Marekebisho sheria ya LST yatoa nafuu kwa wahitimu wa sheria

Marekebisho sheria ya LST yatoa nafuu kwa wahitimu wa sheria

Dar es Salaam. Haitakuwa lazima tena kwa kila mhitimu wa Shahada ya Sheria kupita Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), iwapo hana mpango wa kufanya kazi za uanasheria katika utumishi wa umma.

Matarajio ya kutokea hilo yatafikiwa baada ya marekebisho ya sheria ya kuanzishwa kwa LST, ambayo kwa sasa inalazimu yeyote anayetaka kufanya kazi za uanasheria katika utumishi wa umma, afaulu masomo ya uanasheria kwa vitendo.

Tayari wabunge wamepitisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya LST ya mwaka 2024.

Sambamba na hilo, marekebisho mengine yaliyopitishwa ndani ya muswada huo ni kuongeza wigo kwa LST kutoa mafunzo ya kozi nyingine maalumu za mafunzo ya sheria.

Hatua ya marekebisho hayo inatajwa na wanasheria kuwa itapunguza wimbi la wanaofanya kazi ya uwakili kwa sababu wamepitia misingi ya utendaji wa taaluma hiyo LST kwa sharti la kisheria lililopo.

Muswada huo ulipitishwa bungeni jijini Dodoma Agosti 27, 2024 baada ya kuwasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.

Profesa Kabudi alisema shabaha ya marebisho hayo ni kutatua changamoto zilizobainika katika utekelezaji wa masharti ya sheria.

Marekebisho hayo kwa mujibu wa Profesa Kabudi, yatahusisha kifungu cha 5 ili kuongeza wigo kwa LST kutoa mafunzo ya kozi nyingine maalumu za mafunzo ya sheria.

Pia Ibara ya 7 inarekebishwa kuondoa sharti la kila muhitimu wa shahada ya sheria kulazimika kupitia na kufaulu masomo ya sheria kwa vitendo, hata kama hakusudii kufanya kazi za uanasheria katika utumishi wa umma.

Nini maana yake

Akizungumzia hilo, Wakili wa Kujitegemea, Ipilinga Panya amesema sharti la kila anayehitimu shahada ya sheria kulazimika kusomea uwakili, ndiyo lililosababisha uwepo wa watu wanaojifanya mawakili ilhali hawastahili.

“Kwa sababu mtu anahitimu shahada anakwenda LST kwa namna yoyote ile anapata kujua undani wa utendaji wa wakili, naye anajinasibu kuwa wakili hata kama haikuwa nia yake. Hapa ndipo wanapotokea watu wasio waadilifu,” amesema.

Kuondolewa kwa sharti hilo, Panya ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amesema kutasaidia kupunguza mawakili wasiostahili.

Hata hivyo, amesema TLS itapitia muswada huo wote na kama itaonekana inafaa rais wake, Boniface Mwabukusi atauzungumzia.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Taasisi, Mipango, Fedha na Utawala wa LST, Profesa Ambrose Kessy amesema kinachomaanishwa ni kuondoa ulazima wa mtu anayesoma shahada ya sheria kupitia LST kama hataki kufanya kazi za sheria.

“Lakini wote wanaotaka kufanya kazi za sheria kama wanasheria serikalini au kwenye vitengo vya sheria serikalini, mawakili binafsi, mahakimu, lazima waende LST. Kimsingi ni wote wanaotaka kuitwa wanasheria,” amesema.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories