Mwabukusi aenguliwa kugombea urais TLS

Mwabukusi aenguliwa kugombea urais TLS

Dar es Salaam. Ikiwa imebaki siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Kamati ya rufaa za uchaguzi ya chama hicho, imemuengua wakili Boniface Mwabukusi kugombea urais, ikisema ana doa la kimaadili kinyume na kanuni za uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu, Mwabukusi alikuwa miongoni mwa wagombea sita waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TLS kugombea nafasi hiyo.

Wengine ni pamoja na Ibrahim bendera (Ilala), Emmanuel Muga, (Ilala), Revocatus Kuuli (Mzizima), Paul Kaunda (Kanda ya Magharibu) na Sweetbert Nkuba (Kinondoni).

Mwabukusi aliyejipatia sifa kwa kupinga mkataba wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari kati ya Serikali ya Dubai na ya Tanzania, alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali akimlalamikia kwa kukiuka maadili ya uwakili.

Baada ya shauri lake kusikilizwa, hatimaye alikutwa na hatia na kupewa onyo Mei mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 5, 2024, Mwabukusi amesema rufaa yake ilisikilizwa kwa njia ya mtadao na kuambiwa na kamati hiyo kuwa amepoteza sifa ya kugombea.

“Nimejulishwa jioni hii, kwa sababu rufaa imeendeshwa kwa mtandao kwamba inabidi nienguliwe kwa masilahi ya Taifa,” amesema Mwabukusi.

Hata hivyo, amesema hajaridhishwa na uamuzi huo na ataeleza hatua zaidi atakazochukua.

Mwananchi imezungumza na Katibu wa Kamati ya uchaguzi ya TLS, Nelson Frank na kumuuliza sababu ya wakili huyo kuenguliwa.

“Tangazo la chama cha wanasheria GN 598 la mwaka 2022 kanuni ya 13c, zinataka miongoni mwa mambo mengine, mgombea anayegombea nafasi ya urais asiwe na doa lolote la kimaadili.

“Kuna hukumu ambayo ipo ambayo Mwabukusui alitiwa hatiani na haijawahi kutenguliwa na chombo chochote kwa hiyo bado ipo. Kwa hiyo Kamati ya Rufaa ya uchaguzi ya TS ikaona kwamba ana doa la kimaadili kwa hiyuo hajakidhi vigezo vya kugombea urais,” amesema.

Alipoulizwa sababu ya Kamati ya Uchaguzi kumpitisha wakili huyo kama alikuwa na maadili, Frank amesema uchaguzi ni mchakato.

“TLS huwa kuna Kamati ya Uchaguzi halafu kuna Kamati ya Rufaa ya uchaguzi, hivyo ni vyombo viwili tofauti. Awali kamati ya uchaguzi katika mchakato ule, wao waliona kwa namna moja au nyingine amekidhi vigezo wakamwona anafaa kugombea urais, lakini kuna chombo cha juu ya ile kamati, kwa hiyo ilipofika kwenye ngazi ya juu zaidi ambayo ni kamati ya rufaa za uchaguzi ya TLS, ikaona kwamba kwa mantiki kwamba kuna hukumu ambayo ipo na alitiwa hatiani kwa sababu ya maadili wakaona ana doa,” amesema.

Bila kumtaja aliyekata rufaa, Frank amesema mpaka kamati imefikia hapo, kuna watu ambao hawakuridhika wamekata rufaa.

Amesema rufaa hizo ni mchakato wa ndani wa chama na sasa hatua inayofuata ni kampeni. “Kama mtu hajaridhika na uamuzi ndani ya chama basi atachukua hatua nyingine nje ya chama.”

Alipoulizwa sababu ya rufaa yake kuamuliwa siku ya mwisho, amesema huo ni mchakato ambao kama mtu hataridhishwa na mchakato wa chini, Kamati ya rufaa hukata rufaa na ndio yenye uamuzi wa mwisho.

“Kanuni zinaeleza kuwa, msiende kwenye hatua nyingine kabla ya kumaliza na kutoa uamuzi kwenye hatua ya nyuma. Kwa mfano, kama kulikuwa na rufaa, ni lazima zisikilizwe na ziamuliwe kabla ya kwenda kwenye kampeni.

“Ndio maana umeona Juni 24, 2024 Kamati ya Uchaguzi ilisema hawa wanafaa kugombea kwenye chama, lakini kuna wale ambao hawakuridhishwa, wakakata rufaa kwenye kamati ya rufaa, kwa hiyo leo ilikuwa ni lazima maamuzi yatolewe, kwa mfano mpaka leo kulikuwa na rufaa saba imebidi zisikilizwe, kwa sababu ndio sheria inavyoeleza kwamba uamuzi utoke kabla ya kampeni,” amesema.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories