Dar es Salaam. Saratani ya uume, ugonjwa ambao haujulikani sana kwa wengi nchini Tanzania, unaathiri maisha ya wanaume kwa kiwango kikubwa.
Wakati mwingine, matibabu pekee yanayopatikana ni kukatwa uume, hali inayobadilisha kabisa maisha ya mgonjwa.
Ingawa ni nadra na mara nyingi haijadiliwi wazi, saratani hii inachukua asilimia 27 ya saratani zote kwa wanaume nchini na inahitaji uelewa na tahadhari zaidi.
Dk Crispin Kahesa, mkurugenzi wa Idara ya Kinga katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), anasisitiza umuhimu wa elimu na kuzingatia mtindo bora wa maisha, ili kupunguza hatari ya kupata ugonjwa huu hatari.
Mmoja wa waathirika wa saratani hiyo, anaeleza hisia zake alipofikia hatua ya mwisho na matibabu, ambayo ilikuwa ni kukatwa uume, akisema alihisi maisha yake yamebadilika kabisa, sawa na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili.
Huyo ni mmoja kati ya wagonjwa wengi wa saratani hiyo, ambayo inakadiriwa kati ya wagonjwa 138 wanaogundulika kuwa na saratani ya uume, asilimia zaidi ya 20 hufariki.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Crispin Kahesa anasema saratani ya uume inachukua asilimia 27 kati ya saratani zote na ni tofauti na ya tezi dume.
“Saratani ya tezi dume ni ile inayoathiri tezi la mwanaume, sio saratani ya uume,” anasema Dk Kahesa akibainisha kuwa kama ilivyo huko duniani, hapa nchini pia matibabu pekee ni mgonjwa kukatwa uume.
Mwaka 2022, Jarida la JMIR la Afya ya Umma la Toronto nchini Canada, lilichapisha matokeo ya uchambuzi kutoka nchi 43, ulioonyesha kuwepo ongezeko la wagonjwa wa saratani ya uume.
Kati ya mwaka 2008 na 2012 iligunduliwa kuwa nchini Uganda kati ya wanaume 100,000, waliokuwa wanaugua saratani hiyo ni 2.2. Brazil ilifuatia ikiwa na 2.1 na Thailand 1.4 wakati Kuwait ikitajwa kuwa na na idadi ndogo ya wagonjwa ambako 0.1 walikuwa wanaugua saratani hiyo.
Utafiti kutoka Chuo Kikuu cha China ulionyesha katika nchi zinazoendelea kuna wagonjwa wengi wa aina hii ya saratani.
Utafiti huo ulibainisha ongezeko kubwa pia katika nchi za Ulaya miaka ya karibuni.
Ripoti hiyo inaonyesha Uingereza imeshuhudia ongezeko la saratani ya uume ambapo mwanamme mmoja kati ya 100,000 anaugua ugonjwa huo.
Ujerumani ilishuhudia ongezeko la asilimia 50 ya maambukizi kati ya mwaka 1961 na 2012 na idadi hiyo inaongezeka na ikiwa itaendelea, ifikapo 2050 kutakuwa na idadi ya wagonjwa zaidi ya asilimia 70 ikilinganishwa na idadi ya sasa.
Hali ilivyo nchini
Dk Kahesa anasema, katika miaka mitano takwimu zinaonyesha wagonjwa waliopo ni 283, hiyo ikijumuisha wapya na waliopoteza maisha.
Jinsi ya kuepuka
Dk Kahesa anasema wanaume wanaweza kujiepusha na hatari ya kupata maambukizi ya saratani hii kwa kufuata mtindo bora wa maisha.
“Kwanza ni kufanya tendo la ndoa salama na kujikinga kupata maambukizi ya kirusi cha human papilloma (HPV) ambacho ni moja ya sababu kubwa ya saratani ya uume,” anasema Dk Kahesa.
Anasema, jambo jingine ambalo linaweza kuwaepusha wanaume na hatari ya kupata saratani hiyo ni kuzingatia usafi binafsi.
“Ni muhimu kwa wanaume wa rika zote kuosha uume kwa sabuni na maji kila siku na baada ya tendo la ndoa,” anasema Dk Kahesa na kuendelea.
“Pia wanapaswa kujiepusha na sababu ambazo zinaweza kushusha kinga zao za mwili, kama matumizi ya tumbaku na kuhakikisha wanafanya tohara.”
Anasema waathirika wa saratani hiyo ni wanaume na moja ya kisababishi pia ni endapo watakuwa na michubuko katika sehemu ya uume ambayo inatokana na maambukizi ya HPV.
“Kirusi hiki pia kinaathiri kina mama kwenye saratani ya mlango wa kizazi na kinaambukizwa kwa njia ya kujamiiana.”
“Suala la usafi vilevile linachangia mtu kupata maambukizi. Unapokuwa na usafi duni kuna hatari kwenye uume kuweka ganda la uchafu ambalo linaongeza hatari kama ya kupata michubuko na maambukizi haya,” anasema.
Anasema kwa ambao hawajafanyiwa tohara, wanakuwa na ngozi ya juu ya uume ambayo haiwezi kurudi vizuri wanapokutana kwenye tendo la ndoa, hivyo husababisha sana michubuko na kuongeza hatari ya kupata maambukizi ya saratani ya uume.
Dalili za saratani ya uume
Kwa mujibu wa Kahesa, katika hatua za awali kama ilivyo kwa saratani nyingine, dalili ya saratani ya uume haiwezi kuonekana.
Hata hivyo, anasema kadri siku zinavyozidi kwenda, ndipo waathirika walio wengi huanza kuona mabadiliko ya ngozi katika kichwa cha uume.
“Wakati mwingine huwa chekundu au hubadilika rangi kutegemea na hali ya michubuko, japo kwa wengine wanaweza kuona ganda la juu la ngozi ya uume kama limepata ukoko na kutengeneza kitu kama baka, mfano wa punye,” anasema.
Anasema, punye hilo halitoki na tatizo likiendelea huleta uvimbe kwenye uume na kwa walio wengi uvimbe unakuwa kidonda ambacho hutoa damu na kuambata na maumivu.
“Katika uchunguzi huwa tunagundua pia baadhi ya tezi ambazo ziko ukingoni mwa miguu zinatengeneza mitoki,” anasema.
Matibabu yake
Utafiti wa China Yat-Sen University, Guangzhou (SYSU) unaeleza kuna uwezekano mkubwa wa kupona kupitia matibabu kama vile ya upasuaji na tiba za mionzi.
Lakini ikiwa haitatibiwa, inaweza kusababisha kukatwa kwa sehemu au uume wote kwa ujumla na labda hata viungo vingine vya siri kama vile korodani. Na kwa wagonjwa wengine suluhisho pekee huwa ni kukatwa kwa uume.
Dk Kahesa anasema, kama ilivyo huko duniani ndivyo ilivyo hapa nchini, kuwa matibabu yatategemea na tatizo.
“Matibabu ya saratani ya uume yanafanyika kwa upasuaji na mionzi au mchanganyiko wa dawa za kemikali.”
Anasema, kwenye upasuaji ndipo baadhi hukatwa uume kutegemea na mgonjwa ameathirika kiasi gani.
“Kama kiungo chote kimeathirika inabidi kiondolewe,” anasema Dk Kahesa akifafanua kuwa mgonjwa aliyekatwa uume anavyoweza kujisaidia haja ndogo.
Anasema, kutoa haja ndogo haiusiani na kuwa na uume, kwani haja ndogo ina pitia kwenye njia ya mkojo, hivyo mgonjwa aliyefikia hatua ya kukatwa uume, tundu la kupitisha haja ndogo linabaki.
“Haja ndogo utaendelea kupata kama kawaida kupitia njia ya mkojo ni kama mama akiondolewa mlango wa kizazi, haja ndogo ataendelea kupata kama kawaida,” anasema Dk Kahesa.
Anachoeleza Dk Kahesa kinafafanuliwa na Thiago Camelo Mourão, kutoka idara ya tiba ya njia ya mkojo ya Kituo cha Saratani cha Sao Paulo, Brazil katika andiko lake, kuwa ikiwa kuna kukatwa kwa uume, mkojo unaendelea kutoka.
“Katika kisa cha kukatwa kabisa, njia ya mkono inaweza kuhamishwa kwa sehemu ya mwili, kati ya scrotum (mfuko unaobeba mbegu za kiume) na njia ya haja kubwa, na kusababisha mgonjwa kukojoa akiwa ameketi chooni.” anasema Thiago.
Tofauti ya saratani ya
uume na tezi dume
Saratani hi ya uume, kama zilivyo nyingine, ni ukuaji wa seli usio wa kawaida na usiodhibitika ndani ya uume. Kwa asilimia kubwa huanza kwenye seli za ngozi ya uume kisha kuingia ndani.
Wakati saratani ya tezi dume ni tatizo kama hilo kwenye tezi dume ambayo inakuwa imepata ugonjwa wa saratani.
Na hii hutokea pale ambapo chembechembe hai za tezi huasi na kuanza kujigawanya bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili, chembechembe asi hizi mwishowe hutengeneza vivimbe hatari ndani ya tezi dume na hatimaye husambaa mwilini.
Source: mwananchi.co.tz