Mwakilishi afariki dunia akipatiwa matibabu India

Mwakilishi afariki dunia akipatiwa matibabu India

Unguja. Mwakilishi wa viti maalumu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Panya Ali Abdalla (60) amefariki dunia akipatiwa matibabu nchini India.

Akizungumza hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Utaratibu na Baraza la Wawakilishi), Hamza Hassan Juma amesema Serikali kwa kushirikiana na familia, inaendelea kuratibu mipango ya mazishi na kurudisha mwili wa marehemu nchini.

Mwakilishi Panya amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kabla ya kupelekwa India alianza kupatiwa matibabu katika hospitali tofauti nchini.

Kwa mujibu wa Hamza, Panya amefariki dunia usiku wa kuamkia Julai 25,2024   na kwamba mwili unatarajiwa kupokewa Julai 27, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar na kukabidhiwa kwa ndugu kisha kuzikwa siku hiyohiyo.

“Kwa upande wetu Serikali tumekamilisha mipango ya kusafirisha mwili na watu ambao walimuuguza. Tunatarajia mwili huo utapokewa Jumamosi mchana na watakabidhiwa familia yake, kisha kwenda moja kwa moja kuzikwa,” amesema Hamza.

Baadhi ya wawakilishi wamesema wamepoteza mtu muhimu aliyekuwa na mchango mkubwa siyo tu katika Baraza la Wawakilishi bali Serikali kwa ujumla.

Mwakilishi wa kuteuliwa, Juma Ali Khatib amesema wamepokea taarifa za msiba huo kwa mshutuko kwani alikuwa mahiri na aliyesaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mipango ya Serikali.

“Ni msiba mzito, tumempoteza mtu muhimu ndani ya baraza, mchango wake utakumbukwa ndani na nje ya baraza na serikalini,” amesema.

Amesema wajumbe wa baraza walikuwa Arusha kwa shughuli za michezo lakini baada ya taarifa za msiba huo imewalazimu kuzisitisha.

“Wajumbe wote tulikuwa Arusha kwenye mafunzo maalumu na michezo lakini baada ya kupata taarifa hizi leo Julai 26 tunarudi Zanzibar kwa ajili ya kushiriki shughuli za kumuaga mwenzetu,” amesema.

Katika Baraza la Wawakilishi amekuwa mwenyekiti wa kamati mbalimbali ikiwemo ya maadili.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya Baraza la Wawakilishi, Panya aliyezaliwa Februari 5, 1964 alikuwa mjumbe wa baraza hilo tangu mwaka 2010.

Kabla ya kuwa mwakilishi alishika nyadhifa mbalimbali za Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo mwenyekiti wa wazazi Wilaya ya Kaskazini B, Unguja mwaka 2003 hadi 2012.

Pia alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa mwaka 2003 hadi 2012, mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mwaka 2012/17 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) mwaka 2012/17.

Ni mwakilishi wa pili kufariki dunia tangu uchaguzi mkuu umalizike mwaka 2020 akitanguliwa na mwakilishi wa Mtambwe, Kisiwani Pemba kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Habib Ali Mohammed aliyefariki dunia Machi 3, 2023 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Saifee, jijini Dar es Salaam.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories