Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanzisha mfumo wa malipo ya ada ya nyongeza (Top up tuition fees) ambayo itawasaidia wanafunzi kukamilisha gharama za masomo vyuoni kwa kufidia asilimia iliyopungua baada ya kupata mikopo.
Pia, Serikali imeimarisha huduma kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ikiwemo bima ya afya na kuongeza fedha za matumizi kutoka Sh1.3 milioni hadi Sh1.5 milioni kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Akizungumza wakati akifungua maonyesho ya tano ya wiki ya elimu ya juu katika uwanja wa Maisara kisiwani hapa leo Alhamisi, Julai 18, 2024, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema mfumo huo utawawezesha wanafunzi kukamilisha masomo yao.
“Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kila mwanafunzi anayefaulu kwenda chuo kikuu hakosi masomo kwa sababu ya kushindwa kulipa ada,” amesema.
Amesema wanafunzi wanaosoma Tanzania Bara wameongezewa fedha za matumizi kutoka Sh1.5 milioni hadi kufikia Sh1.8 milioni ili waweze kumudu gharama wanapokuwa vyuoni.
Sambamba na hayo, Hemed amesema Serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar (ZHESLB) kutoka Sh26.93 bilioni mwaka 2023/24 hadi Sh30.5 bilioni mwaka 2024/25.
Amesema fedha hizo zitawanufaisha wanafunzi 7,367, wakiwemo 4,297 wanaoendelea na masomo, wapya 3,070 na 1,000 wa stashahada.
“Kupitia maonyesho ya wiki ya elimu ya juu wanafunzi hupatiwa taarifa mbalimbali za kimasomo zikiwemo za upatikanaji wa mikopo, namna ya kujiunga na vyuo vya ndani na nje ya nchi na kutoa hamasa kwa wanafunzi kusoma kwa bidii,” amesema Abdulla.
Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa amesema kazi inayofanywa na Serikali ya kuimarisha miundombinu ya elimu inasababisha ongezeko la ufaulu na kuiletea heshima Zanzibar.
Miongoni mwa mafanikio amesema ni kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha sita kutoka wanafunzi 2,570 mwaka 2023 sawa na asilimia 99.3 hadi wanafunzi 3,387 sawa asilimia 99.5 kwa mwaka 2024.
Amesema wanafunzi hao wamepata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu na wote wanatarajiwa kujiunga na vyuo vikuu ndani na nje ya nchi.
“Maonyesho ya elimu ya juu yatawasaidia wanafunzi katika kufanya udahili wa vyuo na kupata taaluma ya juu, kupata mikopo ya elimu juu itakayowezesha kusoma pasipo na changamoto ya aina yoyote,” amesema Lela.
Akisoma taarifa ya kitaalamu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (Utawala), Khalid Masoud Waziri amesema lengo kuu la maonyesho hayo ni kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za elimu, vyuo na benki ili kuhakikisha sekta ya elimu inaendelea kuimarika na ufaulu kuongezeka.
Hata maonyesha yenyewe, Khalid amesema yanazidi kuimarika kwani mwaka 2020 washiriki kutoka taasisi za elimu walikuwa 17, mwaka 2023 wakafikia 54 na mwaka huu wapo 77.
Source: mwananchi.co.tz