Serikali yaongeza posho kwa madaktari, wauguzi

Serikali yaongeza posho kwa madaktari, wauguzi

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imeongeza posho za madaktari anapoitwa nje ya saa za kazi, posho ya sare za wauguzi na ile ya kuchunguza maiti kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miaka mingi imepita tangu madaktari na wauguzi nchini, kuomba ongezeko hilo.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Julai 31, 2024 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akitaja maazimio ya mkutano wa siku tatu wa rasilimali watu ulioandaliwa ndani ya Kumbukizi ya Hayati Benjamin William Mkapa uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

“Miongoni mwa maazimio ni pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi tutaendelea kufuata maelekezo yako Rais Samia Suluhu Hassan katika hili.

“Tumeshaanza utekelezaji wa kuongeza ‘OnCall allowance’ za madaktari zilikuwa hazijaongezwa, posho ya sare ya wauguzi, posho ya kuchunguza maiti na nyingine kuanzia Julai hii na hili ulituelekeza,” amesema.

Amesema miongoni mwa mambo yaliyoibuka katika kongamano hilo ni uzalishaji wa madaktari, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa maabara na kukosekana kwa ajira.

“Madaktari na wataalamu tunazalisha wengi kupitia vyuo vyetu na hatuwapi ajira, lazima tutatue changamoto hii. Tutakaa na mabaraza ya wanataaluma wakiwemo MAT, wafamasia, wauguzi, maabara tukubaliane njia bora ya kudhibiti watumishi wa afya ambao wapo barabarani,” amesema Waziri Ummy.

Amesema miongoni mwa maazimio ni pamoja na kuhakikisha hospitali zinaajiri watumishi wa mikataba na kwamba mchakato wa bima ya afya kwa wote utakapokamilika utaziwezesha na hospitali za chini kuajiri watumishi wa mikataba.

Ametaja maazimio mengine ni kuendeleza kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, kuendeleza huduma za ubingwa kwa kuwasomesha wataalamu bingwa na bobezi kama ambavyo Serikali imeendelea kuwasomesha.

“Uendelezaji wa watumishi wa afya kwa sasa tumejenga sana hospitali za Kanda na mikoa ambazo hazina wataalamu na mwaka huu Sh9 bilioni zimetolewa kusomesha ubingwa na ubingwa bobezi na sasa watumishi 708 wamehitimu na tumewapangia vituo,” amesema.

Akizungumzia alama alizoziacha Mkapa, Waziri Ummy amesema: “Mwaka 1999 Serikali yake iliwasilisha sheria ya bima ya afya ilianza utekelezaji ulianza mwaka 2001 kwa wanufaika 991,773 bado inaishi na sasa NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya) ina wanufaika 4,809,000 sawa na asilimia 8 ya Watanzania.”

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories