Makonda aagiza jengo la abiria Uwanja wa Ndege Arusha likamilike haraka

Makonda aagiza jengo la abiria Uwanja wa Ndege Arusha likamilike haraka

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema kukamilika kwa jengo la abiria uwanja wa ndege wa Arusha kutapunguza msongamano na kuongeza utulivu wa abiria.

Makonda amesema hayo baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ukarabati wa jengo la abiria katika uwanja huo ambalo ameagiza likamilike haraka na lianze kutumika Septemba mosi.

Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo, Makonda amesema kukamilika mapema kwa jengo hilo kutawezesha abiria kuwa na mahali pazuri pa kusubiri usafiri na kupunguza msongamano uliopo sasa.

Amesema shauku ni uwanja huo kukamilisha maboresho ikiwemo uwekaji wa taa za kuongozea ndege ambayo yatauwezesha kutumika kwa saa 24, tofauti na inavyotumika sasa saa 12 pekee kutokana na kutokuwepo kwa taa.

“Tumetembelea hapa kuona kazi inayoendelea na ni shauku yetu uwanja utumike kwa saa 24,na kupitia Sh7 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kuweka taa za kuongozea ndege, tunaamini mradi huo utasaidia uwanja utumike kwa saa 24,” amesema

“Kuhusu kuweka taa tumepata taarifa mkandarasi ameshapatikana na mkataba umesainiwa wa miezi 12 ila tumezungumza na mkurugenzi jana, walau miradi ukamilike ndani ya miezi minane,” aliongeza Makonda

Meneja wa uwanja huo, Godfrey Kaaya, amesema mradi wa jengo la abiria na miundombinu yake utagharimu Sh8 bilioni na umefikia asilimia 90.

Amesema jengo la abiria linalotumika kwa sasa lina uwezo wa kuhudumia abiria 150 wakati lile linalokamilishwa likitarajiwa kubeba abiria 1,000 kwa wakati mmoja.

“Tumejipanga kuhakikisha Septemba lianze kutumika kwani limeshafikia asilimia zaidi ya 90,” amesema.

Kuhusu mradi wa taa za kuongozea ndege, Godfrey amesema mkandarasi ameshapatikana na ameshaanza kazi za awali za usanifu na kuwa watasimamia mradi huo utekelezeke chini ya miezi 12, ili kiwanja hicho kiweze kutumika kwa saa 24.

“Kwa sasa kiwanja hiki kinatumika kwa saa 12 tu, ila ni kiwanja cha ndege cha pili kwa miruko mingi ya ndege Tanzania bara baada ya Julius Nyerere,” amesema

“Tuna miruko karibu 150 kwa siku. Kwa mfano kipindi hiki cha msimu wa utalii, zinakuja ndege 75 na zinaondoka ndege 75 na ndege zote ni ndani ya saa 12, tofauti na viwanja vingine ambavyo vinahudumia ndege kubwa,” ameongeza

Kuhusu ongezeko la abiria, meneja huyo amesema kwa kipindi cha mwaka 2019 kabla ya Uviko -19, kulikuwa na watalii wengi akitolea mfano Julai mwaka huo, walivyopokea abiria zaidi ya 38,000 akilinganisha na Julai 2024 walivyohudumia abiria zaidi ya 45,000.

“Hao abiria zaidi ya 45,000 asilimia zaidi ya 90 ni watalii, hivyo ni kiwanja muhimu hasa katika biashara ya utalii,” amesema.

Maboresho ya uwanja huo wa ndege ni muhimu kwani asilimia kubwa ya watalii hupita Kaskazini huku Arusha ikitumika kama lango kuu, hivyo kukamilika kwa miradi hiyo kutachochea kasi ya maendeleo kwa kiwango kikubwa.

Kwa sasa mwonekano wa kuingia katika uwanja huo umeanza kubadilika kufuatia maboresho yaliyofanywa, likiwemo eneo la maegesho ya magari ambalo limekamilika na linatumika.

Barabara ya kuingia katika uwanja huo imeboreshwa tofauti na ilivyokuwa awali, likiwa limebaki jengo la abiria linalokamilishwa na uwekaji wa taa.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories