Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrance Mafuru amefariki dunia leo, akiwa kwenye matibabu katika Hospitali ya Apollo nchini India.
Mafuru aliyekuwa mtaalamu wa fedha na uchumi maarufu hapa nchini, amehudumu katika taasisi kubwa tofauti kwa miongo miwili. Amewahi kuwa Msajili wa Hazina na Ofisa mtendaji mkuu wa Benki ya NBC Tanzania.
Pia amewahi kuwa Naibu Katibu wa Wizara ya Fedha, Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki nchini (TBA) na mwanzilishi wa mwenza wa kampuni ya ushauri wa masuala ya fedha ya Bankable.
Kufuatia taarifa za kifo chake, Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Profesa Kitila Mkumbo, watumishi wa Tume ya Mipango, ndugu jamaa na marafiki.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Bw. Lawrence Nyasebwa Mafuru, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kilichotokea leo tarehe 09 Novemba, 2024 katika hospitali ya Apollo nchini India,” amesema Samia katika salamu zake za rambirambi.
Rais Samia amesema Mafuru atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka, bidii na ubunifu alipotumikia nafasi mbalimbali ndani ya Serikali.
“Mwenyezi Mungu aijaalie familia yake subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na ailaze roho yake mahali pema”
Endelea kufuatilia Mwananchi.
Source: mwananchi.co.tz