Sarafu mtandao zawaingiza matatani walimu wanne, mfanyabiashara

Sarafu mtandao zawaingiza matatani walimu wanne, mfanyabiashara

Dodoma. Walimu wanne na mfanyabiashara mmoja wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwatapeli wananchi kwa kuwadanganya kuwekeza katika sarafu za kimtandao (cryptocurrency), kisha kutoweka na fedha walizowekeza.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ametoa taarifa leo Septemba 11, akieleza kuwa watuhumiwa walikamatwa Septemba 7, 2024, katika Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza kufuatia malalamiko ya wananchi waliodhulumiwa.

Ingawa Misime hakuwataja walimu hao wala shule wanazotoka, amefafanua kuwa watuhumiwa wamehusishwa na ulaghai kwa kufungua mifumo ya kampuni bandia ili kuvutia uwekezaji wa wananchi.

Majina ya baadhi ya kampuni hizo ni MEME BANK, DIGITAL WEALTH INTERNATIONAL, OCTOQUANT AI TRADING, NPAMA FUND, MINDFUL TRADE, na CELESTRIAL TG CRYPTOCURRENCY.

Misime amesema kuwa matapeli hao huanzisha kampuni hizo na kuwapa wawekezaji wa awali fedha kidogo kama faida ili kuvutia wengine wawekeze zaidi.

Hata hivyo, baada ya kukusanya kiasi kikubwa cha fedha, kampuni hizo hufungwa na matapeli hao kutoweka mtandaoni, na kuwafanya wawekezaji kushindwa kuwasiliana nao.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari na kuepuka kujiingiza kwenye udanganyifu huu, kwani teknolojia ya uwekezaji wa sarafu za kimtandao bado haijaidhinishwa rasmi nchini.

Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa wanapoona ulaghai wowote unaohusisha uwekezaji mtandaoni au biashara za aina hiyo, ili kuepusha kupoteza fedha zao.

Misime amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha uhalali wa makampuni au watu wanaohamasisha biashara za mtandaoni kabla ya kujiingiza, kwani wengi wamejikuta wakiibiwa fedha kutokana na kuingia kwenye matapeli wa mtandaoni.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories