MGAO WA MAJI WAWATESA WAZANZIBARI

MGAO WA MAJI WAWATESA WAZANZIBARI

SWAHILI News Exclusive: Na Mwandishi Wetu

Wananchi wengi hasa katika maeneo ya Mjini Unguja, wanalalamikia ukosefu wa maji safi na salama huku Mamlaka ya Maji Zanzibar ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ujuzi na wataalam katika masuala ya uandisi wa Maji na fani nyengine.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mgao wa maji katika Mitaa mbalimbali ya Unguja huku baadhi ya Mitaa ikikosa kabisa huduma hiyo na kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi ambao wanalazimika ama kununua maji kwenye magari na wengine kwenye visima vya watu binafsi.

“Kama unavyoona watu wanahangaika na madumu ya maji, hapa mtaani petu hatupati kabisa maji ya ZAWA, hatuelewi tatizo hili litakwisha lakini tunateseka na maji” Alilalamika Ali Yussuf Mkaazi wa Sogea Mjini Unguja.

Maeneo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni urithi wa Kimataifa unaotambuliwa na Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na kwenye hoteli kadhaa za Kitali, huduma ya maji safi na salama ni ya kubahatisha.

“Hapa Hotelini sisi tunanunua maji kila siku, hatupati kabisa maji ya ZAWA… kwa kweli ni mzigo mzito kwetu gharama zimekuwa kubwa a uendeshaji” Alisema Meneja mmoja wa Hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano ambae hakupenda kutaja jina lake.

Habari zaidi kutoka ZAWA zinasema kwamba wakati wananchi wakikosa huduma ya maji na wengine wakipata maji kwa mgao wa muda mrefu, kumekuwa na kutoelewana miongoni mwa wafanyakazi na uongozi wakiulalamikia uongozi wa Taasisi hiyo kutojali maslahi yao, uwezo wao kufikia ukingoni pamoja na masuala ya itikadi za kisiasa.

Inadaiwa kwamba makundi yaliyopo katika ZAWA ni miongoni mwa sababu zinazozorotesha utendaji kazi pamoja na ukosefu wa weledi katika usimamizi wa masuala ya maji. “Hapa kuna makundi, hatuko kitu kimoja, mkurugenzi ana kikundi chake fulani ndicho anachokiamini” Alisikika Fundi Mmoja akisema.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Nishati na Madini, Mwanajuma Majid Abdullah amewaomba wananchi kuendelea kustahamili wakati Serikali ikishughulikia tatizo la ukosefu wa maji katika maeneo yao mbalimbali kupitia miradi ya maji inayotekelezwa na ZAWA.

“Nafahumu kwamba tatizo la maji halistahamiliki, lakini nawaomba wananchi kuendelea kupokea huduma ya maji kwa mgao kwani sio muda mrefu tatizo la maji litamalizika Zanzibar” Naibu Katibu Mkuu Mwanajuma Majid alieleza Kamati ya Ardhi, Mawasiliano na Nishati ya Baraza la Wawakilishi.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema tatizo la maji Zanzibar limetokana na uwepo wa visima vichache ambavyo vinatumika pamoja na uchakavu wa miondombinu ya maji.

Mkurugunzi Mkuu wa ZAWA Mhandisi Dkt Salha Mohammed Kassim alitaja ukosefu wa wataalam ni miongoni mwa changamoto kubwa inayoikabili Mamkala hiyo kwa sasa na kuiomba Serikali kutoa umuhimu katika kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi kwani hata ikikamilika kwa miradi ya maji bado kutakuwa na changamoto kwa kukosekana kwa wataalam.

Haikuweza kufahamika mara moja ni kiasi gani cha fedha kilichotumika kutoka katika fedha za Uviko 19 zilizotolewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuipatia SMZ pamoja na fedha za Exim Bank ya India ambapo fedha hizo zimepangwa kutumika katika ujenzi wa matangi, ulazaji wa mabomba ,uchimbaji wa visima.

MWISHO.

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year’s Most Read News Stories