Dar es Salaam. Unyeti wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania na rundo la wajibu unaotegemea utashi wa wizara nyingine, ndiyo sababu iliyotajwa na wadau kuifanya wizara hiyo iwe mapito ya muda mfupi kwa kila anayeteuliwa.
Kauli hiyo ya wadau inakuja, wakati ambao Wizara ya Maliasili na Utalii imeonekana kukumbwa na kila mabadiliko ya baraza la mawaziri yanayofanywa na mamlaka ya uteuzi.
Waziri wa sasa katika wizara hiyo ni Dk Pindi Chana aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan jana Agosti 14, 2024 akichukua nafasi ya Angellah Kairuki aliyehudumu kwa miezi 11 pekee.
Si ajabu katika historia ya wizara hiyo, kukuta waziri amehudumu muda mfupi kama aliohudumu Kairuki na wengine wametumikia chini ya muda huo.
Kwa kipindi cha miaka 19, tangu 2005 alipoingia madarakani Jakaya Kikwete hadi sasa Agosti mwaka 2024, Wizara ya Maliasili na Utalii imetumikiwa na mawaziri 14.
Hiyo ni sawa na kila waziri amehudumu wastani wa mwaka mmoja na miezi mitatu ndani ya wizara hiyo kwa kipindi hicho cha miaka 19.
Lakini, tangu uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Wizara ya Maliasili na Utalii, imetumikiwa na mawaziri 27 hadi sasa. Sawa na kila waziri amehudumu kwa wastani wa miaka miwili na miezi mitatu.
Zakhia Megji ndiye mwanasiasa mwenye rekodi ya pekee ya kudumu zaidi ndani ya wizara hiyo, akihudumu tangu mwaka 1997 alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa hadi mwaka 2005.
Mawaziri tangu uhuru
Baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Tewa Tewa ndiye aliyefungua pazia la utumishi katika wizara hiyo akiteuliwa na Baba wa Taifa, Julius Nyerere mwaka 1962 hadi 1965.
Aliyemfuata ni Dereck Bryceson aliyehudumu kuanzia mwaka 1965 hadi 1970, kisha Hosnu Makame aliyekuwa waziri kuanzia mwaka 1970 hadi 1975.
Upepo wa kuhudumu kwa miaka mitano mitano, uliishia kwa Solomon Saibul aliyeongoza kuanzia mwaka 1975 hadi 1980 na waliofuatia ilikuwa ni mwaka mmoja, miwili au mitatu isipokuwa Megji pekee.
Saibul alifutiwa na Isaack Sepetu kuanzia 1980 hadi 1982, kisha Ali Hassan Mwinyi aliyehudumu kuanzia 1982 hadi 1983 na alifuatiwa na Geogre Kahama mwaka 1983 hadi 1984.
Wengine ni Paul Bomani (1984-1985), Getruda Mongela (1985-1987), Arcardo Ntagazwa (1987-1989), Marcel Komanya (1989-1990), Abubakar Mgumia (1990-1993), Juma Omar (1993-1995) na Juma Ngasongwa (1995-1996).
Baadaye walifuata, Zakhia Megji (1997-2005), Anthony Diallo (2005-2006), Jumanne Maghembe (2007-2008), Shamsa Mwangunga (2008-2010), Ezekiel Maige (2010-2012) na Khamis Kagasheki (2012-2013).
Mbali na hao, Lazaro Nyalando alihudumu (2014-2015), Jumanne Magembe (2015-2017), Dk Hamisi Kigwangallah (2017-2020), Dk Damas Ndumbaro (2020-2022), Dk Pindi Chana (2022-2023), Mohammed Mchengerwa (Februari 2023- Agosti 30, 2023), kisha Angellah Kairuki (2023-2024) na sasa amerudi tena Dk Chana.
Kwa nini mabadiliko?
Unyeti wa wizara hiyo na uzito wa majukumu ndani yake ni moja ya sababu za mabadiliko ya mara kwa mara, kama inavyoelezwa na Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli za Kitalii Tanzania (HAP), Kennedy Mollel.
Kinachoipa unyeti wizara hiyo ni kile alichoeleza, imebeba sekta inayoingiza fedha za kigeni zaidi ya eneo lingine lolote na yenyewe imejikita katika huduma na sio bidhaa.
Sambamba na unyeti, amesema wizara ya utalii inagusa sekta nyingine zote na utendaji wake unahitaji mazungumzo na mawaziri wa wizara nyingine, ili kutatua changamoto zitakazoibuliwa na wadau.
“Mwekezaji wa utalii anaweza kusema gharama za kuendesha biashara ni kubwa, lakini hili halitokani na Wizara ya Maliasili na Utalii ni wizara nyingine kama ya fedha, kazi, ofisi ya makamu wa rais mazingira.”
“Leo hii ukiwa Waziri wa Maliasili na Utalii wadau wako wakija wanakwambia changamoto yetu iko wizara ile pale kwa hiyo ukaongee na waziri yule pale,” amesema.
Katika mazingira hayo, amesema waziri wa wizara husika anajikuta na jukumu la kuwaomba mawaziri wenzake vitu vingi kwa ajili ya wizara yake.
“Kwenye kuomba sasa napo kuna gharama zake. Unamuomba mtu afanye mabadiliko yatakayoinufaisha wizara yako na wakati mwingine yanaathiri wizara yake, huwa hali inakuwa ngumu,” amesema.
Kwa msingi huo, amesema kila waziri anayeingia atajikuta anajikita katika maeneo yaleyale yaliyozoeleka kufanywa, lakini si kuondoa vikwazo na kukuza zaidi idadi ya watalii.
Amesema kuna haja ya nchi kukaa pamoja na kuona namna ya kuiendesha biashara ya sekta hiyo, ili waziri atakayewekwa awe na misingi ya kufuata wakati wa utendaji wake.
Mollel amependekeza kutengenezwe malengo ya muda mrefu ya kutangaza vivutio na fursa mbalimbali za utalii ndani yake, ambapo kila waziri atapaswa kutekeleza hayo.
“Kila anayekuja atatekeleza malengo hayo na akitoka anayefuata ataanzia alipoishia mwenzake na sio kuja na mipango mipya. Hivi ndivyo watadumu, badala ya kila mtu kuja na vipaumbele vyake, kila siku watabadilishwa,” amesema.
Kuna tatizo la mfumo
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Out), Dk Revocatus Kabobe amehisi uwepo wa tatizo la kimfumo wa utendaji ndani ya wizara ndiyo unaofanya kila waziri aonekane hatoshi.
“Wizara hii imekuwa ikifanyiwa mabadiliko mengi tangu uhuru mpaka sasa. Pamoja na kwamba sababu za utenguzi wa mawaziri wa wizara mbalimbali anazo mteuzi, kwa maoni yangu nadhani kuna tatizo la kimfumo kwenye utendaji kazi ndani ya wizara hii ambao bado haujapatiwa tiba sahihi tangu uhuru,” amesema.
Ingawa utenguzi wa mawaziri unaweza kuambatana na sababu mbalimbali ukiwemo utendaji usiokidhi malengo ya mteuzi, amehoji kwa nini hali hiyo iwe zaidi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii?
Hata hivyo, amesema utalii ni miongoni mwa sekta muhimu na inayochangia mapato mengi serikalini, ukiondoa madini.
Kwa kigezo hicho, amesema mikikimikiki ya wizara hiyo haiwezi kuwa rahisi kama sekta nyingine ambazo uchangiaji wa mapato kwa mfuko mkuu wa Serikali ni wastani.
Wingi wa vishawishi vya rushwa ni jambo lingine lililotajwa na Dk Kabobe kuwa sababu ya mawaziri kuhudumu kwa muda mfupi zaidi ndani ya wizara hiyo.
Lakini, amehusisha wingi wa changamoto ikiwemo vita ya ujangili, migogoro ya hifadhi za wanyama na binadamu, ugawaji vitalu, migongano baina ya watendaji na ukiukwaji wa haki za binadamu yote yanachochea kumuondoa waziri madarakani iwapo hatasimamia vema.
“Haya yote sio mambo rahisi yanahitaji msuli wa kuyakabili na msuli wenyewe haupaswi kuwa wa mtu bali wa kimfumo na kimkakati.
“Kwa maoni yangu, siamini kama kweli wale wote wanaoteuliwa wana uwezo mdogo wa kuongoza wizara hii la hasha. Nadhani kuna tatizo la kimfumo katika utendaji ndani ya wizara hii,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa mamlaka kutazama upya mfumo wa utendaji ndani ya wizara hiyo aliyoitaja kama miongoni mwa zile muhimu katika Taifa.
Kitakachomkabili Pindi
Kibarua kitakachomkabili Waziri anayeingia sasa, Mollel amesema ni kuendana na uchumi wa kidijitali ambao ndiyo mwenendo wa ulimwengu wa sasa.
Jukumu lingine, amesema ni kuhakikisha anatangaza utalii sio tu kwa kuishia Serengeti, Kilimanjaro na Zanzibar, matangazo yahusishe vivutio vingine ikiwemo Mkomazi na maeneo mengine.
“Atakuwa na kazi ya kuhakikisha kwa muda wa miezi minne iliyosalia anatimiza malengo yaliyowekwa na Serikali ya kufikisha watalii milioni tano kufikia mwaka 2025. Hili atatimiza iwapo atakuja na mkakati utakaomshawishi mtalii aliyekuwa na lengo la kukaa wiki moja avutiwe kukaa wiki tatu nchini,” amesema.
Source: mwananchi.co.tz