halitafikiwa: (i) ndani ya miezi sita kuanzia tarehe ya Notisi ya Mgogoro kuhusiana na Mauritius- Tanzania BIT na (ii) ndani ya siku 45 baada ya Notisi ya Mgogoro kuhusu PSA na GA, PAEM na PAET, kwa mtiririko huo, zitaanza mashauri ya usuluhishi kwa mujibu wa BIT PSA na GA ya Mauritius-Tanzania,” inaeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mvutano uliongezeka pale PAET ilipoiomba TPDC kuomba kuongezewa muda wa leseni Aprili 2023. Licha ya PAET kuomba mara kwa mara, TPDC ilishindwa kuchukua hatua, kutokana na kuwepo kwa hoja za kisheria kuhusu kuendelea kwa PG.
Kusitasita kwa TPDC na tuhuma zinazodaiwa kuwa hazina uthibitisho dhidi ya PAET kulisababisha kuvunjika kwa mazungumzo.
Inadaiwa Aprili 15, 2024, Wizara ya Nishati ya Tanzania iliingilia kati, na kuiagiza TPDC kuendelea kuzalisha PG zaidi ya tarehe ya mwisho ya PPA, kinyume cha makubaliano yaliyokuwepo.
“PAET imekata rufaa kwa maamuzi haya kwa Wizara ya Nishati. Hata hivyo, kutokana na msimamo uliotolewa na Serikali ya Tanzania hadi sasa, PAET inatarajia kuwa Wizara ya Nishati nayo itakataa isivyostahili kuuzwa kwa gesi na PAET kwa masharti ya kibiashara,” inadai taarifa hiyo.
Inadaiwa Agosti 5, 2024, ilithibitishwa na barua iliyopokelewa na PAET kutoka Wizara ya Nishati, ambayo iliitaka PAET kupendekeza maneno yanayofaa kwa ‘mpangilio wa muda’ wa kupanua utoaji wa PG. Barua hiyo inaeleza zaidi kwamba ikiwa PAET itashindwa kufanya hivyo, zinatafutwa ‘njia mbadala’ za kuendesha kitalu husika.
Agizo hili lilitafsiriwa na PAET kama tishio la kupoka mali, na kuwafanya watoe Notisi ya Mzozo Agosti 7, 2024. “PAET imetafsiri barua hii kuwa ni tishio la wazi kwamba iwapo PAET haitavumilia TPDC na Serikali ya Tanzania ukiukwaji wa haki zake, Serikali ya Tanzania itanyang’anya haki za PAET kuhusu kitalu hicho,” inasomeka taarifa hiyo.
PAET imekuwa mwekezaji katika sekta ya nishati nchini Tanzania kwa zaidi ya miongo miwili, ikianza shughuli zake Oktoba 11, 2001.
Katika kipindi hiki, kampuni hiyo inadai imewekeza zaidi ya Dola milioni 311 katika uchumi wa Tanzania, hivyo kuchangia pato la Taifa kwa zaidi ya dola milioni 725 kila mwaka na kutoa zaidi ya Dola milioni 900 za mtiririko wa fedha kwa Serikali ya Tanzania.
Inaelezwa katika taarifa kuwa hoja ya msingi ni kuhusu leseni ya kuendeleza Songo Songo, iliyotolewa kwa TPDC mwaka 2001.
Makubaliano hayo, ambayo yanajumuisha Mkataba wa Kugawana Uzalishaji (PSA) na Mkataba wa Gesi (GA), yalipangwa kuzalisha gesi hadi Julai 31, 2024, hasa kwa ajili ya umeme katika eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Kesi zilizotatuliwa hivi karibuni
Julai 29, Tanzania ilifikia makubaliano ya suluhu na Indiana Resources Limited, kutatua mzozo wa muda mrefu wa kunyang’anywa Mradi wa Nickel wa Ntaka Hills.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania ilikubali kulipa Dola 90 milioni (takriban Sh237 bilioni) kwa Indiana Resources na taasisi zinazohusika, hivyo kuhitimisha takribani miaka saba ya usuluhishi katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Indiana Resources ina hisa nyingi za Ntaka Nickel Holdings Ltd (NNHL), Nachingwea UK Ltd (NUKL), na Nachingwea Nickel Ltd (NNL), Tanzania inatarajia kufanya malipo hayo kwa awamu tatu.
Awamu ya kwanza ya Dola milioni 35 tayari imepokewa, na Dola milioni 25 zinapaswa kulipwa kabla ya Oktoba 25, 2024; na Dola milioni 30 za mwisho zitalipwa kufikia Machi 30, 2025.
Oktoba 2023, Tanzania ilisuluhisha mgogoro na kampuni ya uchimbaji madini ya Winshear Gold Corp ya Canada, kulipa Dola milioni 30 (Sh75 bilioni) kufuatia mzozo wa kunyang’anywa mradi wa dhahabu wa SMP ulio kusini-magharibi mwa Tanzania, ukitaka fidia ya zaidi ya Sh250 bilioni.
Makubaliano hayo, ambayo yanajumuisha Mkataba wa Kugawana Uzalishaji (PSA) na Mkataba wa Gesi (GA), yalipangwa kuzalisha gesi (PG) hadi Julai 31, 2024, hasa kwa ajili ya uzalishaji wa umeme.
Source: mwananchi.co.tz