Tanzania kusaka Sh261 bilioni kila mwaka nchini Uturuki

Tanzania kusaka Sh261 bilioni kila mwaka nchini Uturuki

Dar es Salaam. Tanzania imeweka lengo la kuvutia mitaji ya Sh261 bilioni kila mwaka kutoka kwa wawekezaji nchini Uturuki kupitia sekta kadhaa za uwekezaji, ikiwamo kilimo.

Ili kufikia malengo hayo, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeingia mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Africapital Investiment Holding Limited ambayo itafanya kazi ya kuvutia mitaji na kuiweka pamoja kwa ajili ya kufanya uwekezaji nchini.

Kampuni hiyo itakuwa ikitafuta wawekezaji kutoka maeneo ya Uturuki na nchi jirani kabla ya kuwaleta nchini.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa TIC, Gilead Teri alisema Uturuki ni nchi yenye mtaji mkubwa katika maeneo ambayo yanaendana na mahitaji ya Tanzania kama teknolojia rahisi katika kilimo.

“Vitu kama bidhaa za kielektroniki za majumbani, bidhaa za ujenzi, sekta ya dawa inayojumuisha hospitali na sekta ya utalii, wenzetu wamepiga hatua. Tungependa kujifunza kutoka kwao na kampuni zao zije kuwekeza nchini,” amesema Teri.

Amesema makubaliano yaliyoingiwa ni ya kimkakati kwa sababu kampuni hiyo inajua mitandao ya kiuwekezaji.

Amesema awali taasisi za Serikali kama TIC zilikuwa zikifanya makubaliano na taasisi za uwekezaji za nchi mbalimbali lakini kutokana na kufanya kazi zinazofanana ilikuwa ngumu kufikia malengo.

“Hali hiyo ilikuwa ikifanya kushindwa kufikia lengo kwa sababu wote mnaenda kutafuta wawekezaji walewale wachache ambao wapo duniani, sasa tuliamua kushirikiana na kampuni binafsi ambazo zina fursa za kuleta wawekezaji,” amesema Teri.

Amesema ushirikiano wa kwanza kufanyika ulikuwa kati ya TIC na kampuni ya Sheria nchini China ambayo ina wafanyakazi zaidi ya 5,000 na wateja zaidi ya 50,000 na kati yake kuna kampuni ambazo zinataka kuwekeza nje ya China.

Amesema kushirikiana nao kunaweka urahisi wa wawekezaji kutoka eneo hilo kujua sheria na taratibu za uwekezaji nchini na inaweka urahisi kwao kuwashauri wawekezaji.

“Kuanzia hapo tulianza kuangalia baadhi ya nchi za kimkakati ambazo tunaweza kushirikiana nazo, pia kampuni ambazo zina mitandao mipana ili ziweze kuvutia uwekezaji nchini,” amesema Teri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Africapital Investiment Holding Limited, Burak Kuyuksarac amesema ni makubaliano ya kwanza kufanywa na taasisi ya Serikali nchini.

Amesema mkakati ni kwenda kusaini mkataba kama huo na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa).

“Mbali na kuangalia wawezekaji pia tutaangalia namna ya kuwezesha mawazo bunifu (startups), huku baadhi ya watu wanavutiwa zaidi katika teknolojia za kifedha, kilimo na hata wanaofanya biashara kwa njia ya mtandao,” amesema.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories