Rufaa ya Mbowe yatupwa siku 910 tangu afutiwe shitaka la ugaidi

Rufaa ya Mbowe yatupwa siku 910 tangu afutiwe shitaka la ugaidi

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani Tanzania imetupa rufaa iliyokatwa na Freeman Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akipinga uamuzi wa Jaji Irvin Mgetta.

Hukumu hiyo ya jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, imetolewa zikiwa zimepita siku 910 tangu Mbowe na wenzake watatu wafutiwe mashitaka ya ugaidi na Mahakama Kuu Machi 4, 2022.

Hukumu hiyo imetolewa Agosti 30, 2024 na jopo la majaji Lugano Mwandambo, Issa Maige na Amour Khamis, ambao walikubaliana na uamuzi wa Jaji Mgetta wa Septemba 23, 2021 wa kutupa pingamizi la Mbowe.

Kiini cha rufaa hiyo ni kesi ya ugaidi ya mwaka 2021 ambayo Mbowe na wenzake watatu walishitakiwa kwa makosa mawili, moja la kula njema ya kutenda kosa la ugaidi, na la pili ni kutoa fedha kwa lengo la kufadhili vitendo vya ugaidi.

Hata hivyo, Machi 4, 2022, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), alimfutia Mbowe na wenzake Halfan Hassan, Adamu Kusekwa na Mohamed Ling’wenya, mashitaka ya uhujumu uchumi na kuwaachia huru.

Msingi wa rufaa hiyo siyo uamuzi wa Jaji Joachim Tiganga wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kuifuta kesi hiyo, bali uamuzi mdogo wa Jaji Mgetta katika shauri hilo, wakati kesi ikiwa hatua za mwanzo.

Mbowe alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Jaji Mgetta aliyetupa pingamizi lake, moja akidai polisi hawakumfikisha mahakamani ndani ya saa 48, alipokamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya ugaidi na wenzake watatu.

Hoja ya pili ya Mbowe ni wajibu rufaa katika rufaa hiyo ambao ni DPP, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kutompatia hati ya mashitaka na fursa ya kupata wakili wa kumtetea kortini.

Pingamizi lilivyokuwa

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama Kuu kuhusu pingamizi la Mbowe ambazo majaji wa Mahakama ya Rufani wamezirejea, Mbowe alidai Julai 21, 2021 kwa amri ya IGP alikamatwa na Polisi akiwa jijini Mwanza.

Julai 26, 2021 ikiwa ni baada ya kupita siku sita tangu alipokamatwa alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa makosa mawili ambayo ni kula njama ya kutenda kosa la ugaidi na kufadhili vitendo vya ugaidi.

Akishuku haki zake za msingi zimekiukwa, Mbowe aliwasilisha maombi Mahakama Kuu akiegemea ibara ya 30(3) na (4) ya Katiba ya Tanzania akitaka Mahakama itamke DPP, IGP na Mahakama ya Hakimu Mkazi walikiuka haki zake za msingi.

Katika hoja ya kwanza, Mbowe aliwashutumu DPP na IGP kwa kushindwa kumfikisha kortini ndani ya saa 48 na kwamba, licha ya kukamatwa Julai 21, 2021, wajibu rufaa walimfikisha kortini Julai 26, 2021 ambayo ni siku sita.

Kutokana na kitendo hicho, mrufani (Mbowe) anadai akiwa mahabusu, wajibu rufaa walimtendea vitendo visivyo vya kibinadamu na kufikia hatua ya kulazwa kwenye sakafu ya zege na kutolewa maneno au kauli za unyanyasaji.

Katika hoja ya pili, Mbowe alilaumu Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa kukiuka vifungu vya 29(2) na (3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na kifungu cha 131 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama kilivyofanyiwa marejeo 2019.

Alijenga msingi wa pingamizi hilo kuwa wajibu rufaa hawakumpa nakala ya hati ya mashitaka na hakupata uwakilishi wa wakili alipofikishwa mahakamani mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika kiapo cha majibu, wajibu rufaa walikana kukiuka haki za msingi za mrufani na wakaenda mbali zaidi na kuwasilisha notisi ya pingamizi la awali wakihoji uhalali wa maombi, wakisema kesi ya msingi ilikuwa kortini.

Jaji Mgetta aliyesikiliza pingamizi hilo, alikubaliana na wajibu rufaa akisema wakati huo kulikuwa na mwenendo wa shauri la jinai mahakamani, Mbowe akishitakiwa kwa makosa ambayo ndiyo kiini cha amri ambazo anaziomba.

“Nina mtazamo kuwa muombaji angeweza kutumia fursa ya kuibua madai hayo huko (Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu),” alisema.

Jaji Mgetta alisema Mbowe anafanya mahakama iingilie mchakato wa kesi ya jinai inayoendelea.

“Kwa hiyo katika mazingira hayo, nimeridhika kuwa Mahakama hii haina mamlaka ya kushughulikia madai yaliyowasilishwa na muombaji (Mbowe) ambaye angeweza kuwasilisha madai yake katika Mahakama inayosikiliza (Kisutu)”

Kutokana na hoja hizo, Jaji Mgetta alitupa pingamizi la Mbowe ambaye hakuridhika akaamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani, akiiomba ibatilishe na kufuta amri ya Jaji Mgetta na kuiamuru Mahakama Kuu isikilize pingamizi.

Wakili Kibatala, wanasheria

Wakati shauri la rufaa lilipoitwa mbele ya jopo la majaji watatu kwa ajili ya kusikilizwa, Mbowe aliwakilishwa na wakili Peter Kibatala, wajibu maombi wakiwakilishwa na mawakili wa Serikali, Daniel Nyakiha na Getrude Songo.

Katika hoja zake, Kibatala alieleza kwa kuwa nafuu inayoombwa na mteja wake inahusu Katiba, isingewezekana ishughulikiwe na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo mamlaka yake ni kuangalia hatia ya mshitakiwa.

Wakili Kibatala alisisitiza kuwa, mamlaka ya kusikiliza suala la kikatiba limewekwa pekee kwa Mahakama Kuu ambayo itakaa kwa madhumuni hayo na ni jambo lisilowezekana kwa suala la kikatiba kushughulikiwa na mahakama ya jinai.

Akijibu hoja hiyo, wakili Nyakiha alisema kwa kuwa malalamiko ya mrufani katika Mahakama Kuu ni kuhusiana na madai ya ukiukwaji wa taratibu katika utoaji haki, basi lingepaswa kushughulikiwa kwa mapitio ya mahakama.

Wakili Kibatala katika hoja ya kujazilia alisema nafuu inayoombwa na mteja wake kwa uasili wake, haiwezi kushughulikiwa kwa njia ya mapitio ya mahakama na kwamba, hoja mbele yao ni ya kikatiba ya matendo ya DPP na IGP.

Hukumu ya majaji

Kwa kuanzia, majaji waliosikiliza rufaa hiyo walianza kwa kuelezea Ibara ya 30(3) ya Katiba ambayo inatoa haki kwa mtu yeyote anayedai kifungu chochote cha ibara ya 13 hadi 29 ya Katiba imevunjwa, atawasilisha maombi Mahakama Kuu.

Wakirejea kesi ya mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya AG, walisema nafuu inaweza kutolewa katika shauri linalohusu haki za msingi na wajibu upo katika Ibara ya 30(4(5) ya Katiba ambayo imefafanuliwa katika kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Haki za Msingi na utekelezaji wa wajibu au kwa kifupi Bradea.

Kifungu hicho kinaeleza wakati wa kufanya maamuzi ya shauri lolote na kama Mahakama Kuu inafikia hitimisho haki za msingi, uhuru na wajibu ulizuiwa kinyume cha sheria, ina mamlaka ya kutoa amri yoyote ili kulinda haki hizo.

Hata hivyo, majaji walisema kifungu cha 8(2) cha Bradea, kinaeleza maombi kuhusu kukiukwa kwa Ibara ya Katiba chini ya sehemu ya II haiwezi kusimama pale mtu huyo anapokuwa na fursa ya kushughulikia ukiukwaji huo wa Katiba.

Majaji walisema, ieleweke kwamba madai ya mrufani yanahusiana na kukiukwa kwa taratibu za sheria ya uhujumu uchumi na CPA ambayo yanataka kulindwa kwa haki za msingi ambazo zimetamkwa na ibara ya 13 ya Katiba.

Kwa mtizamo wa majaji na kwa lengo la kupima jukwaa sahihi la kushughulikia hoja hizo, ni vyema kutofautisha kati ya matendo ambayo ni batili kisheria na yale ambayo yanahusu ukiukwaji wa Katiba ya Tanzania moja kwa moja.

“Tunasema hivyo kwa sababu katika nchi kama ya kwetu ambayo inaongozwa kwa utawala wa sheria na Katiba, kitendo chochote cha vyombo vya Serikali lazima kiwe na msingi katika Katiba,” inaeleza hukumu ya majaji hao na kuongeza:

“Ikiwa hii inachukuliwa halisi, inaweza kumaanisha kuwa kila ukiukwaji wa sheria unasababisha mapitio ya katiba ili kuchukua hatua na hii itafanya mamlaka ya mapitio ya Katiba kuwa sawa tu na mamlaka za jumla za mahakama.”

Majaji walisema dhamira ya watunga sheria ilikuwa ni mamlaka ya mapitio ya Katiba ni mamlaka maalumu kwa ajili ya masuala ya Katiba tu na kufafanua kuwa matendo yanayolalamikiwa yanadaiwa kutokea kabla na baada ya kufikishwa kortini.

“Kwa hiyo ni wazi matendo hayo ambayo yanadaiwa kufanyika kabla ya mrufani kupelekwa mahakamani na yanaweza kuwa tayari yalimuathiri na yangeweza yasishughulikiwe na mahakama ya jinai,” wameeleza.

“Vyovyote iwavyo, kwa kuwa kinacholalamikiwa kutendeka kinakatazwa na sheria, kama kitathibitishwa, basi ni matumizi mabaya ya mamlaka kiasi kwamba yanakiuka sheria ambayo yanaweza kushughulikiwa na mapitio ya mahakama,” wameeleza majaji katika hukumu.

Kwa mujibu wa majaji hao, lengo hilo la mapitio ya kimahakama ni kusimamia watunga sheria na watawala pale wanapozidisha matumizi ya mamlaka yao yaliyoainishwa kwa mujibu wa sheria zilizotungwa na Bunge.

Walisema madai ya mrufani ni ya kunyimwa nakala ya hati ya mashitaka na kutokupewa fursa ya kutafuta wakili, madai ambayo yangeweza kushughulikiwa na sheria za kawaida hivyo Jaji Mgetta alikuwa sahihi kutupa pingamizi la Mbowe.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories

Popular
Swahili News Editor

MGAO WA MAJI WAWATESA WAZANZIBARI

Wananchi wengi hasa katika maeneo ya Mjini Unguja, wanalalamikia ukosefu wa maji safi na salama huku Mamlaka ya Maji Zanzibar ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ujuzi na wataalam katika masuala ya uandisi wa Maji na fani nyengine.Continue Reading