Same. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua mradi mkubwa wa maji Same-Mwanga-Korogwe Machi 9, 2025 utakaogharimu zaidi ya Sh300 bilioni.
Mradi huo ambao utanufaisha wananchi zaidi ya 300 katika Wilaya za Same na Mwanga, mkoani Kilimanjaro utasaidia kupunguza changamoto ya maji kwa wananchi wanaoishi ukanda wa tambarare katika wilaya hizo.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2025 wakuu wa wilaya za Same na Mwanga, wamesema mradi huo utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya hizo kwa kuwa wametaabika kwa muda mrefu.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amesema wananchi wanasubiri kwa hamu ujio wa Rais kwa kuwa wameteseka kwa muda mrefu na changamoto ya maji.
“Wananchi wa wilaya ya Same, wanayo furaha kubwa sana, kumlaki Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anakuja kututembelea na kuzindua mradi wa maji Machi 9, mwaka huu,”amasema DC Kasilda
“Shida ya maji Same ilikuwa kubwa sana, wananchi walikuwa wakitembea kilomita tano kutafuta maji na hii ilisababisha baadhi ya ndoa kusambaratika, kwa sababu unakuta mwanamke anaamka usiku wa manane na kumuacha mwanaume ndani,”amesema DC Kasilda
Amesema zaidi ya wananchi 150,000 kutoka Njoro, Same mjini, Stesheni na Kisima ndio watakaonufaika na mradi huo kwa awamu ya kwanza.
Aidha, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwenda kumpokea Rais Samia Suluhu Hassan kwa tukio hilo muhimu.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mwanahamis Munkunda ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuondoa tatizo la maji wilayani humo.

“Mradi huu una historia ndefu kwa sababu umeanza kutekelezwa kwa muda mrefu zaidi ya miaka 19 sasa lakini awamu hii ya sita unatekelezwa na kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi wa Mwanga,”amesema DC Munkunda
Ameongeza, “kwa niaba ya Wanamwanga wenzangu tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu mkubwa wa maji, ambao unaenda kujibu changamoto zetu baada ya kukamilika kwa asilimia 100 na shughuli ya usambazaji wa maji unaendelea.”
Amesema wilaya hiyo ina wananchi zaidi ya 180 watanufaika na mradi huo hususan maeneo ya tambarare ya wilaya hiyo katika kata za Kirya, Same Mjini pamoja na maeneo mengine ya tambarare.
Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Same, Mwanga, Rashid Shaban amesema kwa sasa umekamilika kwa asilimia 100 na katika wilaya hizo mbili uhitaji wa maji kwa siku ni lita milioni sita.
“Mji wa Mwanga pamoja na Same, mahitaji yake ya maji sasa hivi ni wastani wa lita milioni sita kwa siku lakini kabla ya mradi huu upatikanaji wa maji ulikuwa wastani wa lita 3.7 milioni kwa siku, hivyo kulikuwa na mgao mkubwa sana, lakini sasa yatapatikana na kutosheleza mahitaji,”amesema Shaban
Mradi huo chanzo chake ni bwawa la nyumba ya Mungu na kimetengenezwa kidakio kinachochukua kutoka bwawani na kusambazwa kwenye mtambo wa kusafisha na kutibu maji wenye uwezo wa kusafisha lita 103 milioni kwa siku.
Source: mwananchi.co.tz