Zanzibar President Mwinyi warns against force in tax collection

Rais Mwinyi aonya matumizi ya nguvu ukusanyaji mapato

Unguja, Zanzibar:

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewaonya baadhi ya watendaji wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wanaotumia nguvu kubwa kukusanya kodi kwa wafanyabiashara akiwataka waache tabia hiyo.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 29, 2022 wakati wa sherehe za kilele cha shukrani na furaha kwa mlipa kodi mwaka 2021/22 kilichofanyika hoteli ya Golden Tulip Unguja sambamba na kutoa tuzo 41 kwa wafanyabiashara bora katika masuala ya kodi.

“Zipo taarifa baadhi ya watendaji wanatumia nguvu kubwa kukusanya kodi, nawataka waache mara moja. Wafanya biashara wanatakiwa kulipa kodi stahiki na wananchi kudai risiti kwa maendeleo ya taifa,” amesema

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuipongeza bodi hiyo na kueleza anavyoridhishwa na ukusanyaji wake wa mapato tofauti na ilivyokuwa kipindi kilichopita.

“Tusiwe tu wa kukosoa wakati wote, miezi kadhaa nilieleza wazi kutoridhishwa na mwenendo wa ZRB, lakini leo nasimama hadharani kusema kwamba ninaridhishwa sana na ukusanyaji wa kodi na hatua mnazozichukua, hongereni sana,” amesema Dk Mwinyi

Amesema kwa kipindi cha Julai hadi Novemba mwaka huu, bodi hiyo ilipangiwa kukusanya Sh238 bilioni, lakini imekusanya Sh236. 3 bilioni sawa na asilimia 99.1 ambalo ni ongezeko la asilimia 67.9 ikilinganishwa na makusanyo ya Sh141 bilioni kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Amesema mwelekeo wanaokwenda nao kama taifa ni mzuri ambao utawezesha kufikia malengo yaliyowekwa kwenye ilani ya CCM ya kukusanya Sh1.5 trilioni ifikapo mwaka 2025, “Nikupongeza kamishna (Juma Yussuf Mwenda) tokea ushike madaraka unafanya kazi vizuri.”

Mwenda alianza kazi ZRB Machi 2022 baada ya Rais Mwinyi kutengua uteuzi wa Salum Yussuf Ali.

Naye Kamishna Mwenda amesema mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na sbabu kadhaa ikiwa ni pamoja na kukua kwa uchumi, muamko wa wafanyabiashara kulipa kodi na usimamizi mzuri.

“Tumetoa elimu kwa walipa kodi 442 na kuzifikia biashara 456, lakini zaidi tumetoa msaada kwa kaya zisijojiweza 580 na vifaa tiba katika hospitali za Mnazimmoja na Abdallah Mzee Pemba,” amesema

Waziri wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Dk Saada Mkuya, amesema wamefanya maboresho kadhaa ikiwa ni pamoja nay a kiutendaji.

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year’s Most Read News Stories