Polisi Iringa yawashikilia wawili kwa kukutwa na magobore matano

Polisi Iringa yawashikilia wawili kwa kukutwa na magobore matano

Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa linawashikilia watu wawili kwa tuhuma ya kukutwa na bunduki za kienyeji aina ya gobore tano wanazodaiwa kuzitumia kufanyia ujangili.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Kamishna Msaidizi, Alfred Mbena amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni za  mara kwa mara zinazoendelea kufanyika mkoani humo.

Watuhumiwa hao  ambao ni Afya Kityega (47), mkazi wa Idodi na Fredy Lukosi  (25) mkazi wa Kijiji cha Ugwachanya, baada ya kupekuliwa walikutwa na chupa mbili za baruti, kamba ya manila, rissington za gobore  ambavyo ni vipande vya nondo na begi dogo jeusi.

Amesema watuhumiwa baada ya kuhojiwa wamekiri kuzitumia silaha hizo kutekeleza vitendo vya ujangili.

Wakati huohuo Jeshi hilo linamshikilia Thomas Ngoti (37) mjasiriamali na mkazi wa Mgera Kihwele mkoani Iringa akiwa na kofia, suruali moja, mkanda mmoja na begi ambazo ni sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania  (JWTZ ).

Amesema mtuhumiwa alikamatwa  eneo la makazi ya Mkuu wa Mkoa  wa Iringa, Kata ya Gangilonga  na baada ya kuhojiwa alidai  kuwa nguo hizo ni mali yake na amewahi kuwa askari  wa Jeshi hilo kabla ya kuacha kazi.

Katika tukio lingine, Polisi wanawashikilia watu watano wakiwa na vipande vinne vya meno ya tembo.

Amesema watuhumiwa wamekamatwa wakiwa kwenye mkakati wa kufanya biashara  hiyo ndani ya nyumba moja ya kulala wageni eneo la Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo.

Kamanda Mbena amesema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories