
Unguja. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman ametangaza nia ya kugombea urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu ujao endapo chama chake kitaridhia na kumpa jukumu hilo ili awasaidie Wazanzibari.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amebainisha hayo leo Januari mosi, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo huku akiuita mwaka 2025 ni “mwaka wa maamuzi.”
Katika mkutano huo uliofanyika Unguja, Zanzibar, Othman ameangazia miaka minne ya Serikali ya Rais Hussein Ali Mwinyi, akisema imetawaliwa na ufisadi wa fedha za umma hasa kwenye miradi ya maendeleo ambayo zabuni zake hazitangazwi popote kwa kushindanisha wazabuni.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Charles Hillary amesema hivi karibuni Rais Mwinyi atafanya mkutano na vyombo vya habari kuzungumzia tuhuma za ufisadi zinazotolewa na kiongozi huyo.
“Hayo anayoeleza ndiyo hayo kila siku anayaeleza na mheshimiwa Rais alishayajibu. Issue ya tender (zabuni), ukiweka tenda kwa hali yetu ilivyo, hii ni Januari, ule mchakato ukiisha itakuwa ni Septemba na sisi tunataka vitu viende kwa haraka. Lakini tusubiri, Rais ataongea,” amesema Hillary.
Atangaza nia ya urais
Othman amesema amejipima binafsi na kubaini ingawa yeye si mtimilifu wala mkamilifu, lakini anaamini hana kikwazo cha kuyatafuta yale aliyopungukiwa katika sifa za mtu sahihi wa kuinusuru Zanzibar.
“Napenda kwa heshima kubwa kutumia fursa hii kutangaza rasmi kwamba nimekusudia, Inshaallah itapofika wakati wa kuanza mchakato wa kutafuta wagombea katika chama changu, kwa kufuata taratibu ziliopo, kukiomba chama changu cha ACT Wazalendo kinibebeshe dhamana ya kukiwakilisha kwenye nafasi ya kuwania uongozi wa juu wa nchi yetu, ule wa Rais wa Zanzibar ili muda ukifika tuje tuwaombe Wazanzibari, watupe sisi ACT Wazalendo jukumu la kuwatoa hapa mahala walipo na tuwapeleke kwenye maendeleo, uhuru wa kweli na ustawi,” amesema Othman.
Amesema watachukua jukumu hilo kwa sababu wanajua nini kifanyike ili kuipata Zanzibar ya aina hiyo huku akisema imebaki miezi kumi kabla ya uchaguzi mkuu, hivyo ataendeleza wajibu wake wa kuwaelimisha wale ambao wamewatia hofu.
Ametolea mfano nchi za visiwa kama Mauritius, Singapore, Seychelles, Hong Kong, Taiwan na nyinginezo kwamba, zimefika si kwa kuongozwa na itikadi zilizojaa ufisadi, dhulma na ubaguzi bali, kwa sababu yalifanya kazi hiyo kwa manufaa ya watu katika mataifa hayo ya visiwa ikiwamo kujenga Serikali zenye ufanisi, uadilifu na uwajibikaji.
Amesema akiwa Mzanzibari na kiongozi wa chama chake, amejaribu kukiambia chama tawala kuwa sera zake za kizamani zilikuwa zikiwafukarisha Wazanzibari.
Othman amedai itikadi ya kuendesha Muungano kwa misingi wa siasa ya kuidhibiti Zanzibar, haiwezi kulisaidia Taifa hilo, hivyo ni wakati wa kuzingatia masilahi mapana ya kiuchumi na ustawi kwa wananchi na kila upande kuwa na fursa ya kuendelea.
Kiongozi huyo wa chama amesema imebakia miezi 10 kabla ya uchaguzi, hivyo ataendelea na wajibu wa kuwaelimisha wale ambao wamewatia wananchi hofu kwa miongo sita huku akiwaeleza mbadala wa kukabiliana na changamoto zilizopo.
“Tunaukaribisha mwaka huu mpya kwa lengo moja tu, ambalo ni kuinusuru Zanzibar kutoka mikononi mwa utawala uliojengwa katika misingi ya ufisadi uliopora matumaini ya kila kitu; ya kiuchumi na raia kutendewa haki. Sote ni mashahidi, Zanzibar imepitia katika misukosuko mingi,” amesema Othman.
Udhaifu wa SUK
Othman amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK) imekuwa ikisuasua kutokana na kukosekana kwa dhamira ya dhati ya kushirikiana na ACT Wazalendo.
Kiongozi huyo amedai kuwa, ACT Wazalendo hawashirikishwi kwenye baadhi ya mambo kama ilivyotarajiwa.
“Mkwamo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umesababishwa na kukosekana kwa dhamira. SUK ilipoanzishwa baada ya kurekebisha Katiba, ililenga ushirikiano wa vyama vinavyounda Serikali, lakini hilo wenzetu hawalitaki.
“Ilitakiwa kama mwenyekiti wa halmashauri ni wa CCM, basi makamu wake atoke ACT Wazalendo. Kama mwenyekiti wa kamati ya Baraza la Wawakilishi ni CCM, basi makamu wake atoke kwetu, haya yote hayafanyiki,” amesema Othman.
Source: mwananchi.co.tz