Kibondo. Mashirika ya kuhudumia wakimbizi yaliyopo mkoani Kigoma yametakiwa kutokuwa kikwazo kwenye makubaliano yaliyowekwa na serikali za Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), ya kuhamasisha wakimbizi kujiandikisha na kurejea nchini mwao kwa hiari.
Hayo yamebainishwa Juni 20, 2024 wilayani Kibindo na Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi nchini, Sudi Mwakibasi wakati wa maadhimisho ya siku ya mkimbizi duniani yaliyofanyika katika kambi ya wakimbizi ya Nduta.
Amesema Serikali ya Tanzania inasimamia makubaliano hayo na hivyo kila mmoja anapaswa kutekeleza badala ya kuwa kikwazo.
“Kinachofanyika ni kupambania maslahi binafsi na taasisi , wakati Serikali inapambania maslahi ya watu wake na ya Warundi. Sasa haiwezekani Serikali kuumiza wakimbizi kwa sababu ya ajira, naombeni tuwasaidia wakimbizi kurejea nyumbani ili watumie fursa ya kwenda kujenga nchi yao,” amesema Mwakibasi.
Amesema ni vema viongozi wa kambi zote mbili na vyombo vya ulinzi na salama kuhakikisha vijana wa kiume kutotoka ndani ya kambi bila kibali maalumu kwani ni kinyume cha sheria na taratibu zilizopo kwani Serikali haijui wanaenda wapi na kufanya nini.
Mwakilishi wa Shirika la UNHCR nchini Tanzania, Mahoua Parums amesema kama hali inaruhusu wakimbizi hao anapenda kuwahamasisha kuangalia suluhisho la kudumu la urejeaji kwa hiari nchini mwao.
“Ndio tuna masuluhisho mengine lakini nyumbani ni nyumbani, hivyo ni vema kama hali inaruhusu waweze kurejea nyumbani kwa hiari na kwenda kuijenga nchi yao, jambo ambalo ni zuri na linaleta faraja,” amesema Parums.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Aggrey Magwaza amesema hadi sasa wakimbizi ambao wamesharejea nchini kwao kwa hiari ni 170,000 huku wakimbizi waliopo hadi sasa kwa kambi ya Nduta na Nyarugusu wakifikia 246,000.
Nao baadhi ya wakimbizi wa kambi ya Nduta, wamesema wanaendelea kujiandikisha ili waweze kurejea nchini kwao kwa hiari, na kwamba hakuna mwananchi anayeweza kuikimbia nchi yake bila sababu na kwenda kuwa mkimbizi kwenye nchi nyingine.
Mkimbizi Donatha Nibiza amesema Serikali ya Tanzania inatekeleza shughuli ya kuwarudisha nyumbani kwa hiari wakimbizi nchini kwao, lakini kila mkimbizi amekimbia kwa sababu zake maalumu, hivyo ni muhimu kuchukua hatua ya kuwasikiliza kwanza na kujua sababu zipi hasa zilizowafanya waweze kukimbia nchini kwao.
Iveti Nibaruza amesema yeye yupo tayari kurejea nchini kwake kwa hiari na kwamba muda wa promosheni uliotolewa na pande zote, anauunga mkono na atatumia kipindi hicho kwenda nchini kwake kuijenga nchi yake.
Source: mwananchi.co.tz