
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa utaratibu wa misa zake ikiwemo kusitisha kupeana amani kwa mikono ili kujikinga na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox (homa ya nyani).
TEC inechukua hatua hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kuripoti uwepo wa wagonjwa wawili wa Mpox jijini Dar es Salaam ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya Mpox unasambaa kwa njia za matone ya mfumo wa njia ya hewa, ngozi kupitia kugusa na kujamiiana na mtu mwenye maambukizi.
Pia ugonjwa huo unaenea kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu.
Leo Jumanne, Machi 11, 2025, Mkuu wa Idara ya Liturujia wa TEC, Padri Clement Kihiyo ametoa taarifa fupi akisema:”Wapendwa katika Kristo,
kutokana na tahadhari ya kiafya iliyotangazwa na Wizara ya Afya, kwa upande wa Liturujia tunasitisha kwa muda maji ya baraka kwa kuchovya hadi hali itakapotengemaa. Pia tusitishe kwa muda kupeana amani kwa kupeana mikono.”
Source: mwananchi.co.tz