Dar es Salaam. Serikali na wadau wa teknolojia wamedhamiria kuziinua kampuni changa bunifu (startups), ili kufikia malengo ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya utoaji zawadi kwa washindi watatu wa mashindano ya ubunifu kwenye teknolojia (U.S Tanzania Tech Challenge 2024) iliyoandaliwa na ubalozi wa Marekani na kuwakutanisha vijana 100 kwenye mashindano hayo yaliyoanza Juni mwaka huu.
Akizungumza Meneja wa Ubunifu na Teknolojia kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Gerald Kafuku amesema Serikali ina programu za kuwafikisha hatua kubwa wabunifu hapa nchini ambayo inaendelea kuzitekeleza.
“Kama nchi tunaweka mazingira ambayo matumizi ya Tehama yaweze kwenda katika kila sekta ikiwemo uchumi na matumizi ya akili mnemba yasiwe ya kuogopa tena,” amesema.
Katika kusaidia ukuaji wa kampuni changa za kiteknolojia, Dk Kafuku amesema Tanzania ina wabunifu karibu 200 na wenye kampuni za kiteknolojia wako 33 zinazosaidiwa na Serikali.
“Serikali tuna wabunifu karibu 200 na walio na kampuni wako 33 na wengine wanazo kampuni hadi Dubai na Jamhuri ya Kidemokrasua ya Congo. Tunazidi kusaidia kampuni changa nyingi hadi zinakua kubwa,” amesema.
Amesema katika kuwawezesha vijana, wapo 20 waliopitishwa jana na sasa wamefikia uwezo wa kuanza kuzalisha fedha.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Jamii Forums, Maxence Melo amesema kupitia Jamii Check wanasaidia jamii kwa kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi ili waweze kufanya maamuzi.
“Jamii Forums kama taasisi inayosaidia jamii iliamua kuja na Jamii Check ili wananachi wafanye maamuzi sahihi kupitia taarifa sahihi baada ya kufanya tafiti,” amesema.
Amesema waliamua kuanzisha Jamii Check ili kutatua changamoto za wananchi na si kwa ajili ya kupata pesa, hivyo ameshauri wanaoanzisha bunifu wawe na lengo la kusaidia jamii kwanza kabla ya kuwaza kupata fedha.
Loth Makuza kutoka kampuni ya Smart Foundry miongoni mwa washindi hao watatu amesema wanawasaidia watu na kampuni mbalimbali kusoma magazeti kupitia progamu yao maalumu waliyoianzisha kwa ajili ya kurahisisha wasomaji hao.
“Tumerahisisha watu na kampuni kusoma magazeti kupitia application yetu na wameacha kusoma magazeti ya karatasi kisha kuyatupa,” amesema.
Balozi wa Marekani hapa Tanzania Dk Michael Battle amesema ni wakati wa vijana wa Tanzania kutumia fursa ya teknolojia kujiajiri huku akisema ni wakati wao kufanya vizuri.
“Kwa wale ambao wanataka kuwa wabunifu na kubadilisha uchumi, basi pata mshirika mwenye mawazo kama yako, mtu ambaye anataka kuleta mabadiliko na kuisadia jamii.
Awali Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Jerry Silla amesema ubunifu wa kidijitali ndio njia pekee itakaowezesha vijana kujiajiri na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Source: mwananchi.co.tz