Mufindi. Siku chache baada ya Serikali kutoa maagizo ya kukabiliana na mauaji ya watu wenye ualbino nchini Tanzania, Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Godfrey Mnzava amekemea vitendo hivyo, huku akiitaka jamii kushirikiana kutokomeza vitendo hivyo.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa bungeni jijini Dodoma, alitaka kuendelea ubainishaji na usajili wa watu wenye ualbino kuanzia ngazi za kijiji na mtaa, ili kuwalinda watu hao.
Hatua hiyo imekuja kutokana na mauaji ya mtoto Asimwe Novath (2) mwenye ualbino, aliyeporwa mikononi mwa mama yake Mei 30, 2024 na watu wasiojulikana nyumbani kwao Kijiji cha Mulamula, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera na siku 19 baadaye ulipatikana mwili wake.
Akizungumza leo Jumapili Juni 23, 2024 akiwa katika Halmashauri ya Mji Mafinga mkoani Iringa, Mnzava amehimiza ushirikiano na vyombo vya usalama, viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, waganga wa kienyeji, walezi, wazazi, na wananchi, ili kukomesha mauaji hayo.
Mkimbiza Mwenge huyo alikuwa akikagua shughuli za kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambao ni pamoja na wenye changamoto ya usonji na ulemavu wa viungo katika Shule ya Msingi Mchanganyiko Makalala iliyopo katika halmashauri hiyo.
Amesema ni muhimu kamati za ulinzi na usalama za wilaya zikatambua idadi ya watoto wenye ualbino na maeneo wanayoishi kupitia maofisa ustawi wa jamii, ili walindwe na madhira ya ukatili wanayokumbana nayo, huku akihimiza jamii yote kuungana kukomesha matukio ya aina hiyo.
“Siku chache hizi limeibuka wimbi kwa kweli sio utamaduni wetu Watanzania na wala sio mambo yetu. Mtu kumuwinda mwenzie ni vitendo vya kinyama. Hili lipo kwenu ninyi wakuu wa wilaya na kamati zenu za ulinzi kusimamia na kuhakikisha watoto hao wanaendelea kubaki salama,” amesema Mnzava.
Amesema watoto hao wanapaswa kupewa haki ya kulindwa wakati wote, ili waendelee kuwa salama na waishi kwa amani na utulivu katika Taifa lao.
Awali, akizungumza wakati wa kupokea Mwenge katika viwanja vya Shule ya Msingi Wambi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Fidelica Myovella amesema utakimbizwa umbali wa kilomita 49.6 na utapitia miradi tisa yenye thamani ya zaidi ya Sh2 bilioni.
Mkurugenzi huyo amesema wakazi wa mji huo wanajihusisha na shughuli za kilimo, ufugaji, biashara na ajira kwa watumishi wanaohudumu katika sekta za umma na binafsi.
Myovella ametaja baadhi ya miradi ambayo imezinduliwa na kupitiwa na Mwenge huo kuwa ni Shule ya Msingi Makalala kwa ajili ya kukagua shughuli za kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu, uzinduzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Mkombwe na Klabu ya Wapinga Rushwa.
Miradi mingine ni kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.25, kukagua shughuli za vijana, kukagua uendelevu wa mradi wa maji uliozinduliwa mwaka 2023, uzinduzi wa mradi wa kituo cha mafuta NFS, pamoja na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa wodi daraja la kwanza katika Hospitali ya Mji Mafinga.
Source: mwananchi.co.tz