Dar es Salaam. Wakati ripoti ya Takwimu za Msingi Tanzania inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ikionyesha ongezeko la mauzo ya gesi asilia kwa asilimia 75, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetaja mikakati ya kuongeza matumizi.
Ripoti hiyo ya mwaka 2023 iliyotolewa Julai 2024 inaonyesha kuwa mauzo yameongezeka katika vitalu vya Mnazi Bay mkoani Mtwara na Songosongo mkoani Lindi kutoka Sh192.4 bilioni mwaka 2022 hadi Sh336.4 bilioni mwaka 2023 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 75.
Kwa mujibu wa TPDC, gesi ya Mnazi Bay na Songosongo ndiyo inatumika kuzalisha umeme, kuendeshea magari, matumizi ya nyumbani na viwandani.
TPDC yaeleza mikakati
Akizungumza leo Jumatano Agosti 21, 2024 baada ya kutembelea na kukagua kituo mama cha kujaza gesi asilia kilichopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPDC, Balozi Ombeni Sefue amesema shirika hilo ni mdau katika kutekeleza mikakati ya kitaifa na kimataifa ya kuongeza matumizi ya nishati safi.
“Vipaumbele vyetu ni kuhakikisha usafiri, umeme tunaoutumia nyumbani na uzalishaji viwandani kwa kadri inavyowezekana tutumie gesi asilia ambayo ni safi kuliko nishati nyingine,” amesema.
Amesema TPDC inajenga kituo kikuu cha kujaza gesi kwenye magari na kusaidia usambazaji wa nishati hiyo katika Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani ambayo itapelekwa kwa kutumia magari maalumu.
Amedokeza kuwa ujenzi wa kituo hicho ni hatua muhimu kuongeza upatikanaji wa matumizi ya gesi asilia.
“Kituo kitakamilika mwishoni mwa mwaka huu na sasa ujenzi umefikia asilimia 33.5. Uundaji wa mitambo itakayokuja kusimikwa unaendelea kufanyika nchini China na umefikia asilimia 76,” amesema.
Mbali na mipango hiyo, Balozi Sefue amesema TPDC inaleta vituo vingine sita vinavyohamishika vyenye uwezo wa kujaza gesi magari mawili kwa wakati mmoja.
Vituo hivyo vitakuwa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, Dodoma, Manispaa ya Morogoro, Dodoma na tayari kampuni binafsi 40 zimeruhusiwa kujenga vituo vya kushindilia gesi kwenye magari katika maeneo mbalimbali nchini na zipo kwenye hatua za utekelezaji.
“Niwaombe Watanzania kuendelea kuweka mifumo ya gesi kwenye magari yao na kununua magari ambayo tayari yameundwa kwa mifumo ya gesi kwa kuwa mwarobaini wa kero ya upatikanaji wa vituo unakwenda kuisha,”amesema.
Balozi Sefue amesema miundombinu inayojengwa na hamasa inayowekwa kwa wananchi kutumia gesi asilia, ongezeko la matumizi ya gesi nchini yatakuwa makubwa.
Kuhusu kuongeza utafutaji wa gesi, balozi huyo amesema kwa sasa wanatekeleza miradi ya utafutaji na uzalishaji na uendelezaji wa gesi asilia na mafuta.
“Kitalu cha Ruvuma eneo la Ntorya, TPDC inashirikiana na Kampuni ya ARA Petroleum ya Oman kuendeleza gesi asilia iliyogunduliwa, lengo tuanze uzalishaji wa gesi asilia katika robo ya pili ya mwaka 2025,” amesema.
Akizungumza katika ziara hiyo, meneja wa gesi iliyoshindiliwa TPDC, Aristides Kato amesema ujenzi wa kituo kikuu cha kujaza gesi kwenye magari, ununuzi wa magari tisa na ujenzi wa vituo viwili vya kujaza gesi kwenye magari eneo la Muhimbili na Kibaha vitagharimu Sh14.55 bilioni.
Kato amesema kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea gesi futi za ujazo milioni tatu kwa siku, huku zaidi ya magari 1,000 yakihudumiwa kujazwa gesi kwa siku.
“Kupitia mradi huu tutajenga karakana ya kubadilisha gesi kwenye magari na hii itakuwa chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na tutakuwa na umeme wa gesi pamoja na umeme wa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania),” amesema.
Kwa TPDC, hadi sasa kuna magari 2,000, nyumba 1,511, taasisi 10 na viwanda 56 zinatumia gesi asilia kama nishati, gridi ya Taifa zaidi ya asilimia 50 ya nishati yake ikitokana na gesi asilia.
Source: mwananchi.co.tz