
Dar es Salaam. Wasiwasi unaendelea kuongezeka kuhusu wafanyabiashara wa kigeni kuingilia biashara za wazawa, huku Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) likitaka hatua za haraka kulinda biashara za Watanzania.
Akizungumza katika tuzo za Wanawake Wajasiriamali wa Sekta ya Viwanda na Biashara Jumatano jioni, Rais wa TPSF, Angelina Ngalula, alisema raia wa Kichina, ambao awali huingia sokoni kama wawekezaji, wanazidi kujihusisha na biashara zinazopaswa kufanywa na wafanyabiashara wa ndani.
Tuzo za Wanawake Wajasiriamali wa Sekta ya Viwanda na Biashara ziliandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC).
Ngalula alisisitiza kuwa hali hiyo inatishia uhai wa wajasiriamali wa Kitanzania na kuhujumu uhuru wa kiuchumi wa taifa.
“Hakuna namna China inaweza kushindana na Tanzania, wala mfanyabiashara wa Kichina hawezi kushindana na mfanyabiashara wa Kitanzania katika biashara hizi zetu. China ni nchi yenye uchumi mkubwa; hawawezi kulinganishwa nasi.
“Inawezekanaje mfanyabiashara wa Kichina aje kushindana kibiashara na mfanyabiashara wa Kitanzania?” alihoji Ngalula.
Aliitaka Serikali kuwa na kanuni kali ili kuzuia wawekezaji wa kigeni kuendesha biashara katika sekta zilizotengwa kwa ajili ya wenyeji.
Februari 2025, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, aliteua kamati maalumu yenye wajumbe 15 kuchunguza uwepo wa wafanyabiashara wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo zisizo rasmi, maarufu “Umachinga,” katika Soko la Kariakoo na maeneo mengine nchini.
Uamuzi huo ulitokana na ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni moja ya hatua za kutatua malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani, hususan wa Kariakoo, kuhusu ongezeko la wageni wanaofanya biashara katika sekta isiyo rasmi.
Dk Jafo alieleza kuwa, badala ya kuwekeza kwenye miradi mikubwa, baadhi ya wageni wanajihusisha na biashara ndogo zisizo rasmi, jambo linaloathiri biashara za wenyeji.
Kamati hiyo ilipomaliza kazi kwa siku zilizopangwa, ilibaini wafanyabiashara wengi wa kigeni wanafanya biashara zinazofanywa na wazawa, huku wakiuza bidhaa kwa bei ya chini, jambo linaloondoa ushindani sokoni.
Kamati hii pia ilibaini wageni kutumia vitambulisho vya uraia vya Watanzania kusajili biashara zao. Pia, katika maduka 75, walikutwa raia wa kigeni 152 waliajiriwa, huku asilimia 97 kati yao wakijihusisha na biashara za rejareja, 28 wakiishi nchini kinyume na sheria, na 24 wakiondolewa nchini.
Katika kushughulikia suala hilo, kamati hiyo ikiongozwa na Profesa Edda Lwoga, ilipendekeza ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuanzisha kanda maalumu ya biashara Kariakoo na kanzidata na kulifanya eneo hilo kuwa na hadhi maalumu ya biashara.
“Hilo liende sambamba na kutenga maeneo ya biashara za jumla na rejareja, kuwa na huduma za utoaji huduma za Serikali sehemu moja. Pia, inashauriwa Wizara ya Viwanda na Biashara ipitie na kurekebisha Sera ya Maendeleo ya Biashara ya mwaka 2003, toleo la mwaka 2023, ili iainishe aina ya biashara ambazo wageni wanapaswa kufanya,” alisema Profesa Lwoga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Jafo aliunga mkono maoni ya Ngalula, huku akiwahakikishia wajasiriamali kuwa Serikali inachukua hatua kudhibiti ushindani usio wa haki.
Alisema kuwa Serikali, kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imeweka mikakati ya kusimamia shughuli za biashara kwa watu wa jinsia zote, wakiwemo wanawake wajasiriamali, ambao wanapata msaada mkubwa kutokana na umahiri wao wa kusimamia fedha za mitaji.
“Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya biashara. Hata hivyo, wanawake ni nguvu kubwa, na tunatambua ujuzi wenu wa kipekee katika kusimamia biashara, mitaji, na fedha. Kwa hiyo, Serikali itawaunga mkono popote na wakati wowote mtakapoonesha dhamira ya kusonga mbele kibiashara kwa manufaa ya taifa,” alisema Dk Jafo.
Ngalula pia aliwataka wanawake wajasiriamali kuwa makini, kushikilia misingi imara ya biashara, na kupigania nafasi yao halali katika uchumi.
Kwa upande wake, Mwajuma Hamza, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, alisema tuzo za Wanawake Viwandani Tanzania ni fursa ya kusherehekea wanawake wa kipekee wanaoleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali, ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu na ujasiriamali.
“Maadhimisho ya mwaka huu pia yana umuhimu maalumu, kwani yanaambatana na maadhimisho ya miaka 30 ya Jukwaa la Beijing la utekelezaji, ni hatua muhimu ya kimataifa katika kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake,” alisema.
Alisema tukio hilo ni la kihistoria, lililopitishwa mwaka 1995, na limekuwa msingi wa mikakati mbalimbali ya kuimarisha haki za wanawake na uongozi wao duniani.
“Tanzania imekuwa kinara katika kutekeleza Jukwaa la Beijing, jambo ambalo limechangia maendeleo makubwa kwa wanawake katika sekta mbalimbali. Moja ya matokeo ya kuvutia zaidi ni ongezeko la wanawake wajasiriamali mabilionea ambao wamebadilisha taswira ya biashara nchini, wakionesha matokeo chanya ya sera zinazolenga kuwawezesha wanawake,” amesema.
Source: mwananchi.co.tz