Mambo manne yanayoweza kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi Tanzania

Mambo manne yanayoweza kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi Tanzania

Mambo manne yanayoweza kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi Tanzania

Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya ardhi nchini Tanzania wamependekeza mambo manne ambayo yanaweza kutumika katika kupunguza migogoro ya ardhi nchini.

Yaliyopendekezwa ni utoaji wa elimu juu ya masuala ya ardhi kwa wananchi, kutunga sera za ardhi shirikishi, kusimamia upimaji na urasimishaji wa maeneo nchini ambao unakwenda sambamba na kuainisha matumizi ya eneo husika.

Wameyasema hayo leo Jumatano, Februari 12, 2025 katika mjadala wa Mtandao wa Mwananchi X Space uliondaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ikijadili mada isemayo:“Migogoro ya ardhi inavyochangia jinai na changamoto kwenye sekta nyingine, nini kifanyike?”

Mjadala huo umefanyika ikiwa ni takribani siku wiki moja imepita tangu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma aliposema migogoro ya ardhi ndio inayozaa makosa mengi ya kijinai nchini, sambamba na kuwa chimbuko la changamoto katika uwekezaji, biashara na mirathi.

Profesa Juma aliyasema hayo Februari 3, 2025, alipozungumza katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria ambayo kitaifa yalifanyika katika Jiji la Dodoma, huku mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hoja yake hiyo, amesema iwapo suala la ardhi litawekwa vizuri, litasaidia kutatua matatizo mengi na hata Mahakama itakuwa na migogoro michache huku mingi ikiiishia kwenye usuluhishi.

“Katika uzoefu wetu tumeona kwamba, migogoro ya ardhi ndio inazaa jinai nyingi, ni chimbuko la changamoto kwenye uwekezaji, biashara, mirathi na maeneo mbalimbali,” alisema Profesa Juma.

Walichokisema wadau

Katika mjadala wa X Space, Mtaalamu wa masuala ya ardhi, Thom Mnkondya amesema Tanzania imejikita kutatua migogoro ya ardhi badala ya kutatua matatizo ya sekta ya ardhi akisisitiza sekta ya ardhi ina matatizo mengi ambayo yamekuwa yakichangia migogoro ya ardhi.

Mnkondya ametaja matatizo ya sekta ya ardhi ni uelewa mdogo wa masuala ya ardhi baina ya wananchi na viongozi wa sekta ya ardhi akisisitiza uelewa huo umechangia migogoro mingi.

“Watumishi wa sekta ya ardhi hawajui taratibu za kutoa ardhi kwa wawekezaji ndio maana unaweza kukuta mgogoro baina ya wananchi na wawekezaji, utaona madiwani na viongozi wa Serikali za mitaa wanauza maeneo ya wazi,” amesema.

Amesema ni muhimu wananchi na viongozi kupewa elimu kwa kuwa, baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia ardhi kujinufaisha kisiasa.

Maneno yake yaliungwa mkono na Mdau wa masuala ya ardhi, Antony Charles ambaye alitaka mamlaka kuna na mpango mkakati unaoweza kusaidia wananchi kujua taratibu na sheria zinazohusu masuala ya ardhi kama mashamba na viwanja.

Pia, ametaka elimu itolewe ili wananchi wajue wanapotaka kununua ardhi nini wanapaswa kufanya ili wawe salama.

“Huko kwenye ofisi za Serikali hao watendaji pia kusiwe na urasimu, umekuta kiwanja kimeuzwa mara moja, mbili, lakini unazungushwa unapigwa tarehe kinaleta migongano kwenye jamii,” amesema.

Amesema hilo linawezekana kwa Serikali kuja na mpango mkakati wa jinsi ya kudhibiti tatizo hilo ikiwemo kusambaza elimu kwa wananchi ili wajue wakipata shida wakienda wapi wanaweza kusaidiwa.

Mwandishi mwandamizi kutoka Mwananchi, Elias Msuya naye aliutama Serikali kuongeza bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili iweze kupata nguvu katika kurasimisha ardhi na kupima.

Kuhusu sera, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya HakiArdhi, Cathbert Tomitho alitama utungaji sera na miongozo katika sekta mbalimbali nchini kuwa shirikishi ili kuwezesha kumaliza migogoro ya ardhi.

Amesema ili miongozo na sera zilizopo ziwe na nguvu za kumaliza migogoro ya ardhi ni lazima iwe shirikishi lakini shida iliyopo ni mifumo ya utungaji iliyopo.

“Ukimsikiliza nguli wa masuala ya ardhi, Profesa Issa Shivji anasema chanzo cha migogoro hii tuliyonayo ni kukosekana kwa demokrasia katika sekta ya ardhi sekta ambayo imehodhiwa na tabaka tawala,” ameeleza.

Tomitho amesema mifumo iliyopo kwenye sekta ya ardhi inatoka juu kwenda chini badala ya kutoka chini kwenda juu.

Katika eneo la upimaji, Mdau wa masuala ya ardhi Fadhili Mkwachu alipendekeza Serikali kushirikiana na wadau kuongeza jitihada za kupima ardhi katika maeneo ambayo upimaji haujafanyika.

Amesema ardhi ikisajiliwa ni rahisi kutambua historia yake,mipaka na nani anaimiliki kwasababu mipaka ndio imekuwa ikichangia migogoro.

“Hili liende sawa na uwepo wa utashi wa kisiasa kwa viongozi wa juu kuwa na dhamira ya kuhakikisha ardhi ya Tanzania inasimamiwa ipasavyo,” amesema.

Uuzaji wa ardhi nao uliangaziwa ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa HakiArdhi, Cathbert Tomitho kama nchi inakosa utaratibu mzuri wa kuuza na kuna ardhi nchini Tanzania.

Hoja yake ameijenga akirejea utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere akisema kulikuwa na mwendelezo wa kuuza ardhi lakini Sheria za 1999 na kufanyiwa marekebisho 2004 ziliingiza vipengele vya kuuza ardhi pekee.

Vipengele hivyo ndivyo anavitaja kama kichocheo cha migogoro ya ardhi wakati ambapo hakuna mamlaka ya udhibiti uuzwaji wa ardhi.

“Ukitaka kununua ardhi nunua iliyofanyiwa savei, ardhi za mijini tujitahidi kununua zilizofanyiwa survey na kujiridhisha ndani ya Serikali za mitaa kama anayekuuzia ni mtu halali, pia unaweza kwenda kuangalia manispaa ardhi ni ya nani,”

Jambo lingine amesisitiza mikataba akidokeza ni muhimu kununua ardhi kwa mikataba iliyosainiwa na mawakili hai na kuepuka kununua viwanja kutoka kwa kampuni zinazouza ardhi sababu nazo zimechangia migogoro ya ardhi.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories