Dar/Dodoma. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimetoa wito kwa Serikali kuona haja ya kuridhia mkataba wa kimataifa wa ulinzi kwa watu wote dhidi ya kupotea na kutekwa wa mwaka 1994, ili kukabiliana na ongezeko la matukio ya kupotea na kutekwa watu yanayoripotiwa nchini.
Shirika hilo limesema Tanzania haijaridhia mkataba huo ili kuufanya kuwa sehemu ya sheria zake.
Mbali ya hayo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imelaani mauaji ya watu yanayoendelea nchini, ikiitaka jamii kuishi kwa kufuata sheria na kuheshimu haki ya msingi ya kila mtu kuishi.
Akizungumza Dar es Salaam leo Agosti 30, 2024 katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya waathirika wa matukio ya kutoweka na kutekwa, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema kutokana na ongezeko la matukio hayo nchini, hiyo ni sababu tosha ya kuifanya Tanzania kuridhia mkataba huo ili kuweka ulinzi thabiti kwa wananchi.
“Manufaa ya mkataba huu katika ibara ya kwanza unabainisha na kuweka katazo la watu kuwekwa vizuizuini na matukio ya kutekwa kuwa ni kinyume na ulinzi wa haki za binadamu.
“Ibara ya pili mkataba unatafsiri vitendo vya kutoweka na utekaji ikijumuisha vitendo vya kutekwa, kuwekwa kizuizini au namna yoyote ya kumnyima mtu uhuru iwe kwa kufanywa na serikali, vyombo vyake au kwa maelezo ya serikali kwa kuelekeza chombo au mtu kuficha taarifa za alipo mtu aliyekamatwa au kutekwa,” amesema.
Amesema ibara ya sita ya mkataba huo inataka mamlaka kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki na kuwafikisha watu wote waliohusika na matukio ya kuficha taarifa za mtu aliyetekwa katika vyombo vya kisheria.
“Ibara ya 24 ya mkataba huo inaweka sharti kwa mamlaka husika zilizoridhia mkataba huo kutoa fidia kwa waathirika wote wa matukio ya utekaji ikiwemo, kutoa fedha za matibabu, fidia ya madhila na huduma ya kisaikolojia kwa waathirika na familia zao,” amesema.
Pamoja na ulinzi uliowekwa na ibara za 14 na 15 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 katika kulinda haki ya kuishi na uhuru wa mtu, amesema ni wakati kwa Serikali kuridhia sasa.
“Kuridhia mkataba huu si tu itaonesha kujizatiti katika jumuiya ya Umoja wa Mataifa kudhibiti vitendo hivyo, bali itaongeza imani kwa wananchi juu ya ulinzi na usalama wao,” amesema.
Amependekeza hatua zingine zinazopaswa kufanywa na dola ni kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama katika ngazi za jamii kwa kushirikiana na wananchi ili kudhibiti matukio hayo.
“Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama ifanye uchunguzi wa kina wa malalamiko dhidi ya matukio hayo, hususani katika kipindi cha hivi karibuni,” amesema.
Mauaji ya watu
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji mstaafu Mathew Mwaimu amesema tume inalaani mauaji ya watu yanayoendelea nchini, akiitaka jamii kuishi kwa kufuata sheria na kuheshimu haki ya msingi ya kila mtu kuishi.
Jaji Mwaimu ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Agosti 30, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio ya mauaji yanayoendelea jijini Dodoma.
Amesema hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la mauaji ya kutisha yanayoripotiwa na vyombo vya habari na Jeshi la Polisi.
Amesema tume inalaani wimbi la mauaji, baadhi yakitokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi.
“Pamoja na Serikali na wadau kulaani vitendo hivyo mauaji hayo yameendelea kushika kasi licha ya Jeshi la Polisi kufanya jitihada za kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,” amesema.
Baada ya kufuatilia mauaji hayo, tume imebaini kujengwa tabia za baadhi ya wananchi kutozingatia sheria za nchi na kujichukulia sheria mkononi.
“Katika baadhi ya mauaji yaliyotokea kuna viashiria vya ulipaji kisasi, wivu wa mapenzi, imani za kishirikina na baadhi ya wananchi wanajenga imani kuwa wanaweza kutenda uovu na wasikamatwe,” amesema.
Amesema baadhi ya wananchi hawana imani na vyombo vya usimamizi wa sheria na haki, na uwepo wa wananchi wasiopenda kufanya kazi halali na hivyo kuwa na tamaa ya mali.
Ili kukabiliana na matukio hayo, tume imependekeza Jeshi la Polisi liendelee kuchukua hatua mahususi kuimarisha mifumo ya ulinzi kwenye maeneo ya wananchi kuwezesha upatikanaji wa taarifa za mapema kuhusu kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa sheria vinavyosababisha mauaji na vitendo vya ukatili kabla matukio hayo kutokea.
“Jeshi la Polisi liendelee kuchukua hatua kuhakikisha watu wote wanaohusika na mauaji hayo wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo,” amesema,
Mamlaka katika ngazi zote zimetakiwa kuwa na mipango madhubuti kuhakikisha zinakuwapo taratibu za kuimarisha ulinzi na usalama wa raia kwa kushirikiana na Polisi.
Viongozi wa dini wametakiwa kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya dini, maadili na kukemea uovu.
Wananchi wametakiwa washirikishe vyombo vya dola wanapoona maovu yakitendeka ndani ya jamii na kufichua uvunjifu wowote wa sheria na haki za binadamu.
Tume imependekeza asasi za kiraia na vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa umma, kuhusu taratibu zilizopo za namna ya kushughulikia masuala ya kijamii kupitia sheria.
Source: mwananchi.co.tz