Kipanya kumburuza Mwijaku kortini Septemba, kudai fidia ya Sh 5.5 bilioni

Kipanya kumburuza Mwijaku kortini Septemba, kudai fidia ya Sh 5.5 bilioni

Dar es Salaam. Mchora katuni maarufu na mtangazaji wa Clouds Media Group nchini Tanzania, Ally Masoud maarufu Masoud Kipanya, amemfungulia kesi Mtangazaji wa Crown Media Ltd, Burton Mwemba Mwijaku, akidai fidia ya Sh5.5 bilioni kwa kumkashifu na kumshushia hadhi na heshima yake kupitia maandishi aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Masoud amefungua kesi hiyo Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ndogo ya Dar es Salaam dhidi ya Mwijaku, akiomba nafuu 12 ikiwemo kulipwa fidia kwa kumkashifu mtandaoni.

Tayari, Mwijaku ameshapelekewa wito wa kuitwa mahakamani hapo uliosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo jana Jumatano, Agosti 7, 2024 ambao unamtaka kuwasilisha maelezo yake ya utetezi ndani ya siku 21 tangu alipopokea wito huo.

Masoud kupitia wakili wake kutoka kampuni ya Haki Kwanza Advocates, Alloyce Komba amefungua maombi hayo namba 18911 ya mwaka 2024 na kusajiliwa Agosti 5, 2024 na mahakama hiyo.

Mwananchi imefanikiwa kuyaona maombi hayo, leo Alhamisi Agosti 8, 2024 pamoja na wito wa Mwijaku kuitwa mahakamani hapo.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Septemba 3, 2024, saa tatu asubuhi mbele ya Jaji David Ngunyale wa Mahakama hiyo.

Katika kesi ya msingi, Kipanya amemshtaki Mwijaku kwa kumkashifu kwa maandishi Juni 4, 2024 kupitia ukurasa wake wa Facebook wenye utambulisho namba 108657908847651 na kwenye akaunti yake ya Instagram aliandika maneno ya uongo yenye nia ovu na kumfedhehesha yakiwemo kwamba yeye KP anafanya biashara haramu inayoharibu maisha ya vijana wengi nchini.

Katika hati hiyo ya mashtaka, Mwijaku anadaiwa kuandika kwenye akaunti za mitandao tajwa kwamba Masoud huwazodoa na kuwadhalilisha viongozi wa nchi na Serikali hususani marais kwa kuhongwa.

Kipanya anadai maneno hayo ya uongo na yenye nia ovu yaliyochapishwa mitandaoni na kusomwa na watu wengi ndani ya jamii na duniani yametafsiri kwamba yeye KP siyo mtu mwenye tabia nzuri wa kupewa heshima yoyote kwani hafai, anajihusisha na biashara haramu kama dawa za kulevya au nyara za Serikali au magendo.

“Hivyo kipato chake kinatokana na biashara hiyo haramu na siyo uchoraji katuni, utangazaji, ubunifu, ubalozi wa masuala ya kijamii, ukurugenzi wa bodi za taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa,” imedai sehemu ya hati ya mashtaka.

Hata hivyo, Kipanya kupitia wakili wake Alloyce Komba, amechambua katika vipengele 15 akifafanua maana ya maandishi ya Mwijaku kwa tafsiri ya watu wa kawaida ndani ya jamii kwamba mteja wake anaonekana ni mla rushwa, jambazi, tapeli, laghai, asiyeaminika, chanzo cha vijana walioharibikiwa maisha yao.

Pia, mteja wake hapaswi kuhusishwa katika masuala yoyote ya kijamii ikiwemo kupewa fursa na kufanya kazi na taasisi za Serikali ambazo amekuwa akijihusisha nazo katika elimu na malezi ya vijana mashuleni na mitaani.

Mambo 12 aliyoomba kipanya

Wakili Komba amedai kutokana na maandishi ya kashfa ya meneno ya uongo aliyotoa Mwijaku na kunukuliwa akikiri na kuomba radhi mbele ya vyombo vya habari Juni 13, 2024 bila kuchukua hatua ya dhati ya kumsafisha kimaandishi Masoud Kipaya, imeathiri kiajira, kibiashara, kimahusiano ndani ya jamii ya Tanzania kuanzia kwenye familia yake, kisaikolojia na kumshushia hadhi na heshima aliyoijenga kwa zaidi ya miaka 35.

“Hivyo mteja wangu anaomba mahakama imuamuru Mwijaku, amlipe fidia ya Sh500 milioni ya madhara halisi (specific damages) atakayothibitisha kwa ushahidi mahakamani kutokana na kashfa hiyo na fidia ya madhara ya jumla (General damages) yatakayopimwa na kuridhiwa na mahakama kwa mamlaka yake ya Sh5 bilioni,” amedai Wakili Komba.

Pia, wakili Komba alidai mteja wake, ameomba malipo ya kiadhabu kwa mdaiwa yaani punitive dameges na malipo ya fidia ya madhara halisia yaambatane na riba ya asilimia 31 tangu kashfa ilipotolewa yaani Juni 4, 2024 hadi utekelezaji wa hukumu utakapokamilika.

Vilevile Kipanya anaiomba mahakama katika hukumu yake, itamke kwamba maneno yaliyoandikwa na kusambazwa na Mwijaku yalikuwa ni ya uongo, yenye nia ovu na kuharibu hadhi na heshima yake.

Kipanya, pia anaoimba mahakama iamuru Mwijaku kuomba radhi bila masharti yoyote na kuondoa mitandaoni maneno ya kashfa yaliyoandiskwa na kusambazwa.

Ombi lingine, Kipanya anaiomba mahakama itamke na kumuamuru Mwijaku, wakala wake, wasaidizi wake na mtu mwingine yoyote aliye katika mamlaka yake kutosambaza maneno hayo ya uongo na kashfa dhidi ya Masoud Kipanya.

Mchora katuni huyo, pia ameomba kulipwa gharama ya kesi kutokana na kuajiri mawakili na nafuu nyingine ambazo mahakama itaona ni haki na zinafaa apewe.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories

Zanzibar Commerce
Top News
Investment News Editor

Zanzibar Airports Authority enforces Dnata monopoly

. Airlines that have not joined the Zanzibar Airports Authority’s (ZAA) preferred ground handler, Dnata, at the Abeid Amani Karume International Airport (AAKIA) face eviction from the Terminal Three building Dnata is the sole ground handler authorised to provide services for flights that operate at Terminal 3.Continue Reading