Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteua Baraka Leonard kuwa Katibu wa Bunge, kuchukua nafasi ya Nenelwa Mwihabi, aliyeteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Uteuzi huo umetangazwa leo Jumatatu, Septemba 16, 2024 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais-Ikulu ikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.
Taarifa hiyo ya uteuzi imeeleza, viongozi hao wawili wataapishwa Alhamisi ya Septemba 19, 2024, saa 9n alasiri, Ikulu ya Dar es Salaam.
Katika taarifa hiyo, haikuweka wazi Leonard ametoka wapi. Nenelwa anakwenda kuwa Jaji baada ya kuhudumu nafasi ya Katibu wa Bunge kwa takribani siku 1,220 sawa na miaka mitatu na miezi minne. Kabla ya uteuzi huo, Nenelwa alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge.
Uteuzi huo wa Nenelwa uliofanywa na Rais Samia, Mei 15, 2021 ulimfanya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.
Nenelwa aliteuliwa kuchukua nafasi ya Stephen Kagaigai ambaye wakati huo, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Kwa sasa Mkuu wa mkoa huo ni Nurdin Babu na Kagaigai ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Source: mwananchi.co.tz