Unguja. Wakati Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) ikisajili miradi mipya ya uwekezaji 353 yenye thamani ya Dola za 5.5 bilioni za Marekani (Sh14.99 trilioni), uwepo wa amani na kuimarika kwa miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii vinatajwa kuvutia mitaji mikubwa ya uwekezaji kutoka nje.
Miradi hiyo iliyosajiliwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Nane, inatarajiwa kutoa ajira 20,000. Mingi kati ya miradi hiyo ni ya sekta ya utalii.
Akizungumza leo Septemba 21, 2024 wakati wa kuzindua Hoteli ya Shukran Palace, Michanvi mkoani Kusini Unguja, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema uwepo wa miradi mikubwa umechangiwa zaidi na amani na usalama uliopo Zanzibar, pamoja na sera nzuri.
“Uwepo wa amani na usalama katika nchi yetu umekuwa chachu kwa wawekezaji wengi wa kigeni kuona visiwa vyetu vya Unguja na Pemba ndiyo sehemu sahihi ya kuwekeza mitaji yao,” amesema.
Dk Mwinyi amewataka wananchi kudumisha amani na kuendelea kuiunga mkono Serikali ili uwekezaji huo katika miradi ya maendeleo uwe na tija katika kuimarisha uchumi wa Taifa.
Ameipongeza sekta binafsi nchini kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika nyanja za maendeleo ikiwemo sekta ya biashara na uwekezaji.
“Serikali inatambua mchango unaotolewa na sekta binafsi katika kusaidia maendeleo ya nchi yetu,” amesema.
Dk Mwinyi amesema wanaendelea kwa kasi kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ambayo itajumuisha shughuli za bandari ya uvuvi, uhifadhi wa mafuta na gesi, viwanda vya kusindika mazao na ujenzi wa mji wa kisasa.
Mbali ya hayo, amesema Serikali inaendelea kuimarisha na kujenga miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege, kuimarisha upatikanaji wa huduma za nishati, majisafi na salama, elimu bora, afya na huduma nyingine za kijamii.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema sekta ya uwekezaji imekuwa na mchango mkubwa katika kutekeleza falsafa na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050 yenye lengo la kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kupunguza umasikini kwa Wazanzibari.
“Katika kuthibitisha hili ndiyo mafaniko hayo ambayo yametajwa na tunaendelea kuyashuhudia,” amesema.
Amesema miradi 16 ya uwekezaji yenye mtaji wenye thamani ya Dola 377.5 milioni (Sh1 trilioni) imesajiliwa kwa ajili ya uwekezaji katika visiwa vidogo.
“Maono ya uwekezaji katika visiwa vidogo-vidogo yameanza kuzaa matunda, hatimaye mradi wa kwanza katika uwekezaji wa visiwa umekamilika katika Kisiwa cha Bawe, Unguja wenye thamani ya Dola milioni 38 (Sh100 bilioni). Tunategemea kuuzindua rasmi muda wowote kuanzia hivi sasa,” amesema.
Eneo lingine lenye mafanikio amesema ni kuifungua Pemba kama eneo la kimkakati la uwekezaji.
Amesema mfumo wa kisheria ulibadilishwa kushajihisha uwekezaji katika kisiwa hicho uliombatana na utoaji wa vivutio maalumu kwa wawekezaji.
Katika kuhakikisha uwekezaji unaokuja nchini una tija ya moja kwa moja kwa wananchi, amesema wizara inafanya utafiti wenye lengo la kutathmini ajira zilizozalishwa katika miradi ya uwekezaji na kutambua athari zake katika uchumi.
Mkurugenzi wa Mamlaka za Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saada Mohamed amesema mradi wa hoteli hiyo ni miongoni mwa miradi ya hoteli zenye hadhi ya nyota tano katika Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa na majengo 10 yenye jumla ya vyumba 100. Mradi huo umeshatoa ajira rasmi 245 kwa wenyeji.
Mkoa wa Kusini ndiyo unaongoza kupokea uwekezaji mwingi wa sekta ya hoteli.
Source: mwananchi.co.tz