Dodoma. Kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini kuharibu miundombinu ya barabara na eneo la uhifadhi kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka za hifadhi za Taifa (Tanapa) linaandaa andiko la kuomba kukarabati barabara hizo kwa kiwango cha zege na lami.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Machi 10, 2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusiana na hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Amesema sababu za kuomba kibali kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ni kwamba hifadhi za Taifa katika nchi mbalimbali duniani huwa zinapata hadhi maalumu ya kuorodheshwa kwenye urithi wa dunia ambayo inasimamiwa na Unesco.
Amesema kuna kamati inayosimamia hifadhi hizo ambazo zinatunzwa kwa pamoja kati ya Unesco na nchi mwenyeji, kuna kanuni za msingi za uhifadhi ambazo zinapaswa kufuatwa na Unesco huwa inasaidia kitaalamu au msaada wa kifedha, ili kuhakikisha hifadhi hizo zinatunzwa.
“Kwa hiyo, inapotakiwa kufanyika mambo ya msingi kama miundombinu ikiwemo ujenzi wa hoteli au barabara kunakuwa na mashauriano, ili kuhakikisha urithi ule wa dunia unabaki na sifa zilezile ambazo zilisababisha ukakubalika kuwa katika orodha ya urithi wa dunia,” amesema.
Matinyi amesema kutokana na uharibifu uliotokea kwenye hifadhi hiyo kwenye miundombinu ya barabara na eneo la uhifadhi kutokana na mvua za El Nino zilizoanza Oktoba 2023, Tanapa imeandaa andiko la kuomba ukarabati wa barabara hizo kwa kutumia tabaka gumu, ili kuzidumu kwa muda mrefu.
Amesema barabara zilizopo ndani ya hifadhi hiyo zilijengwa kwa kutumia udongo na changarawe na zimetumika kwa zaidi ya miaka 65 sasa, hivyo wanataka kukarabati kwa kutumia tabaka gumu la zege au lami.
Amesema udongo wa eneo la hifadhi ya Serengeti ni dhaifu, kwani unatokana na volcano iliyolipuka miaka mingi nyuma, hivyo ukipata maji kidogo unaharibika, huku changarawe zilizotumika kujenga barabara hizo huko nyuma kwa sasa hazipatikani.
“Njia ya kutumia andiko la kitaalamu ndiyo iliyotumiwa na mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro ambayo sasa imepata kibali cha kujenga barabara yenye tabaka gumu ambayo inaingia kwenye hifadhi ya Serengeti kwa kuzingatia kuwa vivutio hivi viwili maarufu duniani vinapakana.”
Amesema kuna barabara kuu nne zenye changamoto zaidi kutokana na upitaji wa magari makubwa ya abiria na mizigo yanayokwenda mikoa jirani ya Mara, Arusha Manyara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu ambayo imezunguka hifadhi ya Serengeti na kwamba barabara hizo ndizo zinazoingiza watalii kwa wingi.
Amesema barabara hizo hupitisha wastani wa magari 600 hadi 800 kwa siku kwa ajili ya kusafirisha watalii na hivyo kuharibu miundombinu yake hata kama hakuna mvua kubwa na zina urefu wa kilomita 291 ambayo ni asilimia tisa ya urefu wa barabara zote zenye urefu wa kilomita 3,176 za mtandao wa barabara ndani ya hifadhi hiyo.
Msemaji huyo wa Serikali amesema wameamua kuomba kibali hicho cha kuweka tabaka gumu kwenye barabara hizo kwa sababu matengenezo ya mara kwa mara yanaigharibu Serikali fedha nyingi tofauti na kuweka tabaka gumu kama ilivyo kwenye barabara za hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya na Kulga ya nchini Afrika Kusini.
Amesema changamoto nyingine ni uhaba wa maji kwenye hifadhi hiyo ambayo hutumika kukarabati barabara zilizojengwa kwa udongo na changarawe kwa kutumia maji ya visima ambayo kwa sasa hayapatikani kwa wingi kama ilivyokuwa zamani, hivyo wanashindwa kuzikarabati kwa kutumia maji ya mito ambayo ni kwa ajili ya wanyama tu.
“Tanapa inatarajia kwamba utatuzi wa kudumu utapatikana katika barabara kuu hizi zinazoihudumia Serengeti na hivyo kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kiasi kikubwa kutokana na matunda ya filamu ya Royal Tour na kutoa mchango mkubwa katika pato la jumla la utalii ambalo nalo linachangia katika pato la jumla la nchi yetu,” amesema.
Amesema Serengeti ni hifadhi ya Taifa ambayo inaliingizia Taifa fedha nyingi kwa kuwa watalii wengi hupenda kutembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kujionea wanyama wakubwa duniani na uhamaji wa wanyama aina ya nyumbu kwenda nchini Kenya na kwamba imechukua tuzo ya hifadhi bora Afrika kwa miaka mitano mfululizo.
Amesema hifadhi hiyo imeingiza watalii 1,451,176 kwa miezi minane pekee kutoka ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Februari 2024 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo lengo lilikuwa ni kufikisha watalii 1,387,987, hivyo imevuka lengo hilo kwa kipindi cha miezi minane pekee.
Source: mwananchi.co.tz