Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na kuwaondoa mawaziri wawili.
Katika taarifa iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga leo Jumapili Julai 21, 2024 imesema ametengua uteuzi wa mawaziri wawili, Nape Nnauye (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) na January Makamba wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mbali na hao, Rais Samia ametengua uteuzi wa Stephen Byabato aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Pia, Rais Samia amemteua Ridhiwani Kikwete kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).
Awali, alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete anachukua nafasi ya Deogratius Ndejembi ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Rais amemteua Jerry Silaa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Pia, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla ya uteuzi huo, Balozi Kombo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, anachukua nafasi ya January Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Balozi Kombo anateuliwa kuwa Mbunge ikiwa ni saa chache tangu aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amuandikie Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson barua ya kujiuzulu ubunge.
Nafasi ya Balozi Mbarouk imechukuliwa na Cosato Chumi aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Endelea kufuatilia mitandao yetu
Source: mwananchi.co.tz