
Dar es Salaam. Kukosekana kwa mazingira rafiki ambayo yanaweza kuleta faida kwa mwekezaji imetajwa kuwa moja ya sababu inayofanya baadhi ya wabunifu kuendeleza mawazo yao katika nchi nyingine tofauti na zile wanazotoka kama Tanzania.
Hili limesemwa leo Jumatano katika mkutano uliowakutanisha wadau wa elimu kutoka vyuo mbalimbali kujadili masuala ya uhaulishaji na namna wanavyoweza kuyafanya matokeo ya utafiti na bunifu kuwa biashara.
Mkutano huo wa siku tatu umeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Programu ya funguo iliyo chini ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) ukikutanisha wataalamu kutoka nchini Kenya, India, Uingereza, Uganda na Tanzania.
Kauli hii imekuja wakati ambao Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeshuhudia baadhi ya bunifu za raia wake kufanya vizuri katika mataifa mbalimbali ambako zimeendelezwa jambo ambalo linaifanya nchi kushindwa kunufaika moja kwa moja.
Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa National Innovation Agency, Dk Tonny Omwansa amesema mara nyingi wabunifu wamekuwa wakipata fedha kutoka Ulaya na Marekani hata hivyo wawekezaji wanataka fedha zao zirudi kupitia faida itakayotengenezwa.
Amesema jambo hilo linafanya sasa mwekezaji kuangalia mazingira ambayo wazo hilo litakwenda kutekelezwa, Ikiwa mazingira hayatakua ya kuvutia na wamepata wazo zuri, watamwambia mbunifu kusajili wazo lake katika soko jingine ili waweze kuwekeza.
“Hiyo ndiyo maana ya uwekezaji, wanawekeza fedha ili waweze kupata fedha zao tena. Wanataka kuona faida kutokana na mawazo yanayotekelezwa, sasa hapa sera na motisha ndiyo vinaingia. Wawekezaji wanatafuta motisha ili kuwa na uhakika kwamba rasilimali zao zitaongezeka,” amesema Dk Tonny.
Amesema ikiwa motisha haziko vizuri inatengeneza uwezekano mkubwa wa kumhamishia mbunifu katika soko lingine ndiyo waweke fedha zao.
Amesema jambo jingine linaloweza kufanya bunifu kuhamishwa ni nchi za Afrika kuwa na utamaduni ambao unafanya watu kushindwa kuaminiana.
Utamaduni huu pia unaenda hadi katika kujenga timu na mtandao utakaowafanya wawekezaji kuwa na uhakika kwamba mawazo yanasimamiwa na timu nzuri ya watu inayoweza kuleta matokeo chanya.
“Kwa sababu wazo halitakuwa lenyewe, unahitaji ujuzi mbalimbali, unahitaji ujuzi wa masoko, unahitaji ujuzi wa kiufundi, unahitaji ujuzi wa kisheria, unahitaji ujuzi wa maendeleo ya biashara hivyo ni lazima ujenge timu inayoweza kukuza mawazo hayo kwa njia hiyo. Na hivyo, wawekezaji watakuwa na uhakika zaidi wanapoona aina hizo za timu,” amesema.
Jambo jingine ambalo ni changamoto ni namna wabunifu wanavyofikiri, huku akifafanua kuwa wawekezaji huangalia namna anavyoweza kutengeneza fedha zaidi kwa kuangalia soko kubwa liko wapi.
“Wao huwa wanajua kwamba soko haliko tu hapa labda Kenya au Tanzania, wanaangalia soko la kimataifa, hivyo, ikiwa tutafanya mawazo yetu kuwa ya kuvutia soko la kimataifa hii inamaanisha kuwa tunahitaji baadhi ya maonyesho, tunahitaji mitandao, tunahitaji ushirikiano ili kuleta suluhisho hizi kwenye masoko mengine,” amesema.
Amesema ikiwa wazo haliwezi kupanuliwa katika soko la ndani na nje basi linakuwa si la kuvutia hivo ni lazima kuhakikisha mawazo yanayotengenezwa yanakuwa ya kuvutia zaidi kwa wawekezaji wa ndani ya nchi husika na hata kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu amesema Serikali imeweka fedha nyingi kuhakikisha bunifu na tafiti zinakuwa na matokeo chanya hivyo ni wakati wa kuangalia namna zinavyoweza kwenda sokoni.
“Dunia ni kijiji hatufanyi kazi peke yetu tunafanya kazi kwenye ulimwengu hivi sasa hivyo tukikutana kama hivi tunabadilishana uzoefu kwa sababu Tanzania tukiwa na utafiti na ubinfu unaweza kutumika Tanzania na nje, hivyo tunapoona mapungufu kwetu tunajitahidi tuyaondoe pale kwenye fursa tubadilishane uzoefu,” amesema Dk Nungu.
Amesema kinachofanyika sasa kinaendana na kasi ya serikali ya kuhakikisha matokeo ya tafiti na bunifu yanafika sokoni.
Source: mwananchi.co.tz